Connect with us

Mafanikio Sehemu Ya Nne: Ijue Nguvu ya Bidii katika Mafanikio Yako.

Uncategorized

Mafanikio Sehemu Ya Nne: Ijue Nguvu ya Bidii katika Mafanikio Yako.

Bidii ni ile hali ya kufanya jambo fulani kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote .

Bidii ni kufanya jambo kwa hamasa kubwa, kwa uaminifu na msimamo thabit,

Bidii ni kutumia kwa utimilifu maarifa, ujuzi na kipaji ulichopewa katika kufanikisha jambo fulani.

Kuna tofauti kati ya kufanya jambo na kufanya jambo kwa bidii kwa mfano wanafunzi wanaosoma shule za bweni, huwa wamewekewa ratiba moja ya  vipindi vya darasani  ratiba moja ya muda wa kula, muda wa kujisomea n.k wote wanafundishwa na walimu hao hao, wana library hiyo hiyo lakini huwa na tofauti kubwa sana kati ya mtu mwenye bidii na yule ambaye hana bidii kitakachomtofautisha mtu mwenye bidii na yule ambaye hana bidii;

Mwenye bidii anakuwa na hamasa ya kujua zaidi atataka ajue zaidi vile alivyokwisha kufundishwa na mwalimu wake na atataka ajue pia vile ambavyo bado hajafundishwa namna hii itamsababishia mwanafunzi  huyu atumie muda wake mwingi kujisomea library ili ajue zaidi, atatafuta muda wa ziada wa kujisomea tofauti na ule wa kawaida ambao wote huutumia kujisomea atatengeneza uhusiano mzuri na walimu wake na kupata muda wa kuwauliza maswali na hata kuomba walimu wamfundishe zaidi pale ambapo hajaelewa.

Bidii ni siri ya mafanikio tena ni siri ya utajiri, Bidii huharakisha kutimia kwa malengo na maono. Uvivu ni sumu ya mafanikio tena ni chanzo cha umasikini uvivu hufanya akili isifikiri na kuleta majibu. Wengi wetu tunatamani tufanikiwe na huku ndani yetu tumejaa uvivu tunafanya mambo kwa mazoea na wala hatuna bidii.

Kuwa na malengo peke yake haitoshi aidha kujua uwezo ulionao ama kipaji ambacho Mungu amekupa peke yako haitoshi. Ni lazima uwe na hamasa ndani yako ya kutaka kuona malengo yako yanatimia, hamasa ya kuona mabadiliko kwenye hali uliyonayo. Msukumo wa ndani ni wa muhimu sana kukupa bidii ya kufanya zaidi, kuwaza zaidi, kutafuta zaidi ili uyafikie maono yako.

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa watu wenye kipato cha chini  zaidi au watu wenye maisha ya chini zaidi ndio watu wanaopoteza muda mwingi zaidi katika mambo yasiyo na tija kwenye maisha lakini pia watu duni ndio wanaoongoza kwa kulala masaa mengi zaidi. Hii ni tofauti na watu waliofanikiwa sana kwani ni watu ambao muda hauwatoshi, wanafanya kazi kwa masaa mengi na wanalala muda mchache. Utafiti wa kisayansi unasema kwa mtu mzima; masaa sita yanamtosha kupumzika kwa siku pasipokuathiri afya yake.  Watu wengi tunapenda kufanikiwa,tunapenda kuleta tija katika jamii zetu  lakini  tumejawa uoga wa kuingia gharama ya kuyafikia mafanikio. Hatutaki  kujitaabisha, Gharama mojawapo ndiyo hii kufanya kazi kwa bidii.

Kwa jambo lolote lile unalolifanya lifanye kwa bidii kubwa, lifanye kwa kutumia uwezo wote uliopewa na Mungu wako iwe ni kazi,iwe ni biashara,iwe ni kipaji hakikisha kila siku unajikumbusha maono yako, kule unakotaka ufike ili kukupa nguvu  mpya na kuchochea msukumo wa ndani na kuchochea  bidii uliyonayo na imani yako kuhusu jambo hilo.

Bidii na Imani na vitu ambavyo vinafungua milango ya fursa nyingi zaidi kukujilia, lakini pia bidii inakusaidia kutotumia muda wako mwingi kwa mambo yasiyo na maana. Bidii ni silaha ya mafanikio ukitaka kufanikiwa tumia silaha hii vizuri huku ukimwamini Mungu.

