Jinsi ya Kufanikiwa Sehemu Ya nne: Ijue Nguvu ya Nidhamu katika Mafanikio Yako. - Gospo Media
Connect with us

Jinsi ya Kufanikiwa Sehemu Ya nne: Ijue Nguvu ya Nidhamu katika Mafanikio Yako.

Uncategorized

Jinsi ya Kufanikiwa Sehemu Ya nne: Ijue Nguvu ya Nidhamu katika Mafanikio Yako.

Nidhamu ni ile hali ya kuweza kujiwekea utaratibu fulani katika maisha na kuweza kuufuata ama kufuata utaratibu fulani uliowekwa, ni hali ya kuweza kujizuia kwa baadhi ya mambo ili ufanikishe mambo ya muhimu zaidi kwenye maisha ikiwa ni pamoja na kujiepusha na kitu chochote kile ambacho kinaweza kukuzuia au kukuchelewesha kufikia maono yako au mafanikio yako kwa namna moja ama nyingine.

Mafanikio kwenye maisha yanahitaji nidhamu ya hali ya juu, pia mafanikio yanahitaji kujitoa na kuingia gharama kwani kuna wakati utatakiwa kujizuia  katika baadhi ya mambo si kwamba ni mabaya ila tu ni kwa sababu ni kikwazo kwa safari ya kuyafikia mafanikio yako au kutimiza maono yako. Hivyo basi nidhamu ni hali ya kujiwekea misimamo itakayokuwa ni muongozo wa kukusaidia kuwa vile unavyotaka kuwa. Hapa hujumuisha misimamo ya kitabia, kimaadili na kiimani. Nidhamu ni kujitengenezea mfumo wa maisha utakaokuongoza kuyafikia mafanikio yako au kuyatimiza maono yako pamoja na kuhakikisha unauheshimu huo mfumo uliojiwekea.

Jipime kiwango chako cha nidhamu katika mambo yafuatayo:

 • Je ukipanga ufanye jambo Fulani kwa muda fulani unalifanya kwa muda huo?
 • Unaheshimu ratiba yako kwa kiwango gani je unasikia uchungu kiasi gani unapokwenda tofauti na ratiba yako?
 • Unaheshimu Muda kwa kiasi gani Je umepangiliaje matumizi ya Muda wako kwa siku mwezi mwaka.
 • Je muda wako haupotei pasipo sababu ?
 • Je una msimamo gani katika kuipuza tamaa ya mwili ili uyafikie malengo fulani uliyojiwekea.

Nidhamu ni msimamo wa kusimamia kile unachokiamini kwa kiwango cha juu cha uaminifu mpaka kimekuwa vile ulivyotarajia.

Nidhamu ni kupuzia matakwa ya mwili kwa ajili ya kusimamia malengo uliyojiwekea.

Nidhamu ni kusema  hapana kwa baadhi ya mambo ambayo hukuyapangilia ama hayakuwa kwenye ratiba yako.

Nidhamu ndiyo siri pekee inayomuwezesha mtu mmoja kufanya mambo mengi kwa muda mchache, utajiuliza inakuwaje mtu huyo huyo anafanya biashara, huyohuyo ni mfanya kazi, huyo huyo ana huduma bado ana familia   anawezaje kufanya mambo yote haya kwa mafanikio makubwa? siri kubwa ni nidhamu. Nidhamu inamuwezesha mtu huyu kusimamia ratiba yake na kwenda sawa sawa na namna alivyoyapangilia mambo yake.

Nidhamu ni nguzo ya muhimu sana katika kufanya jambo fulani lifanikiwe.

Kwa nini sheria zinatengenezwa na kuwekewa ulazima wa kila mmoja kuzifuata?

Kwa nini kwenye maofisi  huwekwa sera katiba na miongozo ya kazi

Utawekewa muda wa kufika kazini na muda wa kutoka aina za nguo unazotakiwa kuvaa , mambo unayotakiwa kuyafanya na usiyotakiwa kuyafanya, pia utawekewa (targets) mambo ambayo unatakiwa kuyafanikisha kwa muda fulani, wakati wote mfanyakazi anapokuwa kazini anawajibika kufuata na kuenenda sawa sawa na muongozo na matakwa ya kazi yake,  pindi anapokwenda kinyume huchukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kulingana na uzito wa makosa yake.

Mambo haya yote hutengenezwa na taasisi husika ili kuwawezesha wafanyakazi kufanya kazi kwa namna itakayosababisha taasisi husika kufikia malengo yake.

Adui wa kwanza wa mafanikio ya mtu  ni mtu mwenyewe, asili ya mwili wa mwanadamu hupingana na vitu vyenye tija ama vitu vya  mafanikio. Asili ya mwili ni tamaa , asili ya mwili ni kupenda mambo ya anasa  mwili haupendi kujishughulisha ama kufanya kwa bidii nidhamu pekee ndicho kitu kinachouwekea mwili msisitizo wa kufanya kama inavyopaswa kufanywa ili kufanikisha jambo fulani.  Kama jinsi ambavyo taasisi huweka sheria na miongozo kwa wafanyakazi ili kuwatengenezea nidhamu ya kazi ndivyo ambavyo mwili unapaswa uwekewe miongozo na sheria mbali mbali ili umletee mtu mafanikio kwa mfano mwanafunzi bora ni yule anayejiwekea ratiba ya kusoma na kuhakikisha anaifuata ratiba hiyo, kuna wakati atatakiwa aamke usiku kusoma, japo kuwa mwili unapenda usingizi  nidhamu itamsaidia mwanafunzi huyu kuhakikisha anafuata ratiba yake atatakiwa afuate sheria zote zilizowekwa na shule na kusikiliza matakwa ya shule husika haya yote atatakiwa kuyafanya ili afanikiwe katika masomo yake.

