SOMO LA FRED MSUNGU: MAJIRA, KUSUDI NA UKOMO WAKE SEHEMU YA NNE. - Gospo Media
Connect with us

SOMO LA FRED MSUNGU: MAJIRA, KUSUDI NA UKOMO WAKE SEHEMU YA NNE.

Mafundisho

SOMO LA FRED MSUNGU: MAJIRA, KUSUDI NA UKOMO WAKE SEHEMU YA NNE.

NAFASI YA MAONO NA IMANI KATIKA KULIELEKEA KUSUDI.

(Kwanini maono na imani ni muhimu kwenda sambamba na umuhimu wake ni upi?)
Katika safari ya kuelekea majira ya kusudi kuna vitu ambavyo ni muhimu sana ambavyo ndivyo vinavyoweza kuleta yale matokeo ya kusudi kuonekana kwa macho ya kawaida.
Maono vikiambatana na imani naweza kusema hawa ndio wazazi au mama wa kusudi kwasababu huwezi kufikia kusudi kama hukuwa na maono, na sio kuwa na maono tu bali ni kuwa na maono na kuyakubali na kuyaamini bila kujali mazingira yanaongea nini kwa wakati huo. Hivyo Mungu anatakiwa kuhusika kwa asilimiia zote katika kila hatua unayochukua kwani yeye huona mwisho wetu hata kabla ya mwanzo kwasababu mwisho wa safari ni kitu cha muhimu ambacho msafiri anatakiwa kukifahamu hata kabla ya mwanzo wa safari yako kwasababu ni rahisi sana kupotea kama umeanza kusafiri bila ya kujua utaishia wapi, na kitu pekee kinachoweza kukuonesha hatima yako ni Mungu pekee. Pia ni muhimu sana kujua hakuna mtu ambaye yeye mwenyewe anapanga kuona au kuwa na maono makubwa, Maono huletwa na Mungu mwenyewe moja kwa moja kwa muhusika kupitia njia mbali mbali kwa hiyo kwa namna moja ya au nyingine naweza kusema ni neema tu ya Mungu ambayo huweza kuleta maono kwa mtu na sio fedha au umaarufu na vitu vingine kama watu wengi ambavyo wamekua wakidhani.

Mfano: Kuna watu wengi ambao wana fedha nyingi za kutosha kufanya vitu vikubwa sana na wakati mwingine pengine tuliwategemea kuwa ndio watu ambao watavunja rekodi mbalimbali kwa kufanya mambo makubwa katika jamii, Lakini mara nyingi haijawa hivyo kama tulivyotarajia Unaweza kujiuliza ni kwanini? Jibu ni rahisi sana…Umaarufu au fedha haiwezi kuzaa maono, Lakini maono yanauwezo wa kuzaa fedha na umaarufu. Maono kwa lugha rahisi ni tarajio lililo ndani ya ufahamu wa mtu au ndoto ambayo inakupa picha ya mbele ikiwa na majira/kusudi au sababu ya kuwepo kwa hayo maono. Hichi ni kitu muhimu sana kwasababu mtu mwenye maono ni lazima aione hatima ya maono yake kwanza kabla ya kutembea katika maono ili aweze kutimiza kusudi la maono. Katika safari ya kuelekea majira ya udhihirisho, Watu wengi wamefeli mapema sana kwasababu waliianza safari wasiojua mwisho wake ni upi(kutokuwa na maono) Hii ni hatari sana kwasababu utajikuta unaishia popote tu kwasababu huna uhakika wa wapi unatakiwa uishie(hatima) Kuna uwanja mpana sana katika maono ambapo ndani yake lazima kuwe na imani ambayo ni kama mafuta ambayo yatakusaidia kutembea katika lengo mpaka kuufikia wakati wa majira yako ambapo yale maono yanakuwa kitu halisi kilichodhihirika kwa macho ya nyama na kila mtu sasa anaweza kuona matokeo ya uhalisia wake, Na punde unapoyajua maono yako ni nini hapo ndipo safari ya kuelekea majira yako ndipo inapoanza. Kutimia kwa maono yako hiyo ndio alama kubwa ambayo utaiacha na ndio uthibitisho wa uwepo wa majira yako.

