Connect with us

Somo: Namna ya Kushughulikia Roho ya kukataliwa.

Mafundisho

Somo: Namna ya Kushughulikia Roho ya kukataliwa.

Na Mtumishi wa Mungu;
Mwl & Nabii Mwmbeso Mandela Michael

Tuombe kabla ya somo;

Bwana Yesu ahsante, naomba uwafundishe watu wako kama upendavyo wewe kupitia Roho Mtakatifu ambaye ni Mwalimu wa pekee. Mioyo yao, mawazo yao, na ratiba zao naziweka mikononi mwako. Ufalme wako uende mahali walipo na mapenzi yako yatimizwe maishani mwao. Amen.

UTANGULIZI:
#  Somo hili ni la muhimu sana kwako wewe utakayelifuatilia mpaka mwisho na kulielewa nikiamini Maisha yako hayatabaki kama yalivyokuwa kwa msaada wa Mungu.

#  Siku Mungu aliponifundisha somo hili maisha yangu ya utumishi yalibadilika sana ndani ya muda mfupi. Nilipata kiu ya kutaka kumtumikia Mungu zaidi katika maisha yangu na mara hali ya kuona utumishi ni mzigo iliondoka ndani yangu. Hali ya kuomba sana nafasi za kuhudumu na kukataliwa gafla iliondoka bali mialiko ya kuhudumu ndiyo iliyokuja zaidi bila ya mimi kuiomba. Kibali kiliingia kwa watu wa Mungu juu ya huduma yangu, kibali kiliingia kwa watumishi wakubwa walionitangulia kwenye huduma katika nchi hii na Mungu akanipa nafasi ya kuwa karibu nao. Ndio maana leo Mungu amenipa nafasi ya kuwafundisha watu wake.

Lengo la somo hili ni kukufundisha namna ya kushughulikia roho ya kukataliwa kwenye maisha yako. Katika maeneo haya;
i. Katika familia yako.
– Kutoka kwa wazazi wako au wadogo zako ikiwa wewe ni mkubwa wa familia
ii. Katika huduma yako/ wito wako
iii. Katika hali ya kuoa au kuolewa n.k
iv. Katika ofisi yako/kazi yako
v. Katika eneo unaloishi
vi. Katika hali ya Uyatima na ujane

Kunapokuwepo na roho ya kukataliwa utagundua mambo haya;

a. Kuna watu ambao ni waimbaji na wana nyimbo nzuri sana na zina ujumbe lakini hawakubaliki katika jamii zao au wanakubalika kidogo sana.
b. Kuna watu ambao ni wahubiri wazuri sana na wana mafundisho mazuri sana ila hawakubaliki kwa kiasi kikubwa
c. Kuna watu ambao ni viongozi wazuri sana katika nchi hii na wana mawazo mazuri sana ya kujenga lakini hawakubaliki sana au hawasikilizwi.
d. Ikiwa mtu ndio anaanza kutumikia wito alioitiwa basi inakuwa ni vigumu sana kupewa nafasi za kuhudumu wakati ndani yake kuna vitu amepewa kuachilia kwa watu.
e. Wajane wanavyoanza kunyanyaswa na ndugu wa upande wa mwanume baada ya ndugu zao kufa.
f. Yatima wanapokosa msaada hasa msaada wa kusomeshwa na ndugu zao baada ya wazazi wao kufa.

Yajue kwanza mambo haya juu ya roho ya kukataliwa;

 1. Roho ya kukataliwa haishughulikiwi kwa kuikimbia.
  Ukiikimbia itakufuata tu kwenye maisha yako/huduma yako. Paulo/Sauli aliwakimbia Wayahudi na akaenda kujiunga na wanafunzi wa Yesu, nao wakamkimbia.(Matendo 9:20 – 26); 23 Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; 26 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.

 2. Mara nyingi roho ya kukataliwa juu ya mtu huanzia tumboni (kabla mtu hajazaliwa).
  Mfano: Mtoto wa Ibrahimu Ishmaeli aliyezaa na mjakazi wake Hajiri. Alianza kukataliwa nyumbani kwa baba yake akiwa tumboni (Mwanzo 16:1- 9) “….Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. 7 Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. 8 Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. 9 Malaika wa Bwana akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake.”

 3. Roho ya kukataliwa ni matokeo ya kukosa kibali kwa watakatifu wa Mungu.
  Ingawa mtu anakuwa amepata kibali kwa Mungu aliyemwita/aliyeruhusu huyu mtu huyo aje duniani.

