Habari

Waislamu waijia juu serikali ya Rwanda baada ya kupiga marufuku Adhana

Kigali, Rwanda.

Marufuku ya matumizi ya adhana (wito kwa waislamu wa kuingia misikitini kuswali maombi) katika tarafa moja ya mji wa Kigali nchini Rwanda imepingwa vikali na baadhi ya waislamu jijini humo.

Utawala katika tarafa ya Nyarugenge kunakopatikana jamii kubwa ya waislam nchini humo, umebainisha kuwa kumekuwepo kwa muafaka wa kubadili mbinu za kuwaita waumini bila ya matumizi ya njia hiyo ambayo inatajwa kuwasumbua wananchi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa mjini Kigali, John Gakuba amesema wito huo wa waislamu kuhudhuria maombi umetajwa kuwa kero miongoni mwa wananchi.

Tayari mkataba wa kuhakikisha kuwa mwafaka huo unaheshimiwa umetiwa saini kati ya viongozi wa msikiti na utawala wa eneo hilo.

Wito huo wa maombi miongoni mwa jamii za waislamu kote duniani hutumia vipaza sauti na hufanyika mara tano kwa siku.

Licha ya utawala wa eneo hilo kudai kwamba kumekuwa na mwafaka kutoka pande zote mbili, lakini baadhi ya Waislamu waliohojiwa wameonyesha kuwa na hisia tofauti.

Kulingana na katibu mtendaji wa tarafa hiyo ya Nyarugenge, amri hiyo iliagizwa yapata miaka miwili iliyopita lakini ikapuuzwa mbali na Waislamu.

”Pengine wakati ule sababu ambazo watu hawakupokea vyema ujumbe ambao haukuwa umeelezewa sawa sawa ,lakini leo baadhi ya makanisa yalilazimika kufunga milango baada ya kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi huku misikiti yenye vipaza sauti na makanisa yenye kengele tukiyataka kutotumia mtindo huo. Mtu aliye lala akiishi jirani na kengele hiyo inampigia kelele. Kwa hiyo ni uamuzi unaohusu pande zote mbili na ni matarajio yetu kuwa hakuna aliyenyimwa haki,” alisema katibu mtendaji huyo.

Naye mshauri wa Mufti wa Rwanda, Sheikh Mbarushimana Suleiman alisema kuwa hatua hii ya kuzuiliwa kwa matumizi ya adhana misikitini inafuatia operesheni inayoendelea ya kufungwa kwa makanisa zaidi ya mia saba ambao yaliripotiwa kuwa hayajatimiza kanuni za ujenzi na amri ilitolewa kwanza kutimiza masharti ili yapewe tena kibali cha kufanya huduma ya kikanisa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita wiki mbili tu tangu mamlaka jijini la Kigali kuyafunga makanisa zaidi ya 700 kwa madai ya kuzuia kelele zilizotokana na vipaza sauti wakati wa ibada.

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Mama Maggie apewa tuzo ya heshima kwa kuanzisha taasisi ya kikristo kwenye nchi ya kiislamu.

Next post

Audio: Silvabel - Washa