Connect with us

Muna Love – Mwanangu ndiye aliyenifanya niokoke

GospoTV

Muna Love – Mwanangu ndiye aliyenifanya niokoke

Na mwandishi wetu,

Muigizaji na muandaaji wa matamasha ya burudani Tanzania Muna Love amefunguka na kuweka wazi ushuhuda wake uliomfanya yeye kurudisha maisha yake kwa Yesu, hii ikiwa ni baada ya wiki chache zilizopita kuzua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutangaza rasmi uamuzi wake huo ambao ulionekana kama ni kitu ambacho hakijapendezwa na watu wengi ambao walikuwa wakimfuatilia kupitia mitandao ya kijamii na sehemu nyingine mbalimbali.

Muna Love ambaye jina lake kamili ni Rose Alphonce amekiambia chombo kimoja cha habari kuwa kwasasa ameamua kumtumikia Mungu kwakuwa ameona upendo wake mkuu maishani mwake hasa kwa kumuokoa mtoto wake ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo ambalo lilimfanya mara kwa mara kuingiwa na roho ya kukata tamaa.

“Unajua Patrick aliugua kwa muda mrefu miguu. Na ugonjwa wake ulianza kama utani. Tuliamka siku moja akawa hatembei. Anatambaa tu. Nilijua anatania, lakini hali iliendelea kuwa siriaz. Nikampeleka Hospitali ya Agha Khan, akafanyiwa vipimo nikaelezwa ana maumivu tu baadaye atakuwa sawa. Lakini bado hakupona.

Nikampeleka tena Hospitali ya Sanitarian akafanyiwa uchunguzi ndipo wakaniambia nimpeleke Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Muhimbili, baada ya kumchunguza walimfanyia oparesheni na kumuwekea vyuma kwenye mapaja huku wakiniambia anatakiwa kuongezewa madini ya ‘calcium’.

Lakini baada ya muda vile vyuma vikawa vinatunga usaha. Ikabidi wafanye oparesheni ya pili na baadaye ndipo wakafanya oparesheni ya tatu na kumuwekea madini hayo. Madaktari wakaniambia baada ya kuangalia maendeleo yake, atatakiwa tena kufanyiwa oparesheni ya nne na ya mwisho ambayo ndiyo ingemsaidia kurudi kwenye hali yake ya kutembea, lakini ingegharimu kati ya shilingi milioni 25 hadi 50.

Nilihisi kuchanganyikiwa. Zilikuwa ni pesa nyingi ambazo nilifahamu kuzipata kwa haraka ulikuwa ni mtihani mzito. Lakini jambo la kushangaza wakati mimi ninaumiza kichwa juu ya fedha hizo, mtoto yeye kila mara alikuwa ananiambia tu kwamba mama ukiokoka, basi mimi ninapona.

Aliendelea kuniambia hivyo kwa siku kadhaa na kuna wakati hata akina mama niliokuwa nao pale hospitalini (Muhimbili) walikuwa wakiniambia usiku nikipitiwa na usingizi Patrick alikuwa anazungumza peke yake na kudai kwamba anazungumza na malaika. Baada ya kuokoka kweli alipata nafuu, na jambo la kumshukuru Mungu, ile oparesheni ya nne haikuweza kufanyika. Badala yake madaktari waliniambia niende naye nyumbani. Lakini niishi naye kwa uangalifu kwa muda na hakuwa anaruhusiwa kukanyaga chini.

Baada ya kurudi nyumbani, nikiwa sipo, nikirejea nyumbani msaidizi wa kazi alikuwa ananiambia kwamba nikitoka Patrick naye anatoka kwenye machuma na kutembea. Ilinishangaza na nikawa mkali kidogo katika hilo, lakini siku moja aliniambia nikimpeleka kanisani atapona kabisa na alinisisitiza sana.

Nikaamua kufanya hivyo. Nikampeleka kwenye kanisa linaloitwa Dokas. Tulivyofika pale kanisani alipoiona tu picha ya Yesu, akaanza kutembea. Na huo ndiyo ukawa uponyaji wake. Kwa hiyo kuanzia hapo nikaamua kuokoka kwelikweli. Maana kwa haya hata mtu yeyote angeokoka tu!” – Alisema Muna Love

Muna Love amekuwa ni moja kati ya wanawake waliojipatia umaarufu mkubwa kupitia uigizaji wa filamu na mambo mbalimbali yanayohusu burudani nchini, ikiwemo uandaaji wa matamasha ya muziki ikiwa ni moja ya vitu ambavyo vimempa mafanikio makubwa, ukiachilia mbali biashara anazofanya.

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

More in GospoTV

To Top