Mafanikio: Sehemu ya Tatu - Jithamini ili uweze kufanikiwa - Gospo Media
Connect with us

Mafanikio: Sehemu ya Tatu – Jithamini ili uweze kufanikiwa

Uncategorized

Mafanikio: Sehemu ya Tatu – Jithamini ili uweze kufanikiwa

Kujithamini ni nguzo muhimu sana katika maisha aidha ni kati ya mambo ya awali kabisa katika safari ya mafanikio.

Kujithamini ni kujiamini, ni kujiona unaweza ni kuamini katika uwezo ulionao ni kuamini kwamba wewe ni mtu wa thamani ni kuamini kwamba una mchango wa pekee sana katika jamii.

Ni vigumu sana kufanikisha maono uliyonayo mipango na mikakati uliyojiwekea  kama haujithamini, kama hujioni kwamba wewe ni mtu wa thamani ama kama hauamini katika uwezo ulionao.

 • Kila mtu aliyekuja duniani alikuja kwa sababu maalumu na kusudi maalumu.
 • Kila aliyezaliwa amepewa ndani yake uwezo wa asili wa kumfanya afanikiwe.
 • Kila aliyezaliwa amepewa kitu ama jambo kwa ajili ya wengine (jamii ).
 • Kila aliyezaliwa ni mtawala endapo tu ataishi sawa sawa na sababu ya kuumbwa kwake.
 • Kila aliyezaliwa amepewa uwezo wa kuchagua kupanga na kuamua.

Mwanadamu ni kiumbe cha tofauti na viumbe vingine vyote, ni kiumbe pekee chenye utashi wa kuweza kutambua wema na ubaya, ni kiumbe pekee kilichoumbwa kwa mfano wa Mungu chenye kuishi  kwa namna mbili kwa wakati huohuo  namna ya roho na namna ya mwili

JE UMEWAHI KUFIKIRI KWA NAMNA HII AMA KUJIULIZA MASWALI YA NAMNA HII

 • Yamkini mungu alikosea kuniumba!
 • Kwa nini nilizaliwa maskini ?
 • Kwa nini nimekulia mazingira haya ?
 • Kwa nini mimi ni mfupi, mrefu, mwembamba, mnene, mweupe, mweusi?
 • Kwanini sikuwa kama Fulani, sikuwa na pesa kama zake , umbile kama lake?

Je umewahi kufikiri kuwa yamkini wewe unakasoro fulani kwa sababu ya maumbile yako au mazingira yako, Je unaona wengine kuwa ni bora sana kuliko wewe umewaona wao ndio wenye uwezo wa kufanya mambo makubwa na sio wewe.

Maandiko yanatuonyesha wazi kabisa kuwa  vile tulivyo si kikwazo cha kufanikiwa kwetu mifano hii miwili itusaidie kujua uhalisia wa jambo hili.

 • kutoka 4;10 musa akamwambia Bwana Ee Bwana mimi si msemaji tokea zamani wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako maana mimi si mwepesi wa kusema na ulimi wangu ni mzito.
 • Waamuzi 6;15 akamwambia Ee Bwana nitawaokoa kwa jinsi gani ? tazama jamaa zangu ndio walio maskini sana katika manase na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.

Musa alipoitwa na Mungu ili awaokoe wana wa Israel alijitazama udhaifu wake jinsi alivyokuwa mzito katika kuongea kwa lugha ya sasa tunaweza kusema alikuwa na kigugumizi  aliona kana kwamba udhaifu wake unaweza kuzuia mafanikio yake juu ya habari ya wito Mungu aliomuitia.

Kutoka 4; 11-12

Bwana akamwambia ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi au mwenye kuona au kuwa kipofu si mimi Bwana basi sasa enenda nami nitakuwa pamoja na kinywa chako na kukufundisha  utakalonena.

Bwana anatuonyesha wazi kuwa Yeye ndiye muhusika  wa vile alivyomfanya mwanadamu Kwa ajili ya utukufu wake  awe ni bubu au kiziwi mwenye kuona ama kipofu Mungu ndiye aliyewafanya wote kwa makusudi yake,  udhaifu wako usiwe sababu ya kukufanya ujidharau. Kama Bwana alivyomwambia Musa enenda nami nitakuwa pamoja na kinywa chako kukufundisha;  kwa lugha nyingine ni kwamba kuna namna Mungu alitaka kuutumia udhaifu uleule ambao Musa aliuona kuwa ni kikwazo kwa ajili ya utukufu wake ili kutimiliza kusudi lake.

Gidion alipoitwa ili awaokoe wana Israel  aliangalia udhaifu wa mazingira yanayomzunguka gidioni akasema “tazama jamaa zangu ndio walio maskini sana katika manase na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu”

Alitazama umasikini wa  familia yake na alitazama udogo wake , Mambo haya yalimfanya ajiweke kwenye kundi la watu dhaifu watu wasioweza kitu.

