MFAHAMU MLEMAVU MWENYE MAFANIKIO MAKUBWA DUNIANI - Gospo Media
Connect with us

MFAHAMU MLEMAVU MWENYE MAFANIKIO MAKUBWA DUNIANI

Maarifa

MFAHAMU MLEMAVU MWENYE MAFANIKIO MAKUBWA DUNIANI

Unakuwa na miguu, unakimbia kwa kasi huku ukirukaruka. Unakuwa na mikono, unashika kila kitu unachotaka kushika. Mungu amekupa viungo vyote, haimaanishi wewe ni muhimu kuliko walemavu wengine, jua kwamba ni nafasi ya kipekee na ya upendeleo uliyoipata, inawezekana haukustahili.

Kwa jina anaitwa Nicholas James “Nick” Vujicic, ni miongoni mwa watu waliofanikiwa japokuwa hana mikono, na miguu aliyokuwa nayo ni midogo mno. Leo, unapozungumzia kuhusu watu wenye mafanikio ambao ni walemavu, basi jina lake litakuwa miongoni mwa majina hayo.

1142561

Mbali na ulemavu aliokuwa nao lakini Vujicic ni mfundishaji mzuri kwa watu masomo na mbinu zinazoweza kumfanya mtu kufanikiwa (motivational speaker). Katika kila semina anayoifanya, watu wengi wanakusanyika na kumsikiliza huku, wanajifunza mbinu za kufanikiwa kutoka kwa mtu ambaye wala hawezi kukimbia.
Azaliwa akiwa na Phocomelia

Vujicic alizaliwa mwaka 1982 katika Jiji la Melbourne nchini Australia. Mara baada ya kuzaliwa, madaktari walipomuona, walishtuka kwani aligundulika kuwa na tatizo la kukosa viungo ambalo kwa kitaalamu huitwa Phocomelia.

Alipokuwa akikua, hakutaka kujiona kama alikuwa mlemavu bali alichokifanya ni kufanya mazoezi kwa nguvu, kuvipa nguvu viungo vyake hasa miguu yake ambayo ni midogo mno isiyokuwa na uwezo hata wa kuvalishwa viatu.

SAFARI YAKE YA MASOMO

Alianza kusoma katika Shule ya Runcorn State ambayo ipo nchini Australia inayochukua watoto kuanzia miaka 12-17. Alipofikisha miaka 17, akaanza kuzungumza na wanafunzi mbalimbali akiwafundisha kuhusu mafanikio, nini walitakiwa kufanya, nini hawakutakiwa kufanya ili wafanikiwe.

Alipofikisha miaka 21, akamaliza masomo yake katika Chuo cha Griffith na kuchukua Shahada ya Uchumi, pia akachukua Uhasibu na Mipango Fedha kwa pamoja.

Mafundisho yake yaliwavutia watu wengi na hivyo kukusanyika na kuanza kumsikiliza. Wengi walimtabiria mafanikio hapo baadaye, hakuacha kujifunza, ili kuwa mwalimu mzuri ilikuwa ni lazima mtu ajifunze, hivyo akafanya hivyo.

Baada ya kuwafundisha watu wengi kuhusu mafanikio, akaamua kuanzisha taasisi iitwayo Life Without Limbs (Maisha Bila Viungo). Mwaka 1990 akashinda tuzo iitwayo Australian Young Citizen na mwaka 2005 akachaguliwa kuwania Tuzo ya Young Australian of the Year.

AMUOMBA MUNGU APATE MIGUU MIKUBWA NA MIKONO

Kipindi cha nyuma alikuwa mtu wa kulia, alilalamika jinsi alivyokuwa. Alimuomba Mungu apate miguu mikubwa na mikono. Akasema kwamba alikuwa akinunua viatu kwa kuamini kwamba kuna siku Mungu atafanya miujiza ili awe na miguu yenye kumuwezesha kuvaa viatu.

Wakati akiendelea na maombi yake, akagundua kwamba mafundisho yake yaliwabadilisha watu, wengi wakafanikiwa, hivyo akamshukuru Mungu kwa kumpa uhai tu kwani ilitosha kuwabadilisha watu wengine.

MAMA AMPA SOMO

Wakati akiwa amekata tamaa, mama yake akamuonyeshea makala iliyoandikwa kwenye gazeti moja, mwandishi wa makala huyo alikuwa kama yeye, hana mikono, akaambiwa kwamba hata yeye pia anaweza kufanikiwa kama huyo mtu, hivyo akaanza kupambana, kusoma zaidi huku mara zote akimshukuru Mungu kwa kuwa hai, kwani mlemavu hakuwa peke yake kama alivyohisi huko nyuma.

MAFANIKIO YAKE

Mwaka 2005 akatoa DVD yake ya masomo iitwayo Life’s Greater Purpose (Dhamira Kubwa Zaidi Katika Maisha) ambayo ilikuwa katika mtindo wa makala. Mbali na hiyo DVD yake ya pili aliifanya kwenye kanisa alilokuwa akisali lililopo Brisbane huko Australia aliyoiita No Arms, No Legs, No Worries (Hakuna mikono, Hakuna Miguu, Hakuna Mashaka).

Mbali na DVD hizo pia alishiriki katika filamu mbalimbali kama The Butterfly Circus (2010) ambapo alishinda Tuzo ya The Feel Good Film Festival huko Holywood nchini Marekani.

Mwaka 2010 akaandika kitabu chake alichokiita Life Without Limit: Inspiration for a Ridiculously Good Life (Maisha Bila Kikomo: Matumaini Kwa Maisha Mema ya Mzaha.

Trent Nelson | The Salt Lake Tribune Motivational speaker Nick Vujicic speaks to students at Bryant Middle School and beyond about the dangers of bullying. The assembly was simulcast and streamed to some schools across Utah Thursday March 7, 2013 in Salt Lake City

MAISHA YAKE YA NDOA

Vujicic amemuoa mwanamke aitwaye Kanae Miyahara mwaka 2012 ambaye amezaa naye watoto wawili, Kiyoshi James (2013) na Dejan Levi (2015).

TUNAJIFUNZA NINI?
Kama watu tunaotafuta mafanikio, hatupaswi kuangalia udhaifu wa miili yetu. Japokuwa tuna udhaifu fulani katika viungo vyetu, bado Mungu ametupa akili ya kupambana na tukafanikiwa.

16222759
By Eric Shigongo.

More in Maarifa

To Top