Habari

Shepherd Bushiri: Nabii kutoka Malawi anayedai kutenda miujiza na kuwavuta maelfu ya waumini

Huyu ni Nabii anayesema kuwa ana dawa ya walioathirika na virusi vya ukimwi, HIV, anawaponya vipofu, maskini wanakuwa matajiri, na kuna wakati hivi karibuni anadaiwa kuonekana akitembea hewani.

Nabii Mchungaji Bushiri alizaliwa na kulelewa mjini Mzuzu kaskazini mwa nchi ya Malawi. Siku hizi, hujaza viwanja vya michezo kwa maelfu ya wafuasi wake, wafuasi ambao wako tayari kusafiri hadi popote pale duniani kwa ajili ya kumtazama akihubiri yeye mwenyewe.

Amekuwa akitembelewa mara kwa mara na wageni kutoka Marekani, Uingereza hata bara la Asia, ambao hata leo Bendera zao zinapepea kwa mbwembwe ndani ya ukumbi wa kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG). Maana ya jina la kanisa hilo ni Mkusanyiko wa Wakristo Waliookoka

Nakutana na mtu huyu anayefahamika kwa jina ”Mkuu” ndani ya Kanisa mjini Pretoria Afrika Kusini.

Tulipokewa kuelekea mahala patakatifu, pakiwa pametandikwa kitambaa chekundu na zulia jekundu pembeni wamejipanga walinzi.

Kumponya mlemavu

Mhubiri huyu mwenye miaka kama 30 na zaidi hivi anafahamu fika kuhusu shutuma dhidi yake kwa baadhi ya watu wakimuita msanii na mhubiri bandia, lakini amekua akizipuuzia mbali hayo yote.

”Kanisa langu si kwa ajili ya kila mtu, isipokuwa kwa wale wanaoamini,” alinieleza.

”Mimi ni mjumbe wa kazi ya Mungu. Mungu huwaponya watu kwenye kusanyiko letu”.

”Kuna siku nilikuwa na madaktari hapa Pretoria walileta watu wenye virusi vya Ukimwi, waliwapima kabla kuthibitisha kuwa wameathirika. Niliwaombea na sasa hawana virusi tena.”

Wafuasi wengi wanaamini si tu mchungaji huyu kajazwa na nguvu ya utume, lakini pia ana nguvu ya kuponya wanaougua na kuwaombea watu kuwa na mafanikio.

”Miujiza na mafundisho ambayo baba yetu (Nabii Bushiri) hufundisha kila juma ni ya kustaajabisha,” anasema Xolani Msibi kijana wa miaka 24.

Alisema dada yake alikuwa na shida ya kutembea na kuwa aliponywa na nabii ”bila hata kumuwekea mkono”

”Mwenyewe nimekuwa nikihangaika kupata kazi na nilikuja hapa nikapata kazi mbili kwa wakati mmoja ilikuwa suala la kuchagua tu”.

Wahubiri wengine wanaodai kufanya miujiza

Wanawake na wanaume wanaodai kufanya miujiza hawako Afrika Kusini pekee au Afrika pekee wanapatikana katika maeneo mengi duniani.

Benny Hinn, Kiongozi wa Kanisa la Israel lililo na makazi yake nchini Marekani, Grace Copeland na Rienhard Bonnke wa Ujerumani, hao ni wachache tu.

Baraka zimewavuta wafuasi wengi

Nabii Bushiri ana maelfu ya wafuasi, hapa walikusanyika kwenye uwanja unaotosha watu zaidi ya 95,000.

Kwa siku ya kawaida, Jumapili kanisani kwa Bushiri, watu takriban 40,000 hukusanyika kumsikiliza Nabii akihubiri, kisha hununua bidhaa zinazouzwa kanisani kama vile” mafuta ya muujiza’, kalenda, vibandiko vya mkononi na taulo zeye picha, fulana na kofia, vyote vikiwa na picha ya uso wake.

