Connect with us

‘Hali ya Maji Tumwachie Mungu’ – Mkuu wa Mkoa Amos Makalla

Mkuu wa Mkoa Amos Makalla

Habari

‘Hali ya Maji Tumwachie Mungu’ – Mkuu wa Mkoa Amos Makalla

Mwezi uliopita, siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza upungufu wa mvua nchini, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ilitangaza kupungua kwa maji katika Mto Ruvu Chini kutoka lita milioni 520 zilizokuwa zinapatikana awali hadi lita milioni 460 kila siku.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  jana alitembelea mto huo na kukiri kwamba hali bado si shwari na kilichopo ni kuomba kudra za Mwenyezi Mungu, kwani mkoa wake unategemea maji kutoka Mto Ruvu Chini uliopo Bagamoyo na Mto Ruvu Juu uliopo Kibaha.

“Yale ya kibinadamu tumeshafanya kwa uwezo wetu, ikiwamo kuwasaka wachepushaji maji, kilichobaki ni kudra za Mungu. Tumekuja hapa kuona hali halisi ili mkoa uwe mabalozi wazuri wa kuwaeleza wananchi nini kinachoendelea, kwani ukiona kitu kwa macho ni rahisi kuwaeleza watu kuliko kuelezewa,” alisema Makalla.

Katika ziara hiyo, Makalla aliongozana na wakuu wa wilaya zote tano za Dar es Salaam, akisema licha ya juhudi zilizochukuliwa, bado hali si nzuri kutokana na kukosekana kwa mvua.

Chanzo kikuu cha maji katika mto huo alisema ni mvua ambazo zilikuwa zinategemewa kunyesha Oktoba na Novemba, lakini hazijaonekana hivyo kutoa funzo kwa wananchi kuwa wanapaswa kutunza vyanzo vya maji na kuyatumia yaliyopo kwa uangalifu.

“Leo tumeona, kuna upungufu wa maji hadi mashine zinatumika kuyavuta, hivyo itabadilika tu pale mvua zitakapoanza kunyesha. Sala ni muhimu, viongozi wetu wa dini waendelee kuomba kwani tulipofika mambo yapo nje ya uwezo wa kibinadamu.

“Tuombe hali ibadilike kuanzia Novemba hii, Desemba mpaka Januari. Viongozi wa Dar es Salaam tunaotumia maji haya tumejionea ukweli twendeni tukawaelimisha watu,” alisema Makalla mbele ya wakuu wa wilaya alioongozana nao pamoja na waandishi wa habari.

Makalla alisema wameamua kutembelea vyanzo hivyo kujionea hali halisi kwa kile alichoeleza “kuona ni kuamini.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema wamefurahi kupata ugeni huo kwani wanaona Serikali ipo na wao katika kipindi hiki kigumu kukidhi mahitaji ya wananchi.

Chanzo: Mwananchi

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

To Top