MUUJIZA WA BIDII KUKUFANYA UFANIKIWE KATIKA MAISHA

 • Bidii husababisha kutimia kwa malengo na maono ya mtu

Mithali 13:4 “nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa”

Hii inamaanisha unaweza ukawa na nia ya dhati ya kufanikisha jambo Fulani lakini uvivu wako ukawa ni kikwazo,  hivyo unaishia kuwa ni mtu wa kutamani tu lakini hupati kitu chochote, maandiko yanatueleza wazi kabisa kwamba nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa  maana yake bidii ina nguvu ya kufanikisha jambo sawa sawa na vile lilivyo tarajiwa

 • Bidii ina nguvu ya kumfanya mtu mtawala

Mithali 12:24 “Mkono wa mwenye bidii utatawala  bali mvivu atalipishwa kodi”

Moja ya sifa ya mtu aliyefanikiwa huwa ni mtawala  ama kiongozi  hii ni kwa sababu bidii inamsababisha mtu huyu kuwa na maarifa zaidi kuliko wengine ama kuwa na ujuzi zaidi kuliko wengine,  bidii inamuweka mtu huyu kwenye nafasi ya kutatua changamoto za wengine,  wakati mtu mvivu kwa uvivu wake anajiweka kwenye nafasi ya kuwa mtumwa wa wengine.

 • Bidii inampa mtu heshima.

Mithali 22;29 “ je wamwona mtu mwenye bidii  katika kazi yake  huyo asimama mbele ya mfalme hatasimama  mbele ya watu wasio na cheo.

Mtu mwenye bidii huwa habaki hatua ile ile aliyonayo bidii inampeleka mtu kutoka hatua moja ya mafanikio kwenda hatua nyingine  kama unataka kuheshimika fanya kazi kwa bidii bidii itakupa heshima  itakufanya ukae na watu wenye cheo inawezekana unadharaulika katika jambo unalolifanya wala hakuna mtu anayetambua mchango wako fanya kwa bidii bidii itakuletea heshima.

 • Uvivu humfanya mtu aambatane na uharibifu

Mithali 18;9 “Yeye aliye mvivu katika kazi yake  ni ndugu yake aliye mharabu”

mtu mvivu kamwe hawezi kuwa rafiki wa mtu mwenye bidii kwa sababu mwenye bidii hana muda wa kuambatana na watu ama vitu visivyo na tija kwenye maisha mwenye bidii huwaza mafanikio tena anaambatana na watu ama vitu vitakavyomfanya afanikiwe;   kuna msemo unasema “An idle mind is evil’s workshop” maana yake ufahamu ama akili ya mtu asiyejishughulisha(mtu mvivu) ni kiwanda  cha maovu ndiyo maana  maandiko yanatuambia mtu mvivu huambatana na uharibifu kwa sababu kama jinsi ambavyo mtu mwenye bidii huwaza mafanikio vivyo hivyo mtu mvivu huwaza uharibifu.

 • Bidii hutajirisha

Mithali 10:4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini bali mkono wa mwenye bidii hutajirisha.

Unataka kufanikiwa ni lazima uwe mwenye bidii; bidii ni kutochoka, kutokuvunjika moyo kutokukatishwa tamaa mwenye bidii haishii njiani mwenye bidii huendelea mbele hadi atakapoona utimilifu wa malengo na maono yake.

VITA YA UVIVU

Uvivu ni vita  ambayo ni lazima ujitoe kupingana nayo ili uishinde. Uvivu una mashabiki wengi sana.

Shabiki wa kwanza wa uvivu ni  ufahamu wako linapokuja wazo la kukutaka ufanye jambo Fulani lenye tija, wazo lingine linakuambia usifanye au utafanya siku nyingine.

shabiki mwingine wa uvivu ni mwili wako ambao utakutia uchovu ili uone kana kwamba huwezi kufanya hilo jambo kwa muda huo.

DALILI KUU ZA UVIVU

 • Kupenda usingizi ,unalala muda mwingi kuliko muda unaofanya kazi, aidha unathamini usingizi kuliko hata malengo uliyonayo mithali 26;14
 • Kuhairisha hairisha mambo unapanga jambo na kuhairisha bila sababu ya msingi mithali 26;13
 • Kuishia njiani ni pia ni dalili moja wapo ya uvivu unaanza jambo fulani vizuri ukikutana na changamoto badala ya kutatua hizo changamoto kwa sababu ya uvivu unaachana na jambo hilo.
 • Kutumia muda mwingi kwenye mambo yasiyo na maana kama vile kuchati, kuangalia muvi, kukaa vijiweni, kupiga umbea n.k mithali 26;11
 • Kutokuwa na ratiba maalumu kwa maana ya kwamba unaweza kufanya chochote kwa wakati wowote kwa sababu huna ratiba maalumu.
 • Kutokuwa na malengo wala mikakati ya kufikia malengo hayo.
 • Hataki kujifunza hujiona sawa kwa kila jambo mithali 26;16

JIFUNZE KUFANYA KWA NGUVU ZAKO ZOTE

Ili ufanikiwe ni lazima ufanye jambo kwa nguvu zako zote za akili, nguvu zako zote za hisia, nguvu zako zote za roho na nguvu zako zote za mwili.

