Connect with us

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu ya Kwanza

Mafundisho

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu ya Kwanza

Na Dr. Jacob Makaya,

Yesu alipoulizwa juu ya nyakati za mwisho na ujio wake, kitu cha kwanza kabisa alisema ni: “Angalieni mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu,wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi” (Mathayo 24:4—5).

Kwa hiyo, kutokana na maneno ya Yesu, siyo kila anayekuja kwa jina lake ametumwa na Yesu. Siyo kila anayetumia jina la Yesu ni mtumishi wa Mungu. Kuna watumishi wa Shetani ambao wanatumia jina la Yesu kwa kusudi la “kudanganya wengi.”

Yesu alisema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).

Inapofika kwenye kuzungumzia juu ya watumishi wa uongo, watu wengi wanapenda kusimamia msitari huu: “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi” (Mathayo 7:1).

Haya ni maandiko ambayo Shetani huwa anayaweka katika mioyo ya watu ili uovu usikemewe.

Kumbuka ni hatari sana kuingia kwenye Biblia na kuchukua msitari mmoja bila kuelewa kile Mungu alikuwa anasema.

Yesu mwenyewe alisema, “Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki” (Yohana 7:24).

Pia Paulo aliandika, “Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya Maisha haya?” (1 Wakorintho 6:2—3).

Hivyo Yesu aliposema “msihukumu, msije mkahukumiwa” alikuwa anazungumza nini kwani Yesu huyo huyo anazungumza pia “kufahanya hukumu iliyo ya haki?”

Biblia inasema, msingi wa kiti cha enzi cha Mungu ni haki na hukumu (Zaburi 89:14). Neno la Mungu ndiyo kipimo chetu katika kuhukumu matendo yasiyotokana na Mungu.

Mfano: Kama Biblia inasema “usiibe” halafu ukaona mtu anaiba na kumwacha ukisema “Yesu alisema tusihukumu.” Neno linasema, “usizini.” Je ukiona mtu anaishi ya zinaa, utaacha kumwambia eti “Yesu alisema tusihukumu?”

Yesu alichokataza ni sisi kutoa hukumu ya macho ambayo haitokani na neno la Mungu. Lakini ni haki yetu kutoa hukumu ya haki kutokana na neno la Mungu linavyosema. Hata katika utumishi ni hivyo hivyo.

Neno linasema, “kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo ya giza, bali myakemee” (Waefeso 5:9—11).

Unabii wa uongo na kuwapotosha watu ni moja ya “matendo ya giza” ambayo tunatakiwa tuyakemee. Kwa mfano, Biblia inasema, “Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo asilonena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope” (Kumbukumbu 18:22).

Kwa lugha nyepesi, nabii anayetabiri kwa jina la Bwana halafu havitokei, huyo ni NABII WA UONGO.

Roho Mtakatifu hawezi kumuongoza mtu kutabiri uongo kwani neno linasema, anatuongoza katika kweli (Yohana 16:13).

Biblia iko wazi kabisa kuwa “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa kwa Roho Mtakatifu” (2 Petro 1:20—21).

Kuna manabii wa uongo ambao ni rahisi kuwatambua na wengine siyo rahisi. Mfano wa manabii wa uongo ambao ni rahisi kuwatambua ni wale ambao wanatabiri vitu halafu havitokei kama walivyotabiri.

Kwa mfano, unapoona TB Joshua anatabiri halafu havitokei kama alivyotabiri, hiyo inakuambia kuwa huyo ni nabii wa uongo.

Manabii kama Joshua wanaotabiri vitu halafu havitokei, hao ni rahisi kuwatambua. Shida ni kuwatambua manabii wa uongo ambao wanatabiri vitu na vinatokea.

Kumbuka kipimo cha manabii wa ukweli au wa uongo siyo wao kutumia “jina la Bwana.” Ile kwamba mtu anatabiri na kusema, “Bwana amesema” haina maana huyo ni nabii wa ukweli.

Manabii wa uongo hawana alama usoni ilivyoandikwa “Mimi ni nabii wa uongo.” Biblia imetuonya kwamba, “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu wakati” (Mathayo 7:15).

Biblia imeweka wazi kuwa “Mtawatambua kwa matunda yao” (Mathayo 7:16).

NJIA ZA KUWATAMBUA MANABII WA UONGO.

  1. ROHO YA UTAMBUZI:

Manabii wengi wa uongo wanatumia “roho ya utambuzi” ili watu wawaamini kuwa ni watumishi wa Mungu. Ile kwamba mtu anaweza kukwambia jina lako, unatoka wapi, ulizaliwa lini, una watoto wangapi, n.k. haina maana ni nabii wa kweli.

Roho au pepo ya utambuzi ni njia ambayo Shetani anaitumia kudanganya watu. Mtu anaweza kuwa na roho ya utambuzi kwa ajili ya kupata faida kifedha.

“Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua” (Matendo 16:16).

Mtu huyu alitumia pepo wa uaguzi kupata faida kama jinsi ambavyo manabii wengi wa uongo wanatumia roho ya utambuzi ili kupata faida.

Kazi kubwa Shetani anayoifanya ni kujaribu kukushawishi ili ufikiri kwamba Mungu ndiye anafanya, kumbe Shetani ndiye anafanya.

  1. WATU WANAOJIINUA BADALA YA KUMUINUA MUNGU:

“Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake” (Matendo 8:9—11).

Nataka uone kuwa huyu mtu alikuwa mchawi, lakini watu walidhani ametoka kwa Mungu. Kwa hiyo, inawezekana kabisa mtu kuwa anatumia uchawi halafu ukadhani anatokana na Mungu.

[Kwa mfano: Biblia inatumwambia yule mwanamke ambaye ni MAMA WA MAKAHABA (Kanisa lililozaa makanisa mengine) (Ufunuo 17:5) linatumia uchawi kudanganya watu (Ufunuo 18:23)].

Lakini nataka tujifunze kitu cha msingi kutoka kwa huyu mchawi katika Matendo 8. Biblia inasema, huyu mtu alikuwa “akisema yeye ni mtu mkubwa.” Unapoona mtumishi anajitukuza na kusema yeye ni mtu mkubwa na kufanya ishara nyingi, huyo anatokana na Shetani.

Shetani tangu mwanzo alikuwa mtu wa kujiinua sana. Hivyo hii roho hata kwa watumishi wake utaikuta. Ukishaona watu wanasema wao ni “Big Prophet, Major Prophet, Major One, ” na majina mengine kama hayo, inatakiwa ikuambie kitu.

Kwenye Biblia, hakuna nabii wa Mungu hata moja ambaye alijiinua. Wote walimwinua Mungu kwani hawakutafuta utukufu wao, bali walitafuta kumpa Mungu utukufu. Yesu alisema, mtu anayetaka kuwa mkubwa na awe mtumishi (Mathayo 20:26).

Hivyo ukishaona watu wanajisifu na kujiinua badala ya kumuinua Mungu katika Kristo Yesu, wanatumia roho ya Shetani.

  1. BIASHARA YA UPAKO:

Ukisoma habari za yule Simoni aliyekuwa mchawi, neno linasema, “Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka” (Matendo 8:13).

Ukiendelea kusoma, neno linasema, “Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono na mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu” (Matendo 8:18—19).

Kwa lugha nyingine, Simoni alitaka “kununua upako.” Yesu alipokuwa anawapa upako wanafunzi wake, alisema, “mmepata bure, toeni bure” (Mathayo 10:8b).

Ukishaona nabii au mtumishi anafanya biashara ya “kuuza upako,” huyo ni “mtumishi wa Shetani.” Roho Mtakatifu hawezi kuongoza watu kuuza upako kwani Biblia inasema, Roho Mtakatifu anagawa karama mbalimbali kwa kadri apendavyo (1 Wakorintho 12:4—11).

Ukiona watu wanauza “maji ya upako, mafuta ya upako, sabuni za upako, kitambaa cha upako n.k.,” hiyo inatakiwa ikuambie kuwa hao wanatokana na Shetani. Ukifatilia, huo upako hautokani na Roho Mtakatifu, bali Lucifer.

Kuna madhara makubwa sana ya kununua hivi vitu kwani unapovinunua, unajiunganisha na miungu yao na Shetani anakuwa na uhalali wa kufunga maisha yako. Kwenye Biblia hamna “biashara ya upako” ila hii ni mbinu ambayo watumishi wa Shetani wanaitumia kupata fedha nyingi.

Kuna mtu mmoja alinunua mafuta ya upako kwa nabii mmoja mkubwa wa uongo wa Nigeria na baada ya hapo, aliona mambo ya ajabu.

  1. MATUNDA YAO:

Utawatambua watumishi kwa “matunda yao” na siyo “karama zao” kwani siyo kila karama zinatokana na Mungu. Asilimia kubwa wanatumia nguvu za giza, bali wanadanganya watu kuwa ni nguvu za Mungu.

Hivyo angalia kama wanazaa “tunda la Roho” (Wagalatia 5:22—23). Usiangalie kwamba wanatabiri au wanafanya miujiza mingi bali angalia wanapeleka moyo wako wapi: Kwa Mungu au kwa miungu yao? (Kumbukumbu 13:1—4).

Utaangalia matunda yao kwako kwa kuangalia kama unapata nguvu ya kuomba, nguvu ya kusoma neno, na kiu ya kumtafuta Mungu na ufalme wake. Ukiona baada ya unabii moyo wako uko kwenye pesa na mambo ya dunia hii, hiyo inatakiwa ikuambie huyo siyo mtumishi wa Mungu.

