Habari

Jukumu la Kuliombea Taifa lipo mikononi mwa watanzania wenyewe – Naibu Waziri

Na Peter Mkwavila, Dodoma
Naibu Waziri wa Kilimo Dk Mary Mwanjelwa amewakumbusha waumini wa kanisa la Assemblies of God -Mlima wa Moto lililopo eneo la Sabasaba, mjini Dodoma kuongeza bidii katika kuifanya kazi ya Mungu kwa malengo ya kuwagusa wanadamu ili waweze kumkimbilia Yeye, na hatimaye waachane na maovu.

Dk Mwanjelwa ambaye ni mshirika wa kanisa hilo ambalo kiongozi wake mkuu ni mchungaji Dk Getrude Rwakatare, alitoa neno hilo alipopewa nafasi ya kusalimia waumini katika ibada iliyofanyika kanisani hapo, hivi karibuni.
Awali, naibu waziri huyo aliwaambia waumini hao kuwa jukumu la kuliombea Taifa na serikali iliyopo madarakani lipo mikononi mwa watanzania wenyewe ambao wanaomba kwa uaminifu na kwa ukweli.

Alisema kuwa Watanzania walio waaminifu kwa nchi na serikali yao ndiyo watakaolifanya Taifa liwe na amani, utulivu, upendo na mshikamano, jambo ambalo alisema linawapa nafasi wao kama Wakristo kuendelea kuabudu kwa uhuru, na hata kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo bila hofu.

Hata Rais mwenyewe na wasaidizi wake wanategemea maombi kutoka kwa watanzania wanaoipenda nchi yao kwa kuiombea, hivyo ninawaomba waumini wezangu tuendelee kumwombea kiongozi wetu huyu ili utendaji wake usije ukatetereka kwa kukosa msaada wa maombi yenu, alisema.

Mchungaji wa kanisa hilo, Silivanus Komba alisema kuwa kwa upande wao kama kanisa la mahali, wamejiwekea utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu kufanya maombi kwa ajili ya Rais wa nchi pamoja na viongozi wengine wa serikali ili waweze kuwatumikia watanzania kwa uaminifu na kwa hofu ya Mungu.

Alisema kanisa hilo litaendelea kuwajibika katika kuomba ili viongozi na watendaji wa serikali iliyoko madarakani watimize wajibu wao katika kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.

Chanzo: Mwanzo News

Like facebook page >> GOSPOMEDIA  Follow instagram page >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Music Audio: Vanesa Kasoga - Tangulia

Next post

Music Video | Music Audio: Benachi - Hallelujah