Wauzaji huwaambia wanunuzi kuwa bidhaa zote hizo zimeombewa na Bushiri mwenyewe na vina nguvu ya uponyaji, Kwa miaka mingi Bwana Bushiri amejipatia utajiri mkubwa, Vipi kuhusu wanaohoji amepata wapi pesa zote hizo? “Ubaguzi wa rangi huo,” anasema.

Shepherd Bushiri ni nani?

Nabii Shepherd Bushiri

  • Ni “nabii” mzaliwa wa Malawi aliye na makanisa mataifa mengi Afrika, miongoni mwake Ghana, Afrika Kusini na Tanzania.
  • Anadaiwa kupigwa marufuku nchini Botswana kutokana na “pesa za miujiza”
  • Anadai kwamba amewatibu watu wenye Ukimwi
  • Alidaiwa kutembea angani kwenye video iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii
  • Ana ndege nne binafsi.

Moja ya ndege za kibinafsi za Nabii Bushiri.

Hakuna hasa rekodi ya utajiri wake wote lakini inafahamika amekuwa akipata faida kwenye migodi kadhaa na anamiliki ndege binafsi na hoteli kadhaa kwa jina la kampuni yake ya uwekezaji Shepherd Bushiri Investments, makao makuu yake yakiwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Suala la yeye kupata utajiri huo kwa madai ya ujasiriamali haliaminiki

Mwenyewe alisema ”Mimi ni mfanyabiashara. Hiyo ni kando na kuwa Nabii. Mafanikio yamekuja kutokana na biashara zangu binafsi. Maswali ya namna hiyo hayaulizwi kwa viongozi wa makanisa ya wazungu, lakini mwafrika akifanikiwa ni tatizo.”

Kisha kidogo anaonyesha kuchukizwa, anaongeza ”inakuwaje kuuza bidhaa kanisani mwangu iwe tofauti na kanisa katoliki kuuza Rozari na makanisa ya Uingereza kuuza Biblia? hii si sawa. Kufanikiwa kwangu ni kioo kwa wafuasi wangu. Wanafikiri kama Mungu anaweza kunitendea mimi, anaweza kuwatendea wao pia. Kama waliamini kuwa kuna shida kwenye hilo basi wasingenifuata”.

Bidhaa za Nabii Bushiri kama vile mafuta ya muujiza huuzwa nje ya Kanisa.

Kupokea vitisho

Amekuwa akipokea vitisho kwa wale wanaomuona kuwa mshindani wao, wengine wamekuwa na wasiwasi namna ambavyo watu wamekuwa wakitumia pesa kwenye kanisa.

Kumekuwa na sheria nchini Afrika Kusini kuhusu makanisa ya kisasa, nako pia nchini Botswana Kanisa la Bushiri limefungwa kutokana na kutumia kile kinachodhaniwa kuwa ni ”pesa za muujiza” ambako kunakiuka sheria za matumizi ya pesa nchini humo.

Thoko Mkhwanazi-Xaluva ni mkuu wa Tume ya kulinda tamaduni, dini na lugha ndani ya jamii. Hivi karibuni alitoa ripoti kuhusu kuchipuka kwa makanisa mengi ambayo yamekuwa maarufu barani Afrika.

“Tumegundua kuwa baadhi ya makanisa yamekuwa yakijipatia faida kutokana na bidhaa za imani zinazonunuliwa na watu maskini wenye shauku ya kubadilisha maisha yao kuwa mazuri,” anaeleza

Ripoti hiyo imeeleza zaidi kuwa kuna vitendo vinavyofanywa visivyo salama kwa waumini kama vile kula Panya, Nyoka, Majani na kunywa mafuta ya petroli ili kuwapima imani yao. Pia kumekuwa na shutuma za udhalilishaji wa kijinsia kwa baadhi ya makanisa, Hata hivyo Mkuu huyo anasema suala la dini ni uamuzi wa mtu mwenyewe.

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Audio: Sampamba - Roho Mtakatifu

Next post

Video | Audio: Goodluck Gozbert - Hauwezi Kushindana