Habari

Askofu mkuu EAGT Dk. Brown Mwakipesile – Hatutafanya suluhu na wapenda dhambi.

Dodoma;

Askofu Mkuu wa Kanisa la The Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dk Brown Mwakipesile, amesema msingi mkuu wa kanisa hilo ni kusimamia utakatifu, hivyo halitakuwa tayari kufanya suluhu na mtumishi yeyote ndani ya kanisa ambaye atazoelea dhambi na kuifanya kuwa sehemu ya maisha yake.

Akizungumza mbele ya wachungaji na maaskofu wa kanisa hilo wapatao 1800 kutoka makanisa ya EAGT nchi nzima, waliohudhuria Mkutano Mkuu uliofanyika mjini Dodoma, wiki iliyopita, Askofu Dk Mwakipesile alisema: Hatutakumbatia kabisa watenda dhambi. Tuko tayari hata kufa tukitetea utakatifu ndani ya kanisa. Hatutaweka suluhu na wapenda dhambi.

Askofu huyo ametoa ujumbe huo ikiwa ni takribani miaka miwili na miezi miwili tangu alipochaguliwa kwa kura nyingi kuwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo Septemba, 2015 na kusimikwa rasmi Februari, mwaka jana.

Aidha, ujumbe huo ameutoa wakati ndani ya kanisa hilo kukiwa na chokochoko kufuatia makamu wake, John Mahene kuondolewa na kanisa katika nafasi hiyo akidaiwa kuanguka kimaadili ya utumishi wa Mungu kabla ya kurejeshwa na Mahakama Kuu, kwa madai kwamba taratibu za kumwondoa kikatiba hazikufuatwa.

Baada ya Mahakama Kuu kumrejesha, Mahene anadaiwa kuwa amekuwa akiratibu mambo mambo mbalimbali, ikiwemo kushawishi wachungaji kupinga mabadiliko ya Katiba ya kanisa ambayo tayari yameridhiwa. Harakati za Mahene zimekuwa zikitafsiriwa kuwa na lengo la kulipasua kanisa.

Lakini, katika hotuba yake bila kuingia kwa undani kuhusu chokochoko hizo, Askofu Dk Mwakipesile alisema: Kuna EAGT moja tu, kuna askofu mkuu wa EAGT mmoja tu pamoja na wasaidizi wake, na kwa pamoja tutaliongoza kanisa kuhakikisha linasimama katika misingi ya utakatifu.

Askofu huyo ambaye kwa miaka mingi alitumika kama katibu mkuu wa kanisa hilo wakati askofu mkuu akiwa mwinjilisti Dk Moses Kulola, aliyefariki dunia Agosti 2013, aliwataka wachungaji wa kanisa hilo kokote waliko kusimamia msingi mkuu wa kanisa, ambao ni utakatifu.

Alitoa mfano kwamba, ni lazima wachungaji ndani ya kanisa hilo waheshimu maandiko katika Biblia yanayozuia Wakristo kuoa na kuacha. Kwa siku za karibuni, sio tu katika kanisa la EAGT bali katika baadhi ya makanisa ya Kipentekoste kwa ujumla, imeanza kujitokeza tabia ya kutoheshimiwa kwa maandiko ambapo baadhi ya wachungaji wamekuwa wakifungisha ndoa waumini ambao wameishaoa au kuolewa, na wakaacha au kuachana kinyume na taratibu za Kibiblia.

Katika hotuba yake hiyo Askofu Dk Mwakipesile aliwaelekeza wajumbe wa mkutano mkuu huo kuwa, wajibu wao mkubwa katika huduma yao ni kuhubiri injili kwa nguvu, na akasema itapendeza kama kufikia mwakani kila kanisa la EAGT litazaa kanisa.

”Hili ndilo hitaji letu kubwa. Tuhubiri injili kwa nguvu kwa sababu hitaji la injili bado ni kubwa. Tufungue makanisa, na ikiwezekana kufikia mwakani kila kanisa letu la EAGT lizae kanisa. Tuweke bidii tufungue makanisa zaidi huko nje ya nchi”, alisema Dk. Mwakipesile, ambaye hivi karibuni alikuwa nchini Zambia ikiwa ni sehemu ya mipango ya kanisa kuona EAGT inazidi kupanuka zaidi.

Askofu huyo pia alizungumzia nia ya kanisa kushirikiana na serikali katika utoaji wa huduma za kijamii, ambapo alisema tayari EAGT inamiliki shule moja ya sekondari iliyoko Kahama, mkoani Shinyanga, na kwamba mipango ya kanisa hilo ni kuwa na shule zaidi katika maeneo mengine nchini.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Mchungaji Dk Leonard Mwizarubi aliwataka wachungaji na maaskofu wa EAGT kuungana pamoja na askofu mkuu katika kuliweka kanisa mahali sahihi kwa ajili ya kumngoja Bwana Yesu Kristo.

”Mimi kama mtendaji wenu wa EAGT naiona nia ya dhati kabisa iliyomo ndani ya moyo wa askofu mkuu wetu ya kumwangalia Yesu Kristo, kanisa safi, takatifu tayari kunyakuliwa, alisema Mchungaji Dk.Mwizarubi na kuongeza:

Kama ambavyo naiona nia ya dhati ya Rais wetu mpendwa Dk John Pombe Magufuli ya kuipeleka Tanzania katika anga zingine za kiuchumi, nawaomba wachungaji wote na maaskofu wa majimbo na kanda, tushirikiane na askofu wetu katika kusimamia utakatifu kwa nguvu zote huko mlikotoka.

Huu ni wakati wa sisi kama watumishi wa EAGT kuwaaibisha kwa vitendo wote waliokuwa na tamaa ya fisi, waliodhania kuwa EAGT itagawanyika ili waweze kujipatia wachungaji kutoka kwetu.

Dk. Mwizarubi alisema kuwa Kamati Kuu ya kanisa la EAGT inawasihi wachungaji na maaskofu wote kupendana, kusaidiana, kuheshimiana na kuwa tayari kupokea na kuamini taarifa zinazotoka kwenye chanzo sahihi.

Kamati Kuu ya kanisa inawasihi pia kila mmoja aadhimie kutoka ndani yake kuongeza bidii katika wito alioitiwa maana iko siku atasimama mbele za Mungu, alisema katibu mkuu huyo.

Chanzo: Mwanzo News

Like Page yetu ya facebook >> GOSPOMEDIA.COM instagram: @gospomedia

Advertisements
Previous post

Music Video | Music Audio: Emily Nakhungu - Umetenda

Next post

Music Video | Music Audio: Walter Chilambo - Kuna Jambo