Muhubili 9:10 Lolote mkono wako ukakapolipata kulifanya lifanye kwa nguvu zako zote kwa kuwa hakuna kazi wala shauri wala maarifa wala hekima huko kuzimu uendako

Muhubili ametukumbusha kufanya kwa nguvu zetu zote swali la kujiuliza ni je mambo yale Mungu amekupa kuyafanya je unayafanya kwa nguvu zako zote

 • Je unamtumikia Mungu kwa nguvu zako zoteUnatumia karama na kipawa Mungu alichokupa kwa nguvu zako zote?
 • Unafanya kazi Mungu aliyokupa uifanye kwa nguvu zako zote?

ILI UWE NA BIDII.

Bidii huchochewa na kuhamasishwa  hii ni kwa sababu asili ya mwili ni uvivu mwili haupendi kutaabishwa kwa namna yoyote ile  lakini ili ufanikiwe ni lazima ukubali kuutaabisha mwili  yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yatachochea bidii  yako.

 • Hamasa ya utimilifu wa maono uliyonayo

Matamanio ya kuona na kuishi maono uliyonayo ni kati ya mambo yenye nguvu kubwa ya kuchochea bidii yako maono uliyonayo ni kitu cha kujikumbusha hasa pale unapohisi uchovu au uvivu wa kufanya jambo fulani. Jikumbushe jinsi ambavyo unatamani kuyaishi maono uliyonayo, jikumbushe jinsi ambavyo uvivu wako ni kikwazo kikubwa sana katika kuyafikia maono yako,  unapotafakari mambo haya utapata nguvu mpya na uvivu wa mwili utaondoka.

 • Jiwekee mipaka ya muda wa kukamilisha jambo

Unataka kukamilisha jambo kwa muda gani ? usifanye jambo lolote bila ya kujiwekea (time flame) Muda wa kukamilisha jambo hilo; Mwalimu anapotoa kazi shuleni huwapa wanafunzi muda wa kukamilisha kazi hiyo, vivyo hivyo taasisi hujiwekea muda wa kukamilisha malengo yake.  Jiwekee muda maalumu wa kukamilisha jambo fulani na uhakikishe unakamilisha ndani ya muda huo hii itakusaidia kuchochea bidii uliyonayo na kukamilisha mambo yako kwa wakati.

 • Ishinde asili ya mwili

Maandiko yanasema mtu mvivu huutia mwili wake katika usingizi mzito.

Anayeamua jinsi mwili unatakiwa uishi ni mtu mwenyewe mwili umepewa kutii amri ya mtu. kumbuka kuwa Mungu ametupa mwili utusaidie katika kutimiliza kusudi lake tukiwa hapa duniani kumbuka kuwa mwili una asili yake, maandiko yanatuambia kuwa nia ya mwili ni mauti (warumi 8;6) hii inamaanisha mwili hauna asili ya kumfanya mtu afanikiwe kwa hiyo ili mtu afanikiwe ni lazima ajue jinsi ya kuwa na amri kwa mwili wake. Tunamshukuru Mungu aliyeupa mwili kutii  jinsi vile wewe unavyotaka uenende ndio maana ukiuzoesha mwili kuamka kila siku saa kumi na moja asubuhi siku za mwanzo mwili utapingana sana na wewe, lakini baada ya muda mwili utatii kile unachotaka mwili ukishatii utajikuta kila siku saa kumi na moja tayari uko macho hatakama haujaweka kitu chochote cha kukusaidia kuamka. mwili utafanya hivyo pia unapotaka kujiwekea muda maalumu wa kulala, mwili utafanya hivyo unapotaka kujiwekea mazoea ya kufanya jambo lolote lile  ukitaka kuwa mwenye bidii ni lazima ukubali kushinda asili ya mwili kwa sababu mwili unatii kile unachotaka wewe.

 • Hamasa ya kujua zaidi

“Moyo mwenye busara hupata maarifa na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa” mithali 18:15

Maandiko yanatuambia kutafuta maarifa ni hekima, tena ni busara.  Hekima na busara ni kiwango cha juu zaidi cha kuweza kutatua matatizo yako binafsi na matatizo ya wengine.

Hamasa ya kujua zaidi itakupatia maarifa, maarifa yatakupatia hekima kwenye eneo husika. Hamasa ya kujua zaidi itakufanya utafute maarifa zaidi kwenye kazi yako, kwenye ndoa yako, kwenye biashara yako,  hamasa ya kujua zaidi itakufanya uwe na bidii  na kukusaidia kutunza muda wako vizuri  hivyo basi ukitaka kuwa na bidii ni lazima uwe na hamasa ya kujua zaidi kama kichocheo muhimu cha kukufanya utafute maarifa zaidi ili uwe na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali kwenye eneo hilo unalolitafutia maarifa.

