Connect with us

Askofu Shoo Awashukia Dk Kimei, Ndakidemi

Askofu Shoo Awashukia Dk Kimei, Ndakidemi

Habari

Askofu Shoo Awashukia Dk Kimei, Ndakidemi

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amepinga hoja za wanasiasa wa Mkoa Kilimanjaro wanaotaka wananchi waruhusiwe kufanya shughuli za kibinadamu katika msitu wa Nusu Maili.

Eneo hilo la ukanda wa Nusu Maili (half mile strip) lenye ukubwa wa kilometa za mraba 51.2 ni tegemeo kubwa la ikolojia ya Mlima Kilimanjaro na ndio sehemu ya vyanzo vya maji ya mito na vijito katika Mkoa Kilimanjaro na nchi jirani ya Kenya.

Mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa (UN) ulisema barafu ya Mlima Kilimanjaro itakuwa imetoweka ifikapo mwaka 2040 endapo kasi ya mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira ya mlima unaoendelea hautadhibitiwa mapema.

Askofu Shoo amewataka wanaotoa hoja hiyo wasifikirie tu kile ambacho wapiga kura wao wanataka leo au kinachowafurahisha, badala yake watangulize masilahi mapana ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Wanaotoa hoja ya kutaka wananchi waruhusiwe kuingia katika msitu huo ambao ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, ni pamoja na Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi.

Mbali na wabunge hao, baadhi ya madiwani wanashikia bango hoja hiyo na Oktoba 25, 2021, Diwani wa Kata ya Katangara Mrere wilayani Rombo, Venance Maleli aliwasilisha hoja katika Baraza la Madiwani kuhusu suala hilo.

Kauli ya Kimei

Katika kikao cha madiwani, Kimei aliwasihi wananchi kutekeleza agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro wakati wao, kama wawakilishi wao bungeni, wakitafuta njia za kuhakikisha agizo hilo linarekebishwa na Serikali.

“Kilichotokea juzi ni kwamba waziri amekuja kibabe akaamua kusema hakuna kutumia kabisa (Msitu wa Nusu Mali). Sheria inasema mtu asiingie hifadhini lakini angetunga kanuni kumsaidia mwananchi si kumkandamiza,” alisema.

Dk Kimei alisema ingawa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Kinapa na RCC kuruhusu wananchi kwenda kuokota kuni yalimalizika, kabla ya tamko lolote waziri alipaswa akutane na wadau kujadili suala hilo.

“Hakuna maeneo. Watu wanafuga mifugo ndani, hawana mahali pa kupata majani wakienda kule (hifadhini) wananyanyaswa tena sasa hivi wanaogopa kabisa kuvuka. Kinapa hawa sio watu,” alisema Dk Kimei.

“Wanapigwa, na sio kupigwa wengine wanauawa. Tulisikia cases (matukio) hapa ndani watu watatu waliuawa hapa nyuma,” alieleza.

“Tatizo sio sheria bali ni implementation (utekelezaji) wake na kanuni zake. Ndio maana waziri anapewa mamlaka ya kutunga kanuni ambazo ni rafiki kwa wananchi. Waziri aangalie namna ya kuondoa kero hii”

Rais Samia awagomea

Oktoba 15, 2021 mbele ya Rais Samia, Profesa Ndakidemi aliwasilisha ombi la kutaka wananchi ndio wapewe wajibu wa kutunza eneo la Nusu Maili, ombi ambalo lilikataliwa papohapo na Rais akisema hilo litaathiri mazingira ya Mlima Kilimanjaro.

“Nataka niwaambie shughuli za wanadamu ni lazima ili tupate maisha lakini na shughuli za kuhifadhi maeneo yetu zina ulazima pia. Eneo lile lina hifadhi nzuri, tunahifadhi Mlima Kilimanjaro,” alisema Rais Samia.

Pamoja na Rais kukataa ombi hilo, bado kumekuwepo na kampeni za baadhi ya wanasiasa kutaka eneo hilo liondolewe Kinapa na wananchi waruhusiwe kuingia kuokota kuni na kukata majani, vitendo vilivyochochea uharibifu wa mazingira.

Alichokisema Askofu Shoo

Akizungumza na wanahabari, Askofu Shoo ambaye ni mmoja wa wakereketwa wa mazingira, alisema eneo la Nusu Maili likitolewa na likaanza kutumika kwa shughuli za kibinadamu madhara yake ni makubwa kwa mabadiliko ya tabia nchi.

“Ninaunga mkono kabisa msimamo wa Rais kwamba kwa ajili ya utunzaji wa mazingira, vyanzo vya maji na kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo, hilo eneo lisitolewe kabisa kwa shughuli za kibindamu,” alisisitiza Askofu.

“Mimi siungani kabisa na wanasiasa wetu, wabunge wetu ambao wanaona bado ni hoja eti kusema wananchi wapatiwe hilo eneo la Nusu Maili. Hiyo ni hatari na itakuwa matokeo mabaya sana kwa mazingira ya Mlima Kilimanjaro.”

“Miti tunayotumia leo imeoteshwa na vizazi vilivyotangulia na sisi tunao wajibu kwa vizazi vijavyo….“Tusifikirie tu leo au kile ambacho wapiga kura wetu wanataka kwa leo na kinachowafurahisha lakini tuangalie madhara yake kesho yatakuwa nini,” alisema.

Kaimu mkuu wa Kinapa, Charles Ngendo alisema mwaka 2014, kikao cha ushauri cha Mkoa wa Kilimanjaro (RCC), kiliazimia wanawake waingie katika msitu huo mara mbili kwa wiki kwa ajili ya kukata majani na kuokota kuni.

Baada ya hatua hiyo wanawake na wanaume waliingia na kukata magogo kwa ajili ya kuni na iwapo Serikali isingezuia, msitu huo ungetoweka ndani ya miaka tisa.

Sheria zilizoanzisha Hifadhi haziruhusu shughuli za kibinadamu na eneo hilo na miaka ya nyuma, msitu huo ulisimamiwa na Idara ya Misitu hadi Septemba 16, 2005 ulipoingizwa Kinapa.

Chanzo: Mwananchi

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

To Top