Familia ni Mahali Pa Kurithisha Imani - Papa Francisko - Gospo Media
Connect with us

Familia ni Mahali Pa Kurithisha Imani – Papa Francisko

Habari

Familia ni Mahali Pa Kurithisha Imani – Papa Francisko

Papa Francisko

Maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, yanafunga rasmi shamra shamra zote za Liturujia ya Kipindi cha Noeli. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko mjini Vatican.

Jumapili tarehe 13 Januari 2019 ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 27, kati yao watoto wa kiume ni 12 na wa kike ni 15 walioandaliwa, ili waweze kuzaliwa upya kwa “Maji, Roho Mtakatifu na katika Neno” tayari kushiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka wazazi, walezi na wasimamzi wa Ubatizo kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani ya Kanisa, kwa kuanzia na ushuhuda wa imani toka ndani ya familia ambako watoto wanaanza kujifunza mambo msingi ya maisha, na baadaye kuendelea na katekesi ya kina utakapofika wakati wake! Lakini, familia ni chemchemi na shule ya imani kwa watoto! Hii ndiyo imani ambayo wazazi na wasimamizi wa Ubatizo wameomba kwa Kanisa, ili kwa njia ya imani watoto hawa waweze kumpokea Roho Mtakatifu anayewakirimia neema ya utakaso wa dhambi na hivyo kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu; tayari kupokea Mapaji ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anawaachia chapa ya kudumu katika nyoyo zao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia inapaswa kuwa ni mahali pa kwanza pa kurithisha imani. Baadaye watoto hawa wataweza kupata nafasi ya kuendelea kujifunza Katekisimu ya Kanisa ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Shuleni na Parokiani wataweza kujifunza mambo haya kwa kina, lakini familia ndiyo chimbuko la imani inayofumbatwa katika ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika maisha ya kifamilia, katika lugha inayofahamika na watoto wenyewe na hatimaye, watoto wanaweza kujifunza pia kutoka katika jamiii inayowazunguka.

Chanzo: Vatican News

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Habari

To Top