VITU VYA KUZINGATI UKISHAYATAMBUA MAONO (KUSUDI)
(1)kutumbea katika maono (kutunza maono)

Kutunza maono ni kitu cha muhimu sana kwasababu katikati ya safari kuna wakati mazingira yanaweza kusema kinyume kabisa na vitu unavyovitarajia au ulivyoviona, Ninaposema mazingira namaanisha kunaweza kukajitokeza tatizo au pingamizi la aina yoyote katika mazingira yaliyokuzunguka ambayo kwa namna moja au nyingine yanachangia uwepo wako kwa wakati ule. Vitu vinavyoweza kusimama kama vikwazo ni kama taizo la kifedha, upinzani kutoka kwa watu wanaokuzunguka au hata wakati mwingine hali yako halisi kama vile mazingira ya familia unayotoka au afya yako pia kuna wakati inaweza kupingana na maono ambayo Mungu ameweka ndani yako. Lakini kitu cha muhimu unachotakiwa kukumbuka hapa ni kuwa wewe ndie mwenye maono yaliyokamilifu katika ufahamu wako. Kwa maana nyingine naweza kusema ile picha halisi ya kitu unachokitarajia ni wewe pekee ndiye unayeijua, Kwasababu hili ni swala la mtu binafsi (mbeba maono) na Mungu bila kumuhusisha mtu mwingine yeyote. Hivyo unatakiwa kuwa mwangalifu sana na watu wanaokuzunguka wanazungumza nini juu yako au mazingira yanasema nini kwa wakati huo, Simaanishi ni vibaya kupokea ushauri kwa watu bali unatakiwa kuwa na mlengo ambao utakuongoza kuhakikisha kwamba hutoki nje ya lengo. Unatakiwa kuelewa kitu kimoja cha msingi sana hapa kwamba katika maono kuna aina mbili za kweli.

1. Kweli ya nje:
Hii ni ile hali ya kuyaona mazingira jinsi vile yalivyo au yanavyoonekana kwa macho ya nyama. Mfano:Unaweza kuwa na maono ya kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa lakini kwa wakati huo hauna hata mtaji unaweza kukufanya pengine kujitosheleza hata kwa mahitaji ya kawaida kabisa, Kwa lugha rahisi naweza kusema wewe ni mtu duni au wa hali ya chini. Na huo ndo ukweli wa nje jinsi unavyoonekana na ndivyo ilivyo katika mazingira hayo.

2. Kweli ya ndani:
Kweli ya ndani ni ile hali ya kusikia kitu chenye msukumo mkubwa ndani yako kikikanusha hali halisi ya mazingira ya nje na kuumba mazingira ya kitu halisi ambacho hakijadhihirika nje bado kwa wakati huo lakini ikielekeza mkazo na imani yako kwa mlengo wa kitu husika. Mara nyingi umuhimu wa kweli ya ndani huwa ni kuumba imani ambayo hapo awali tumeona kwamba ni mfano wa mafuta yatakayo kusaidia kufika mahali hatima yako ilipo.

Tumeona kweli za aina zote mbili hapo lakini nataka kutilia mkazo sana katika kweli ya pili ambayo ni kweli ya ndani, Au kwa maneno mengine tunaweza kuiita imani.
Kweli ya ndani ni kitu cha muhimu sana kwa mtu anaeyaelekea majira yake ya udhihirisho kwasababu ni kitu ambacho kinamuonesha jinsi alivyo na jinsi atakavyokuwa.

-Kwanini kweli ya ndani ni ya muhimu kuiamini?
Ni muhimu sana kuiamini kweli ya ndani kwasababu ndio inauwezo wa kuona mwisho wako tofauti na kweli ya nje au kweli ya mazingira ambayo hiyo inatathimini hali yako ulionayo sasa. Ni sawa na ujenzi wa ghorofa, mwanzo wa ujenzi wa ghorofa ni sawa kabisa na ujenzi wa nyumba nyingine ya kawaida kabisa kwasababu vyote huanza na msingi. Sasa kwa mtu asiyehusika na ujenzi ule akipita kwa mara moja na kuuona msingi kwa wakati ule anaweza kujitia ujasiri na kusema kwamba nyumba inayojengwa pale ni ya kawaida kama nyumba nyingine kwasababu hiyo ndio hali aliyoiona kwa wakati ule, Na kwa hakika hiyo ndio hali halisi kwa wakati huo. Lakini itakuwa tofauti sana kwa muhusika wa ile nyumba au mwenye ramani nzima kwasababu ni kweli hata yeye kwa wakati ule atauona msingi ni wa kawaida kama Yule wa awali ambavyo aliona lakini atakuwa na uhakika kichwani mwake kwamba kitakachojengwa pale si nyumba ya kawaida bali ni ghorofa. Utaona kwamba huyu muhusika wa hii nyumba ameenda mbali zaidi na kuona mwisho wa ile nyumba japokuwa ipo katika hatua ya mwanzo kabisa ya msingi. Na hii ni kwasababu anauhahika kabisa na ile ramani alionayo na kwasababu yeye ndiye muhusika wa eneo hivyo anaelewa lengo lake ni nini.
Kwa kupitia mfano huo unaweza ukaona jinsi ambavyo msafiri au mbeba maono jinsi anavyotakiwa kuiamni kweli ya ndani kuliko ya nje kwasababu kweli ya ndani ina majibu ya hitimisho au ina picha ya kitu kamili wakati kweli ya nje inakuja na picha ya wakati husika ambayo ni ya kitambo tu.
Na hii ndio sababu kubwa ya kwamba hutakiwi kumruhusu mtu yeyote kusema au kuamua kuhusu hatima yako kwasababu hajui mwisho ni nini ila atakachokiona kwa wakati huo ni yale mazingira ya wakati uliopo ambayo ni ya kitambo kidogo. Lakini unatakiwa kumtazama Mungu ambae pekee ndie mwenye ramani nzima ya maisha yako kwa maana nyingine anajua mwanzo na hata njia utakazozipitia mpaka mwisho wako na si mazingira ya wakati uliopo.

