Connect with us

Tamasha la miaka 30 ya CVC kukutanisha kwaya kongwe

Habari

Tamasha la miaka 30 ya CVC kukutanisha kwaya kongwe

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Kwaya ya AICT Changombe Choir, maarufu kama CVC, ya jijini Dar es Salaam, Jumapili ijayo Aprili 29 inatarajia kufanya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, tukio ambalo litakutanisha kwaya maarufu zinazokonga nyoyo za Wakristo wengi na wapenzi wa nyimbo za injili ndani na nje ya nchi.

Kwaya zitakazoshiriki maadhimisho hayo ambayo yataenda sambamba na tamasha la uimbaji ni: Kinondoni Revival ya Kanisa la TAG Kinondoni, Tumaini Shangilieni kutoka Arusha, KKKT Uinjilisti Kijitonyama, Sonda ya Dilu kutoka kanisa la SDA, KKKT Ukombozi kutoka kanisa la KKKT Msasani, AICT El Shadai ya AICT Mbagala, AICT Dar es Salaam ya AICT Magomeni; pamoja na kwaya zote zilizo chini ya Kanisa la AICT Changombe.

Katibu Mtendaji wa CVC, Hosea Kashimba amesema kuwa, maadhimisho hayo yataanza Jumamosi Aprili 28 kwa kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha mikutano cha kwaya hiyo kinachojulikana kama CVC Centre katika eneo la Mtoni Kijichi.

Amesema, jiwe la msingi litawekwa na Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Dayosisi ya Pwani, Charles Shilagi Salala.

Amesema Aprili 29 maadhimisho yataanza kwa ibada maalum ya uzinduzi wa DVD ya maadhimisho, na baadaye mchana kutakuwa na tamasha la uimbaji ambalo litajumuisha kwaya zote hizo.

Kashimba amesema, maadhimisho hayo yataambana na uchangiaji fedha kwa ajili ya kufanikisha maono ya ujenzi wa CVC Centre ambao unaendelea. Mradi huo unatarajiwa kuwa chanzo cha mapato kwa kwaya hiyo pamoja na kutoa ajira kwa vijana.

Katibu mtendaji huyo alisema kuwa, pamoja na kwaya hizo maadhimisho hayo pia yanatarajiwa kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa kanisa na taasisi mbalimbali.

Katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1988, CVC imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutoa nyimbo mbalimbali ambazo zimefanyika kuwa baraka kubwa kwa watu. Miongoni mwa albamu zake ambazo zimejipatia umaarufu ni pamoja na Gusa, Vunja, Gusa, Jihadhari na Mpinga Kristo na Usiku wa Manane pamoja na Pazia.

Pamoja na mradi wa ukumbi wa mikutano wanaoendelea kujenga, kwaya hiyo pia inamiliki studio inayojulikana kama CVC Studio ambayo ipo katika eneo la kanisa la AICT Changombe, Barabara ya Mandela, ambayo imeajiri baadhi ya waimbaji.

Chanzo: Mwanzo News

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Habari

To Top