 4. Roho ya kukataliwa huwa inaambatana nyuma yake na roho ya kujiua/roho ya mauti.
  Mfano; Ndugu zake Yusufu baada ya kuanza kumkataa ndugu yao na kumuuza walitaka kumuua mwanzoni (Mwanzo 37: 26 – 27). 26 Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? 27 Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu.

Ukifuatilia zaidi roho ya kukataliwa inapoingia kwenye maisha ya watu utagundua mambo haya;

i. Watu wanajiua baada ya kukataliwa na wazazi wao au ndugu zao
ii. Watu wanajiua baada ya kuachwa kwenye mahusiano
iii. Watu wanatoa mimba baada ya wale waliowapa mimba kukataa hizo mimba (mwanamke kutoa mimba ni matokeo ya kukataliwa mtoto aliyeko tumboni)
5. Roho ya kukataliwa juu ya mtu haina maana kwamba alitenda dhambi mbele za Mungu.
(Ishmaeli hakutenda dhambi maana alikuwa tumboni)

TUANGALIE MIFANO INAYOONESHA ROHO YA KUKATALIWA ILIVYOWASUMBUA WATU KWENYE MAISHA YAO KIBIBLIA.

Mifano hii itakusaidia sana wewe unayefuatilia somo hili kwasababu mazingira ambayo watu hao walikutana na roho za kukataliwa yanafanana kabisa na mazingira tunayoishi sasa. Kwa mfano kuzaliwa nje ya ndoa (Ishmaeli), kukataliwa na ndugu zako( Yusufu, Daudi), Kukataliwa katika huduma/wito ulioitiwa (Paulo) n.k

1. Roho ya kukataliwa kwa YESU
#  Roho ya kukataliwa ilimsumbua sana Yesu katika huduma yake. Roho ya kukataliwa kwa Yesu ilianza kumfuatilia tangu akiwa tumboni, ndio maana Yusufu mchumba wake Mariamu alipogundua kuwa mchumba wake ana ujauzito akawa amemua kukimbia na Mungu akawa amembana kwenye ndoto ili asikimbie. (Mathayo 1: 18 – 24)
19 Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.20 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu
#  Hata baada ya kuzaliwa na kuanza huduma yake bado roho ya kukataliwa iliendelea kumfuatilia kwenye maisha yake ndio maana maandiko yanatuambia hapa kwenye Yohana 1:11“Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea”. Neno hawakumpokea linamaanisha walimkataa.
#  Kwa namna hiyo ya kumkataa ndio inayoonekana hadi sasa ulimwenguni kwasasabu sio wote wanaomwamini Yesu na kumpokea na hii ndio maana kuna dini nyingi ulimwenguni ambazo wanadamu wanaziamini. Mfano, Uislamu #  Nabii Isaya alitangulia kutabiri hapa kwa habari za Yesu kukataliwa, Isaya 53:3
Isaya 53:3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu
#  Pamoja na ishara zote na miujiza aliyoifanya mbele ya Wayahudi katika huduma yake ikiwemo kumfufua Lazaro (Yohana 11) lakini baadhi yao hawakumwamini kuwa yeye ni mwana wa Mungu hadi ulipofika wakati wa kifo chake.
Mathayo 27:54 “Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu”.

