Habari

Rais Magufuli apuuza waraka wa maaskofu Tanzania

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ameupuuzilia mbali waraka wa maaskofu uliotolewa wakati wa kuanza kwa msimu wa Pasaka akisema hauna msingi wowote ule.

Aliendelea kwa kusema pia kwamba mbona hakuna aliyetoa waraka wakati mauwaji ya Kibiti yakiendelea.

Rais Magufuli amesema hayo katika hafla ya kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa rada za kiraia uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Majibu yake kwa waraka wa maaskofu aliyatoa wakati akiwapongeza wasaidizi wake, mawaziri, viongozi wa ulinzi na usalama pamoja na wasaidizi wengine, ambao amewasifu kwa kuendelea kutimiza majukumu yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli na waumini wengine wakifurahia jambo wakati wa mahubiri ya Paroko Msaidizi Venance Tegete katika Maadhimisho ya Misa ya Ibada ya sikukuu ya Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam jana Jumapili Aprili 1, 2018

“Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ndio maana tuko salama leo, ilifikia mahali hata kwenda Kibiti tu ni kazi. Hatukuona mtu yeyote analaani,” amesema Dkt Magufuli.

“Kufa kwa Kibiti ni salama, hakuna hata waraka uliotoka. Ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili kwa kwa sababu najua halina msingi, wala halitafanikiwa na wala hakuna lolote. Kwa sababu serikali ipo, nimekabidhiwa na wananchi, kuilinda kwa nguvu zote”.

Amesisitiza serikali ipo na amekabidhiwa na wananchi na kuapa kwamba atailinda kwa nguvu zote.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kujibu moja kwa moja waraka uliotolewa na maaskofu wa kanisa la Kilutheri nchini Tanzania wiki chache, ambao pamoja na mambo mengine ulionya juu ya mwenendo wa demokrasia nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimia waumini wenzie baada ya Maadhimisho ya Misa Ibada ya sikukuu ya Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam jana Jumapili Aprili 1, 2018

Maaskofu walisema nini?

Katika waraka wa ujumbe wa Pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo liliorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Serikali ya Tanzania mwanzoni ilijibu tu kwa kusema kuwa kwa wakati huo haikuona cha kujibu na kwamba iliwatakia tu waumini kheri ya Pasaka.

Chanzo: BBC Swahili

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Video | Audio: Shadrack Robert - Siyabonga Jesu

Next post

Muna Love - Mwanangu ndiye aliyenifanya niokoke