Habari

Askofu Mbepera azikwa kanisani kwake EAGT Galilaya

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

Mwili wa Mchungaji Philbert Mbepera wa Kanisa la The Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Galilaya Temple, Msasani jijini Dar es Salaam, ambaye alifariki dunia March 15 ya wiki iliyopita wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, umezikwa jana alasiri katika eneo la kanisa hilo huku wachungaji wa makanisa mbalimbali, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wakishiriki.

Mbepera ambaye alikuwa askofu wa kwanza wa Kanisa la EAGT Jimbo la Dar es Salaam lililokuwa likiundwa wakati huo na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani, pia alikuwa kada wa CCM na aliwahi kushika nafasi ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msasani, na mpaka mauti inamkuta alikuwa mlezi wa UVCCM Msasani Bonde la Mpunga, kwa mujibu wa wasifu wake uliosomwa msibani hapo. Pia aliwahi kuwa askofu wa EAGT Kanda ya Kinondoni.
Wakati Katibu Mkuu wa EAGT Taifa, Mchungaji Dk Leonard Mwizarubi akiongoza mazishi hayo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sita aliwakilisha serikali. Pia alikuwepo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Mchungaji Elingalami Munisi, ambaye alisema anawakilisha CPCT Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Mkuu mstaafu wa CPCT, Askofu David Mwasota, Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la KLPT, Mchungaji Fanuel Shekihiyo,maaskofu wa majimbo na wachungaji mbalimbali wa makanisa ya EAGT pamoja na makanisa mengine.

Mbepera ambaye alizaliwa Februari 5, 1950 katika Kijiji cha Mahenge, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, baada ya kumaliza elimu ya kati (middle school) alijiunga na chuo cha polisi na baada ya kumaliza masomo yake alipangiwa kufanya kazi jijini Dar es Salaam.
Aliokoka mwaka 1977 na baadaye alijiunga na chuo cha Biblia cha Kanisa la EAGT kilichokuwa Temeke, na mwaka 1980 aliamua kuacha kazi ya serikali(jeshi la polisi) na kuingia katika huduma moja kwa moja.

Mwaka 1982 alifungua huduma Msasani akitumia chumba cha darasa katika shule ya msingi Msasani. Iliwalazimu yeye na mkewe Magreth wawe wanatembea kwa miguu umbali wa kilometa 30 kutoka Keko walikokuwa wakiishi wakati huo hadi Msasani walipokuwa wakihudumia.

Alianza kuugua Septemba mwaka jana, ambapo alitibiwa katika hospitali ya Mikocheni, Agha Khan na baadaye hospitali ya Taifa ambako mauti yalimkuta. Taarifa iliyotolewa msibani hapo inasema kuwa, mchungaji Mbepera alikuwa na uvimbe tumboni na alipofanyiwa upasuaji katika hospitali ya Muhimbili hakusema tena, mpaka mauti yalipomkuta.

Marehemu amaeacha mjane mmoja, watoto kumi, wajukuu 16 na kitukuu mmoja.

Kwa niaba ya uongozi wa Gospo Media tunatoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kwa kufikwa na msiba huu, Bwana ametoa Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.

Chanzo: Mwanzo News

Like us on facebook >> GOSPO MEDIA  Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Video | Audio: Ringtone Feat Ada - This Year

Next post

Wanandoa wa kimisionari wafariki kwa ajali ya gari nchini Kongo