2. Roho ya kukataliwa kwa YUSUFU
#  Roho ya kukataliwa ilimsumbua Yusufu kutoka kwa ndugu zake na waliamua kumuuza. Kitendo cha kuuzwa maana yake ni hali ya kukataliwa. Inayomaanisha kwamba hatukuhitaji.
#  Ndugu zake Yusufu walimchukia sana kwa sababu zifuatazo; a. Alipendwa sana na baba yake kwasabu alikuwa mkweli.
(Kila ndugu zake walifanya mambo mabaya alimwambia baba yao, Mwanzo 37:2, 4)
b. Aliwashirikisha ndoto za maisha yake.
(Mwanzo 37: 2 -11). Kadri unavyowashirikisha idadi kubwa ya watu juu ya ndoto za maisha yako ndivyo unavyojiongezea idadi ya maadui.
Roho tano (5) mbaya ambazo zilimfuatilia Yusufu kwenye maisha yake;
i. Roho ya chuki
Kutoka kwa ndugu zake (Mwanzo 37: 2 – 11)
ii. Roho ya Mauti
Kutoka kwa ndugu zake, ndio maana walitaka kumuua (Mwanzo 37: 18 – 21)
iii. Kukataliwa
Kutoka kwa ndugu zake, ndio maana walimuuza (Mwanzo 37: 26 – 28)
iv. Roho ya Kusingiziwa
Alisingiziwa na mke wa Potifa kuwa yeye ndiye aliyetaka kumbaka na hatimaye akatiwa gerezani. (Mwanzo 39: 13 – 20)
v. Roho ya Zinaa
Kutoka kwa mke wake Potifa alikuwa boss wake Yusufu, aliyetaka kulala nae.
(Mwanzo 39: 7 – 12).
Ukiona roho ya zinaa inamfuatilia sana mtu ujue mbele yake kuna mambo mazuri ambayo Mungu amemwandalia na shetani ameyaona hivyo anaamua kupambana nae.
(Mfano ni Rahabu aliyekuwa kahaba; Yoshua 2, 3, 4, 5, 6 ambaye ndiye aliyekuja kuikoa familia yake). Shetani alijua kabisa kuwa Rahabu amebeba majibu ya familia yake ndiyo maana alipambana nae sana na akajikuta anafanya ukahaba.
Dhambi ya zinaa mara nyingi huwa inamfanya Mungu aondoe Baraka zake juu ya mtu akiifanya.
#  Jiulize kuna wanawake wangapi katika nchi hii, Afrika, duniani ambao ni makahaba na pia jiulize wamebeba nini kwa ajili ya familia zao?
* Ukija kufanya utafiti utagundua kuwa wengi ni watu ambao;
a. Familia zilikuwa zinawategemea sana na shetani alijua hilo
b. Wengi wamezaliwa wakiwa ndio wenye jinsia ya kike peke yao kwenye familia zao, unakuta wengine ni wanaume wote hivyo yeye ndiye alikuwa mwanamke pekee.

3. Roho ya kukataliwa kwa Mtume PAULO/SAULI
Mtume Paulo alisumbuliwa na roho ya kukataliwa kutokana na historia mbaya ya kuwaua watumishi wa Mungu aliyokuwa nayo kabla ya kumpokea Bwana Yesu kwenye maisha yake. Roho ya kukataliwa aliipata kutoka maeneo mawili;
a. Wayahudi wasiomwamini Yesu
Baada ya kumpokea Yesu Kristo na kuanza kushuhudia habari zake kwa Wayahudi wale ambao hapo awali waliijua historia yake vizuri wakataka kumuua.
Matendo 9:22- 23; 22 Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. 23 Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue;
b. Wanafunzi wa Yesu
Kutokana na historia aliyokuwa nayo ya kuua watumishi wa Mungu hata baada ya kuokoka wanafunzi wa Yesu hawakumwamini maana walishuhudia Stefano akiuawa mbele yake na hivyo wakawa wanamkimbia.
Matendo 26; 26 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.
TAFAKARI: Inapotokea mtu ameokoka halafu watu waliomtangulia wakawa wanamkatisha tamaa au wanamkimbia, basi ni rahisi sana huyo mtu akarudi kwenye maisha ya zamani na kuuacha wokovu. Neema ya Mungu ilikuwa tu juu ya Paulo maana baada ya kuona mitume wa Yesu wanamkimbia ilikuwa ni rahisi kwake kumuacha Yesu.

4. Roho ya kukataliwa kwa YOSHUA
#  Yoshua alipata wakati mgumu kwa wito wake baada ya kupewa nafasi ya kuwaongoza wana Israeli kwenda nchi ya ahadi ambayo ilikuwa ni nafasi ya Musa baada ya Musa kufa(Yoshua 1:1-2)
Yoshua 1: 1 – 2; 1 Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, 2 Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.
#  Wana Israeli walimpa Yoshua masharti magumu kwamba sisi tutakusikiliza ila Mungu aliyekuwa pamoja na Musa awe pamoja nawe , Yoshua 1: 17
Yoshua 1: 17; 17 Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; Bwana, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa.
#  Yoshua alipita katika wakati mgumu kutoka kwa wana Israeli ambao walikuwa wamemzoea sana Musa na ndiye waliyekuwa wamemuweka katika mioyo yao.
#  Hiki ndicho kilichomfanya Mungu amwambie Yoshua maneno haya (Yoshua 3: 7)
Yoshua 3: 7; 7 Bwana akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
v Mtu wa Mungu unayefuatilia somo hili;
Hakuna kitu kibaya kama ukapewa nafasi ya kuingoza familia yako ukiwa ndio mkubwa wa familia yako halafu ndugu zako/wadogo zako wasikukubali.
Hakuna kitu kibaya kama kupewa nafasi ya kuongoza mahali fulani halafu watu wasikukubali na wakawa wamemuweka moyoni mwao mtu aliyatangulia/aliyemaliza muda wake.
Hakuna kitu kibaya kama kupewa kuongoza ofisi ambayo kuna mtu aliyekuwa anakubalika Zaidi kwenye hiyo ofisi halafu ukakosa msaada wa Mungu.

