Habari

Gabola ndio Kanisa pekee la walevi linalosifu na kuabudu unywaji wa pombe.

Gabola ni kanisa jipya lililopo nchini Afrika Kusini ambalo limekuwa likiwashangaza watu wengi kwa namna ya uendeshaji wa huduma zake.

Kanisa hilo linalofahamika kwa jina Gobola (yaani nipe Ulevi ninywe kidogo kwa Lugha ya Kitswana, moja ya lugha rasmi nchini humo) lina mwaka mmoja hivi tangu kuanzishwa kwake.

Mwasisi wa kanisa hilo ni Tsietsi D Makiti, 53, ambaye kwa sasa anajiita Papa Makiti. Hujieleza kama papa wa kwanza mweusi kutoka bara la Afrika.

Alilianzisha kanisa hilo katika baa moja, na kanisa hilo hufanya ibada zake katika baa na vilabu.

Kanisa kuu la Gobola limo ndani ya baa inaitwa Freddie’s Tarvern na mwenye baa hiyo Askofu Freddie Mathebula ndiye naibu wa Papa Makiti, husaidia kuongoza mahubiri na ibada wakati mwingine.

Tangu kuanzishwa kwake, kanisa hilo limekuwa likipata umaarufu na inakadiriwa kwamba kwa sasa lina waumini kati ya 500 na 2,000, ingawa idadi yenyewe ni vigumu kuithibitisha.

Kanisa la Gobola lina watu wa tabaka mbali mbali wanaume kwa wanawake na ndani yake kuna vyeo sawa na ilivyo kwenye makanisa na madhehebu mengine. Mfano wamo wachungaji, makasisi na maaskofu lakini hakuna kadinali.

Kila siku ya Jumapili wasaidizi wa Papa Makiti wanavalia rasmi mavazi yao ya upadri.

Lakini mwenyewe anasema siyo hoja kujuwa wapi walikosomea mafunzo ya dini ya Kikristo kuweza kupewa vyeo hivyo jambo ambalo Baraza kuu la makanisa Afrika Kusini huwa linalisisitiza kwamba ni muhimu katika kanisa lolote lile.

Baraza la makanisa lenye makao yake mjini Johannesburg nchini Afrika kusini limesema halikubaliani kabisa na mafundisho ya kanisa la Gobola na kwamba ni njia moja ya kuwapotosha wafasi wa dini ya Kikristo.

Papa TD Makiti naye amekua akiwalaumu viongozi wa baraza la makanisa kusini mwa Afrika kuwa hawana mamlaka ya kumshutumu wala kumhukumu kwa anayoyafanya.

Amesema mwenye uwezo wa kumhukumu ni Mwenyezi Mungu peke yake, na kwamba ni dhambi kubwa kwa hao wanaomtuhumu na adhabu yao watakwenda motoni.

Papa Makiti anasema Kanisa la Gobola halitaki kutegemea sana misaada kutoka kwa wahisani na ndio maana wanawahimiza wanachama wao kununua pombe kwa wingi, kutoka duka lao lililopo ndani ya kanisa na hivyo kulifanya kanisa la Gobola kulipa kodi ya serikali.

Katika kanisa hilo, watu huwa hawatoi sadaka, mapato hutoka kwa mauzo ya bia na vileo vingine.

Kwa upande mwengine Kanisa la Gobola halina tofauti na makanisa mapya yanayoanzishwa Afrika Kusini kila kukicha kama kitega uchumi, viongozi wao kutajirika sana na wengine kumiliki hata ndege za kibinafsi.

Kanisa hili pia lina nyimbo zao walizotunga wenyewe, miongoni mwa hizo ni pamoja na ule uitwao Gabola Mpepe unaosema ‘Ninapoonja kidogo, huwa na lewa lewa, hii haina maana kwamba huwa sifuati njia iliyonyooka’.

‘Walevi wote ni wanachama’

Kwa sasa Kanisa la Gobola lipo na linatarajiwa kuendelea kuwepo na wengi wa wanywaji pombe, bia na vileo vikali ukizungumza nao kuhusu kanisa hilo wanakwambia ni mpango mzuri walevi nao wajihisi wana kundi la kuwatetea.

Kanisa la Gobola linasema kila mlevi nchini Afrika Kusini ni mwanachama wa kanisa hilo na wala haina haja ya kujua kuna idadi ya walevi wangapi walio nchini humo.

Wote wanakaribishwa kwa mikono miwili ya Papa Makiti mkono wa kulia ukiwa na chupa ya kileo na mkono wa kushoto ukiwa na kitabu cha Biblia.

Ili kuwa mwanachama kamili lazima Papa Makiti akubatize kwa pombe unayoipenda zaidi, inaweza kuwa Johnnie Walker, Red Label, Guinness, Smirnoff na kama ingekuwa Afrika Mashariki pengine Serengeti, Castle, Tusker au hata Konyagi.  “Iwapo wewe hunywa bia, basi unabatizwa kwa bia,” Papa Makiti anasema.

Chanzo: BBC Swahili

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Audio: Neema Mudosa-Umenitoa Mbali

Next post

Audio: Ambwene Mwasongwe-Tumekubalika