 • Kukosa nidhamu ya maisha kumewafanya wengine kufanya dhambi ya kuua kwa kutoa mimba ambazo hawakutarajia.
 • Kukosa nidhamu kumewafanya wengine kuuza usichana wao.
 • Kukosa nidhamu kumewafanya wengine wapoteze kazi.
 • Kukosa nidhamu kumewafanya wengine wafukuzwe shule.
 • Kukosa nidhamu kumewafanya wengine wafilisike.
 • Kukosa nidhamu kumewafanya wengine wasiolewe au wasioe.
 • Kukosa nidhamu kumefanya wengine wapewe talaka.
 • Mafanikio ya kila jambo katika maisha hutegemea sana nguzo hii muhimu ya nidhamu.

Kwa mfano ukishakuwa na maono au ndoto ya kufikia hatua Fulani

nidhamu ni kama ulinzi kwako itakusaidia kuzuia kitu chochote kile kinaweza kukutoa katika njia ya kufikia mafanikio yako. Kwa mfano unapohitaji kupata mtaji wa biashara na ukajiwekea kanuni ya kujiwekea akiba ya kiasi fulani cha pesa kila siku, nidhamu ndiyo itakayokusaidia kufikia malengo hayo kwa sababu kuna wakati utatamani utumie hiyo pesa kwa sababu ya shida nyingine uliyonayo, ama kuna kuna wakati utatamani kitu fulani na utahitaji utumie pesa hiyo ili ukipate. Nidhamu peke ndiyo itakayokusaidia kuzuia hayo yote hivyo kutimiza maono yako.

Thamani yako au uwezo ambao Mungu ameweka ndani yako aidha tunu au talanta ulizonazo zinahitaji nidhamu kubwa sana ya kimaisha; ili uweze kuleta matokeo yenye tija kwa maisha yako na kwa jamii inayokuzunguka.

Ni lazima ujue kuwa si kila kitu kinakufaa hata kama kina mwonekano mzuri kwa sura ya nje swali la kujiuliza ni je kinakusaidia kufikia malengo yako?. Vijana wengi wameshindwa kufikia malengo Kwa sababu ya ulevi, uzinzi na kupenda anasa. Wakati mwingine mambo hayo yamewafanya vijana wajiingize kwenye utapeli au biashara haramu ili wapate pesa watakazotumia kwa starehe.

Ni lazima ujifunze kuwa na nidhamu katika maisha bila ya kujali wengine wanakuona vipi maadamu unajua unakokwenda na unachokitaka kwenye maisha kuwa mvumilivu ili uweze kutimiza ndoto zako.

Yusufu alikuwa ni kijana mzuri mwenye kutamanika aliyebeba maono na ndoto za ukuu, ushawishi wa mkewe potifa  ungeweza kuwa na nguvu kubwa sana kama asingekuwa na nidhamu ya kulinda uthamani wa maono yake  ni vema ujue wazi kuwa kuna wakati nidhamu ina gharama kubwa kama jinsi ilivyomsababishia Yusufu afungwe gerezani kwa kusingiziwa kosa ambalo hakulifanya lakini tunaona jinsi ambavyo nidhamu hiyo hiyo ndiyo iliyoleta utimilifu wa maono yake.

Daniel pamoja na wenzake  nidhamu waliyokuwa nayo kwa Mungu wao iliwafanya  wakatae kula chakula cha mfalme  ili kulinda miili yao isitiwe unajisi nidhamu iliwapa msimamo thabiti wa kusimamia kile wanachokiamini na mwisho wa yote walionekana kuwa ni bora mara kumi kuliko wengine wote.

Watu wengi hawafanikiwi kwasababu hawana nidhamu, nidhamu ya matumizi ya pesa, nidhamu ya masomo, nidhamu ya ndoa, nidhamu ya maisha nk.

Mungu humpenda mtu mwenye nidhamu kwasababu nidhamu huleta utii usikivu na unyenyekevu Ayubu alipendwa na Mungu kwa sababu ya nidhamu aliyokuwa nayo maandiko yanatuonyesha jinsi ambavyo Mungu anajivunia ayubu kwa nidhamu aliyokuwa nayo.

Unataka kufanikiwa ni lazima ujifunze kuwa na nidhamu, nidhamu ya kusimamia mipango uliyonayo, nidhamu ya kutunza Muda, nidhamu ya kitabia, nidhamu ya Kumcha Mungu katika roho na kweli, Nidhamu katika mapato na matumizi ya pesa.

Maandiko yamenena wazi kuwa asiyeweza kuizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai nidhamu itakuwezesha kujizuia kwa baadhi ya mambo ambayo hayana tija kwako na kuyasimamia kwa uaminifu mkubwa mambo ambayo yana tija kwako ili yalete matokeo chanya yatakayokuwezesha kufanikiwa katika maisha.

INAENDELEA…………………………

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Emmanuel Mwakyembe kupitia:
Simu/WhatsApp: +255 716 531 353/+255 766 939 969
Facebook Profile: Emmanuel Mwakyembe
Istagram: @emmanuelmwakyembe
Email: emamwakyembe@gmail.com

Like Page yetu ya facebook > GOSPOMEDIA.COM instagram: @gospomedia

More in Uncategorized

To Top