Itaendelea……..!

Kuna wakati ambapo mazingira yamenena kinyume na maono ya mtu binafsi na kwa kutokujua tumejikuta tukianguka au tukiyafuata mazingira badala ya ahadi ya Mungu juu ya kile ambacho amekiweka ndani yako na kukifunua kwako kwa njia ya ndoto, kuona na wakati mwingine hata kwa sauti ya kusikika kwa masikio. Hata siku moja usiyaruhusu mazingira yakawa mbadala wa maono yako kwasababu mazingira ni rahisi sana kupotosha ule ukweli wa ndani. Wakati huu unaweza usieleweke sana hata na watu wa karibu yako wanaokuzunguka kwasababu kuna wakati huwa kuna nafasi fulani zinaweza kujitokeza kama bahati au kitu ambacho kinaweza kukuharakisha kukupeleaka kwenye hatima yako, Na ni kweli vitu hivyo huja na sura ya kupendeza sana kwa nje kiasi kwamba unaweza ukashawishika, Lakini kama viko nje ya lengo hata kama ni vizuri kiasi gani unatakiwa kuwa na nidhamu na mlengo wako kwasababu ni kweli vinaweza kuwa ni vizuri lakini havitakufikisha kwenye lile lengo ambalo Mungu aliliweka ndani yako. Hapa unaweza usieleweke sana hasa na watu wanaokuzunguka kutokana na kitu kinachoweza kuonekana kwamba kuchezea muda au kutojali fulsa zinazojitokeza, Kitu muhimu unachotakiwa kukumbuka katika wakati huu ni kwamba wewe ndiye uliyeona picha ya kitu unachotaka kiwe kwa hiyo hakuna mtu mwingine yeyote ambaye anaweza akawa na jibu sahihi la ukamilifu wa maono yako zaidi yako wewe na Mungu, ukilitambua hili itakuwa rahisi sana kwako kutoendeshwa na mazingira bali utatembea katika lengo, mfano rahisi ni huu gari aina ya corolla 110 na benz ukiangalia kwa haraka umbo lake ni kama gari ambazo zinafanana lakini ukija katika uhalisia ni gari aina mbili tofauti sana ambazo hazifanani kwa chochote kuanzia utendaji mpaka gharama. Sasa hivyo ndivyo mazingira yanavyoweza kuongea katika maono yako au hata watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti juu yako na wengine wanaweza wakaja na uzoefu wao wa walioyapitia na walipofika si vibaya kijifunza kutoka kwa wengie lakini ni jambo la busara zaidi kuitambua thamani yako na ya mtu unayejifunza kwake. Kwasababu ukweli ni kwamba si kila mtu anaweza kuwa ni mfano mzuri kwako kwasababu tunazidiana viwango vya maono pia kwa hiyo ukijipima kwa mtu aliyechini yako jibu lake ni kupata matokeo ya chini pia, Ni kweli corolla nayo ni gari na inaweza kukutoa mahali pamoja mpaka pengine lakini ukweli wa ndani ni kwamba huwezi ukaifananisha na Benz kwasababu ni vitu viwili ambavyo vimezidiana kiwango kwa hali ya juu sana. Vivyo hivyo kwenye maisha yetu ndivyo ilivyo usiruhusu mtu yeyote aseme chochote kuhusu wewe(fikra sahihi hutokana na watu sahihi) Ukifanikiwa kutembea katika lengo na ukafanikiwa kuyatimiza maono katika uhalisia ambapo kila mtu anaweza kuyaona na kushuhudia utendaji wake kazi hapa sasa ndicho kipindi ambacho kila mtu anaweza akakuelewa ni kwanini ulivikataa vitu ambavyo vilionekana kama ni mbadala unaoweza kukufanikisha na pia linaweza kuwa ni somo pia kwa watu waliokushuhudia tangu mchakato ulipoanza kuchakata mpaka wakati wa udhihirisho wa kile kitu ulichoona kwa miaka mingi kinapokuja kuwa wazi machoni kwa watu wote.

Fred Msunguxc

FRED MSUNGU

PURE MISSION | +255653318117

(C) 2016

 

Like Page yetu ya facebook >>>> GOSPOMEDIA

More in Mafundisho

To Top