5. Roho ya kukataliwa kwa DAUDI
#  Mtumishi wa Mungu Daudi nae alifuatiliwa na roho ya kukataliwa kutoka kwenye familia yake. Roho ya kukataliwa kwa Daudi inaonekana pale Nabii Samweli alipotumwa katika nyumba ya baba Daudi mzee Yese kwenda kumpaka mafuta ili awe mfalme juu ya taifa la Israeli.
#  Mzee Yese aliwaita watoto wake alikuwa anawaamini kuwa wanaweza wakawa wafalme juu ya Taifa la Israeli isipokuwa Daudi aliyekuwa amemtuma kuchunga kondoo. (1Samweli 16: 1 – 13)
11 Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. 12 Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.

NAMNA YA KUSHUGHULIKIA ROHO YA KUKATALIWA
#  Roho ya kukataliwa huwa inashughulikiwa kwa njia ya MAOMBI.
#  Roho ya kukataliwa inaposhugulikiwa katika maisha ya mtu huwa kinatokea kitu kinachoitwa KIBALI.

 • Mtume Paulo alikuja kugundua kuwa pamoja na neema aliyopewa ya kuwahubiri mataifa habari za Yesu Kristo ila alihitaji sana msaada wa maombi ili kile ambacho Mungu alikuwa ameweka ndani ya moyo wake kipate KIBALI kwa Mataifa.

Warumi 15: 30 – 31; 30 Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; 31 kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;

 •  Mungu anaporuhusu uzaliwe na akaweka vitu ndani yako maana yake umepata kibali ndani ya macho yake ila ile hali ya kupata kibali mbele za macho yake haina maana utakuwa umeshapata kibali kwa watu wake.

Roho ya kukataliwa katika kuoa au kuolewa

 •  Kuna familia nyingi ambazo zinazosumbuliwa na roho ya kukataliwa. Wasichana wanakuwa hawaolewi au wakiolewa basi wanaachika baada ya muda fulani na ikiwa ni mwanaume anakuwa ni mtu wa kukataliwa na kila mwanamke kabla ya kuoa au akishaoa wanawake wanamkimbia.
 •  Kumbuka kuwa mara nyingi hili jambo limekuwa likihusisha mambo ya maagano katika familia nyingi ambayo yalifanywa na watu waliowatangulia katika familia/ukoo.  Hivyo unaposhughulikia roho ya kukataliwa juu ya kuoa au kuolewa unatakiwa ufanye yafuatayo;
 1. Maombi ya toba ili kuondoa uhalali wa kisheria

 2. Maombi ya kufuta maneno yaliyonenwa na waliowatangulia katika familia wa vizazi vilivyopita, yaliyonenwa na adui zenu, yaliyonenwa na wewe mwenyewe Yakobo 3: 10, “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana”.

 3. Kuvunja maagano yaliyofanyika ikiwemo utoaji wa sadaka katika ibada za miungu mingine au ibada za kifamilia

 • Tumia damu ya Yesu kufuta hayo maagano. Waebrania 12:24 “Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili”.
 1. Kiruhusu kinywa chako/ ulimi wako kuumba maneno mapya Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi”

 2. Omba Mungu aachilie kibali juu yako na familia yako katika swala la kuoa au kuolewa
  TUANGALIE VIBALI AMBAVYO VILIKUWA JUU YA WATU WA MUNGU.
  Kwa kuangalia mifano hii itakusaidia wewe kuomba mbele za Mungu ili uvipate katika maeneo mbali mbali yanayohusu maisha yako.
  a. Kibali juu ya mtoto Samweli
  1Samweli 2:26 Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa Bwana, na kwa watu pia

 • Kupitia mfano huu tunaona namna ambavyo mtoto Samweli alivyopata kibali maeneo yote mawili, kwa Bwana na kwa wanadamu.

b. Kibali cha Esta

 •  Ukisoma vizuri habari za Esta utafahamu kuwa Esta alipata kibali kwa Mungu na pia kibali kwa mfalme/watu wote.

Esta 2:15 Naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona.