Udhaifu wako na mazingira yako yasiwe kikwazo ukaona kama huwezi kufanikiwa ukaona wewe ni wakushindwa ukajitoa kwenye kundi la watu wanaoweza kuleta mabadiliko Inawezekana umezaliwa na ulemavu wa aina Fulani Inawezekana unaishi katika mazingira magumu sana. Hayo yote  hayaondoi uthamani wako  jithamini amini katika uwezo wako Jikubali jinsi ulivyo.

Je unajiweka kwenye kundi la watu wa aina gani:

Watu wazuri ama watu wabaya wenye nguvu ama dhaifu, wanaoaminika ama wasioaminika, wenye busara ama wapumbavu.

Kujithamini si kuvaa vizuri si kujiremba ama kujipamba sana kwa vitu vya thamani,  ama kuiga maisha ya mtu fulani  kujithamini ni kujikubali vile ulivyo na kuamini katika uwezo wako Kujithamini huleta uhuru, kujiamini pia  hutengeneza msimamo wa kimaisha.

Mungu wetu ni Mungu anayeufanya mwisho tangu mwanzo

Mungu ndiye aliyeufanya mwanzo wako  haijalishi ni mwanzo wa aina gani Mungu ndiye aliyeufanya  pia anajua na mwisho wako.

 • Mungu hakukosea kukuumba hivyo ulivyo hakukosea kukupa rangi uliyonayo, wala hakukosea kukupa kimo ulichonacho Mungu alifanya kwa makusudi yake.
 • Mungu hakukosea kukupa umbile ulilonalo uwe mwembamba au mnene umbo namba nane ama english figure Mungu alikufanya kwa makusudi yake.
 • Mungu hakukosea kukufanya uzaliwe kwenye familia uliyozaliwa, na wazazi hao waliokuzaa ,ukulie kwenye mazingila hayo uliyokulia , yawe ni mazingira magumu Mungu alifanya kwa kusudi lake.
 • Yamkini hukubahatika kuwafahamu hata wazazi wako,ama yamkini hata ndugu zako , Mungu alifanya kwa makusudi yake.

Kumbuka jambo hili la muhimu sana ya kwamba vile ulivyo kwa namna yoyote ile Mungu alikufanya kwa makusudi yake maalumu.

Kosa la kwanza na kubwa kuliko yote katika mafanikio ni Kujidharau, kujiona kana kwamba kuna jambo limepungua kwako ama kujiweka kwenye kundi la watu walioshindwa watu waliokata tamaa, kuona kana kwamba kuna vitu huvistahili ama vipo kwa ajili ya wengine.

Kufanikiwa huanza pale mtu anapojithamini anapojikubali jinsi alivyo anapojikubali na mazingira aliyonayo

 • Mungu angezidisha hata chembe ya rangi yako usingefaa kwa kusudi alilokuumbia
 • Mungu angezidisha hata chembe ya kimo chako usingefaa kwa kusudi alilokuumbia
 • Mungu angezidisha hata chembe ya umbile lako usingefaa kwa kusudi alilokuumbia
 • Mungu angezidisha hata chembe ya vile ulivyo vile alivyokuumba usingefaa kwa makusudi yake

Usijaribu kupima uwezo wako kwa kujifananisha na mtu fulani ama usijaribu kutaka kufanana na mtu Fulani. Utasikia kauli nyingi za vijana kama  “Nataka kuwa kama  yeye”. “Nataka  nifanye kama anavyofanya”

Kila mtu ameumbwa na Mungu kwa namna tofauti, hakuna mtu anayefanana na mwingine kila mtu ana upekee wake hata kama wanafanya vitu vinavyofanana. Amini na thamini uwezo ulionao. Amini kwamba ulichonacho ndicho kinachohitajika haswa ili kutoa majibu ya matatizo yanayozunguka jamii.

Vijana wengi wametumia muda wao mwingi kufuatilia maisha ya watu wengine na pengine wametamani kuwa kama  wao, kuliko wanavyotumia muda wao kujua wao ni wakina nani.Vijana wengi wamejikuta wanaishi maisha ya watu fulani Fulani.Anaongea kama mtu Fulani,anavaa kama mtu Fulani na anataka kuishi kama mtu fulani. Kuishi maisha ya watu wengine kunafisha uwezo halisi ulionao.

Usikatishwe tamaa katika kufanyia kazi mawazo  ulioyonayo ili kudhihirisha uwezo wako halisi. Anza sasa kuishi wewe halisi. Wewe halisi ndio pekee unayehitajika kutoa majibu ya changamoto zinazoizunguka jamii

INAENDELEA………………

Kwa mawasiliano zaidi na ushauri wasiliana na Emmanuel Mwakyembe kupitia:
Simu/WhatsApp: +255 716 531 353/+255 766 939 969
Facebook Profile: Emmanuel Mwakyembe
Istagram: @oficial-mryopace
Email: emamwakyembe@gmail.com

Like Page yetu ya facebook > GOSPOMEDIA.COM instagram: @gospomedia

More in Uncategorized

To Top