  1. KUWA NA NENO:

Biblia inasema, “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote” (Wakolosai 3:16). Kuwa na neno la Mungu ndio kitu cha muhimu kuliko vyote.

Mtu kama hana neno la Mungu, hawezi kutofautisha kati ya nabii wa ukweli na nabii wa uongo kwani atawaona wote wanatumia Jina la Yesu. Mtu asiye na neno hawezi kutofautisha kati ya “kondoo” na “mbwa—mwitu mwenye mavazi ya kondoo” kwani atawaona wanafanana.

Siku moja nilikuwa namsikiliza mtumishi mmoja akasema: “Mtoto mchanga katika Kristo anafikiri TB Joshua ni mtumishi wa Mungu” kwani hawezi kutofautisha mema na mabaya (Waebrania 5:13—14).

Mtu ambaye hana neno la Mungu atakuwa anatumia “macho ya nje” badala ya kutumia “macho ya ndani.” Biblia ilisema wazi kuwa tuzijaribu roho kama zinatokana na Mungu (1 Yohana 4:1).

Siyo rahisi “kuzijaribu roho” kama hajui “namna ya kuzijaribu” kwa kutumia neno la Mungu. Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga wowote ukatao kuwili (Waebrania 4:12). Manabii wa uongo wote wana “upanga ukatao kuwili.”

Biblia imetuonywa kuwa nyakati hizi watu watajitenga na imani na kusikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani (1 Timotheo 4:1).

Mtu asiye na neno, hawezi kutofautisha “mafundisho ya Mungu” na “mafundisho ya mashetani” kwani yote yanatoka kwenye Biblia. Mtu asiye na neno, hawezi pia kutofautisha kati ya “kanisa la Mungu” na “kanisa la Shetani.”

Hivyo ni muhimu kuwa na “neno la kutosha” ili uweze kuzijua roho zinazotokana na Shetani ili kudanganya watu. Ukiwa na neno la Mungu, utajua kazi za manabii katika Biblia zilikuwa zipi. Hivyo manabii wa uongo utawatambua kirahisi kwani watakuwa wanaenda tofauti na neno la Mungu.

HATARI YA KUTOPOKEA KWELI YA MUNGU.

Kuna hatari kubwa sana ya kukataa kweli ya Mungu na kutaka unabii wa aina fulani. Ukikataa kweli ya Mungu, Mungu atakuletea manabii wa uongo ili upotee.

Ukisoma habari za Ahabu, neno linasema, “Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya” (1 Wafalme 22:18)?

Mfalme aliona kila mara anatabiriwa “mabaya” badala ya kuangalia kuwa anatabiriwa “ya kweli.” Kwa sababu hakuwa tayari kuipokea kweli ya Mungu, Mungu alimletea wakumdanganya.

“Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth—Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo” (1 Wafalme 22:20—22).

Hapa tunaona Mungu akiruhusu pepo wa uongo waende kumdanganya Ahabu kwani hakutaka kupokea kweli ya Mungu. Unapozidi kuikataa kweli ya Mungu, Mungu anakuletea wa kukudanganya.

Ukisoma habari za mpinga Kristo, Neno linasema, “yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyanyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo” (2 Wathesalonike 2:9—11).

Kuna watu ambao wamekuwa wakitafuta utabiri na wanatoka kwa nabii mmoja kwenda kwa nabii mwingine. Pamoja na kutabiriwa kuwa matajiri, bado wapo pale pale. Kibaya wengine wamejikuta wanapata roho za kutoka kwa Shetani zinazowatesa.

Kinachotakiwa ni kuishi kwa neno la Mungu na kumtegemea yeye. Yesu aliweka wazi kuwa mlango mpana unaenda upotevuni.

Ahadi za Mungu kwa wana Israeli ni kwamba wakitii watabarikiwa, wasipotii watalaaniwa (Kumbukumbu 28). Ahadi ya Mungu kwetu ni tuutafute ufalme wake kwanza na haki yake; na mahitaji yetu yote atatuzidishia (Mathayo 6:33). Mbali na hapo, ni roho ya unabii wa uongo.

KWA NINI WAFUASI WENGI WA MANABII WA UONGO SIYO RAHISI KUTOKA HUKO?

Wafilipi walipofanikiwa kumkata Samsoni, kitu cha kwanza walifanya ni kumtoboa macho ili asiweze kuona (Waamuzi 16:21).

Katika ulimwengu wa roho ni hivyo hivyo. Shetani akikamata mtu kitu cha kwanza anafanya ni kumpiga upofu ili asione kama anadanganywa.

Maombi yetu kwako Mungu akusaidie kusimama katika kweli ili usidanganywe.

Somo litaendelea… .. Mungu akubariki sana kama umeguswa na somo hili, Amen. Mimi ni mtumishi Jacob Makaya, PhD – Kingdom of Heaven Ministry.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top