 •  Maombi ndio yaliyomsaidia Esta kupata tena kibali kutoka kwa mfalme ambacho alikipoteza na badae roho ya kukataliwa na mfalme ilikuwa juu yake.

Esta 4:16 Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.

 • Baada ya maombi tunaona Esta akipata tena kibali mbele ya Mfalme ambacho kilikuwa kimetoea

Esta 5:1-14; 1 Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba. 2 Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.

c. Kibali cha wana Israeli
Kutoka 11:3 Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake.
ü Hapa tunaona kibali cha aina mbili kwa wana Israeli, Kibali kwa Mungu na kibali kwa adui zao.

d. Kibali cha Danieli
Danieli 1:9 Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.
e. Kibali cha Yusufu

 •  Pamoja na roho ya kukataliwa kuwa juu ya Yusufu kutoka kwa ndugu ila kila alipoenda alipata kibali kwa wakuu na kila alilolifanya lilifanikiwa.
 1. Aliponunuliwa na Potifa alipata kibali kikubwa sana
  Mwanzo 39:5 – 6; 5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. 6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu.

 2. Alipoenda gerezani alipata kibali kwa wakuu wa gereza
  Mwanzo 39:21 – 23; 21 Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. 22 Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. 23 Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya.

 3. Alipoenda kwa Farao akapata kibali na akawa Waziri mkuu (Mwanzo 41:1-57)

 •  Utakapokuwa unaghulikia roho ya kukataliwa utakuwa unaomba ili upate kibali kwa watu wa Mungu kama vile ulivyopata kibali kwa Mungu.
 • Unapota nafasi yoyote katika eneo, mfano kwenye wito, ofisi n.k unatakiwa kuomba kibali kwa Mungu ili aachilie kwa watu wake wa eneo hilo. Kibali ndicho kitakachokufanya ukubalike katika eneo lolote ulioitiwa.

Unaweza ukaomba kibali;
1. Katikati ya wahubiri wenzako na watakatifu wa Mungu ili wapate kukupa nafasi ndani ya mioyo yao ili wakipokee kile ambacho Mungu ameweka ndani yako.

 1. Katikati ya waimbaji wenzako na pia kipate kukubalika na watakatifu wa Mungu ili wapate kukipokea

 2. Katikati ya wafanya kazi wenzako na pia kwa wakubwa zako kazini. Na hapa Mungu anakupa heshima ya kusikilizwa.

 3. Ukiwa mzazi au unatarajia kuwa mzazi basi waombee wototo maombi ya kibali. Hii itawafanya wapate kibali kuanzia wakiwa watoto na hata watakapokuwa wanasoma watapata kibali katikati ya wanafunzi wenzao na walimu wao.

 4. Unapokuwa umefiwa na wazazi kumbuka kuomba maombi haya maana Mungu anaweza akawainua watu wa kukusaidia ambao wakati mwingine wanaweza wasiwe ndugu zako

Kuna watu wengi sana wa Mungu ambao wapo katika kilio cha namna hii cha roho za kukataliwa,
I. Wako wahubiri ambao wapo katika kilio cha namna hii na wanaanza kuona kama Mungu hajawaita katika utumishi,
II. Wako waimbaji ambao wako kilio cha namna hii na wamekata tamaa ya kutumika tena
III. Wako watu waliokosa kibali katika familia zao ingawa wao ni wakubwa na wanadgarauliwa na wadogo zao
IV. Wako Yatima na wajane ambao wako katika kilio cha namna hii
V. Wako watu wengi sana ambao wako katika mazingira magumu sana katika maeneo yao ya kazi

MWISHO WA SOMO
Hili somo ni muhimu sana katika maisha ya mtu yeyote ambae anaishi hapa duniani na Mungu amekusudia liwasaidie watu wengi.Unaweza ukawa ni wewe mwenyewe, mzazi wako, kaka au dada yako, rafiki yako, mume wako au mke wako, mtoto wako. Mshirikishe hili somo mahali popote alipo ili limsaidie katika maisha yake.
Watumie watu mbali kwenye magroup ya WhatSapp na watu binafsi ulio na namba zao na wanatumia WhatSapp.
Utukufu na heshima ni kwa MUNGU WANGU ALIE HAI PEKE YAKE (Luka 17:10).

Somo hili limeandaliwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu na Mtumishi wa Mungu;
Mwl & Nabii; Mwambeso, Michael Mandela
Mawasiliano: 0752 197 065; 0784 136 816
Email; mwambeso89@gmail.com

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top