 • NGUVU YA MAOMBI

Kuna wakati nguvu zetu zinafika mwisho kuna wakati tunakata tamaa na kuona kana kwamba atuwezi kuendelea mbele kunawakati tunaona kama bidii yetu haizai matunda yanayotarajiwa  Yesu alipokuwa anakaribia mateso maandiko yanatuambia jinsi ambavyo alitambua kwamba nguvu za mwili pekee hazitoshi Yesu akasema Roho Iradhi lakini mwili ni dhaifu Ndipo yesu akaanza kuomba  ndipo malaika wa Mungu wakaja kumfariji na kumtia nguvu. Kuna wakati wanafunzi wake walimuuliza yesu kuhusu jambo fulani kubwa alilolifanya walimuuliza yanawezekanaje mambo haya yesu akajibu akawambia kwamba namna hii haiwezekani ila kwa kufunga na kuomba.

Tunamuhitaji Mungu  kwa njia ya maombi  atuwezeshe atusaidie atutie nguvu  kwa sababu nguvu zetu pekee hazitoshi, hivyo unapofanya jambo lolote kwa bidii yakupasa uombee jambo hilo kwa bidii sana, ili nguvu ya Mungu ikusaidie pale nguvu ya mwili inapofika mwisho,  mwili unapokuwa dhaifu na kukata tamaa katika maombi yote yanawezekana.

 • Hamasa ya kutobaki jinsi ulivyo leo

Mara kadhaa ninapotaka kukata tamaa, kuchoka ama pale ambapo  mazingira yananivunja moyo huwa najikumbusha  na kujiuliza jambo hili muhimu “Je nataka kubaki jinsi nilivyo, je nakubaliana ama nimeridhika na hali niliyonayo sasa” huwa najikumbusha kwamba ninapokata tamaa najicheleweshea mafanikio yangu mimi mwenyewe.Ninapojikumbusha namna hii Napata nguvu mpya  na bidii yangu inachochewa  kwa sababu ya hamasa ya kutobaki jinsi nilivyo. Ni lazima tuelewe kuwa watu wengi tunaowaona wamefanikiwa sasa kuna wakati walikubali kutesa miili yao kuna wakati walijinyima kuna wakati hawakulala usingizi wa kutosha kwa sababu tu walikuwa na hamasa ya mabadiliko swali la kujiuliza ni je kama wao waliweza kwanini wewe ushindwe?

Bidii na uvivu vyote ni vitu ambavyo ni asili ya mwili mwili una tii wewe unataka nini na unapenda nini unapenda uvivu mwili utakufanya uwe mvivu unapenda kuwa na bidii mwili utakufanya kuwa na bidii

Bidii ama uvivu vyote hutegemea maamuzi ya mtu mtu anaamua kuwa mvivu ama kuwa na bidii, Uvivu ama bidii vyote vina matokeo m uvivu una matokeo na bidii una matokeo.

Matokeo huletwa na bidii katika kile unachokifanya ukitaka matokeo makubwa ni lazima ukubali kujibidiisha zaidi.

Kumbuka kuwa mtu mvivu huthamini starehe kuliko kazi hupenda sana usingizi na kukaa vikao visivyo na faida  Muda wa mtu mvivu hupotea bure  mtu mvivu ni mzigo kazini kwake ni vigumu sana kufanya kazi na mtu mvivu, tena ni changamoto kubwa kumuongoza mtu mvivu  mtu mvivu ni sumu ya mafanikio tofauti kabisa na mtu mwenye bidii yeye huthamini muda wake na kuutumia ipasavyo hufanya majukumu yake kwa wakati  mwenye bidii hupendwa  na kuheshimiwa  katika kazi yake mwenye bidii ni chachu ya  mafanikio kumbuka ni wakati huu wa sasa unatakiwa ufanye bidii katika jambo unalolifanya ili ufaidi matunda mema ya kazi yako unataka kufanikiwa, unataka kuwa na heshima unataka kutawala inawezekana kama ukikataa uvivu na kuambatana na bidii.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Emmanuel Mwakyembe kupitia:
Simu/WhatsApp: +255 716 531 353/+255 766 939 969
Facebook Profile: Emmanuel Mwakyembe
Istagram: @emmanuelmwakyembe
Email: emamwakyembe@gmail.com

Like Page yetu ya facebook > GOSPOMEDIA.COM instagram: @gospomedia

More in Uncategorized

To Top