Connect with us

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watuminshi wa Uongo – Sehemu Ya Pili

Mafundisho

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watuminshi wa Uongo – Sehemu Ya Pili

Na Dr. Jacob Makaya,

Bwana Yesu asifiwe, Siku chache zilizopita tulianza kujifunza juu ya manabii/watumishi wa uongo wanaodanganya wengi. Ni muhimu kuelewa kwamba Mungu ana manabii wake kwani huduma ya nabii ni muhimu sana.

Neno linasema, “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe” (Waefeso 4:11—12).

Hivyo huduma ya nabii ni muhimu na Mungu ana manabii wake ambao wanaifanya kazi yake. Kwa mfano, kuna nabii mmoja ambaye Mungu alimuonyesha mwaka 2007 kuwa Donald Trump ataenda kuwa raisi wa Marekani. Mwaka huo hata Obama alikuwa hajawa Raisi na huo unabii ulienda kutimia miaka 9 baadae.

Miezi michache kabla ya uchaguzi wa Raisi wa Marekani, kuna nabii wa Mungu alitabiri na kusema “imekwisha kuamuliwa kutoka mbinguni kuwa Donald Trump atakuwa Raisi wa Marekani.”

Huyu pia ndio nabii ambaye siku moja alienda mji wa Houston Texas na alipotua airport Mungu akamuonyesha kuwa ule mji utaenda kukumbwa na mafuriko makubwa. Alisema “Mji huu utaenda kukumbwa na mafuriko makubwa sana ambayo yataleta uharibifu mkubwa sana.”

Mwaka mmoja baadae, mji wa Houston ulikumbwa na dhoruba kubwa na mafuriko makubwa ambayo yaligharimu Marekani zaidi ya dola billion 120 ambayo haijawahi kutokea.

Huyu ni nabii ambaye kila mara anaonya watu juu ya ghadhabu ya Mungu kutokana na uovu na kuhimiza watu watubu na kumrudia Mungu na huwezi kumsikia anatabiri mambo kama kupewa pesa na vitu kama hivyo.

Nilitaka uone kuwa Mungu ana manabii wake kila mahali. Mambo machache juu ya manabii:

1. Katika Agano Jipya, Mungu hatumii sana manabii kama alivyokuwa anafanya katika Agano la Kale.

“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema kwa sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu” (Waebrania 1:1—12).

Mungu hatumii sana manabii kama alivyofanya zamani kutokana na utabiri wa Yoeli:

“Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” (Yoeli 2:28).

Kumbuka kuna utofauti kati ya “nabii” na “upako wa unabii.” Mungu anaweza kuachilia upako wa unabii kwa mtu ye yote akatabiri. Ila hii haimfanyi kuwa “nabii.”

2. Biblia imeonya juu ya ujio wa manabii wa uongo zaidi kuliko huduma zingine. Biblia imesema katika nyakati hizi, watatokea manabii wa uongo, waalimu wa uongo, wachungaji wa uongo, mitume wa uongo, na wainjilisti wa uongo.

Lakini katika huduma hizo tano, maandiko mengi zaidi yameonya juu ya “manabii wa uongo.” Maana yake manabii wa uongo katika nyakati hizi ni wengi zaidi kuliko wa ukweli.

Eliya alipambana na kuwaua manabii wa Baali 450 (1 Wafalme 18:22). Hapa tunaona katika manabii 451, mmoja alikuwa wa Mungu na 450 walikuwa wa uongo.

Ahabu aliita manabii wake 400 na baadaye nabii wa Mungu Mikaya naye akaenda kutoa unabii. Hapa tunaona kuwa katika manabii 401, mmoja alikuwa wa Mungu na 400 walikuwa wa uongo (1 Wafalme 22:6—22).

Maandiko haya yanatuonyesha kuwa kwa kila nabii mmoja wa Mungu, Shetani ana mamia ya manabii wa uongo. Sasa unaweza kuelewa kwa nini katika nyakati hizi, karibia kila mtaa kuna manabii.

WACHUNGAJI WA UONGO:

Biblia pia imeonya sana juu ya wachungaji wa uongo. Kuna wachungaji wa aina kubwa tatu:

1. Wachungaji wa kweli: Yesu alisema, “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo” (Yohana 10:11). Kipimo kikubwa cha “wachungaji wa kweli” ni utayari wao wa kutoa maisha yao kwa ajili ya kondoo.

Kumbuka Yesu aliketi katika kiti cha enzi cha Daudi na Daudi ni mfano wa “mchungaji mwema.” Neno linasema:

“Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo wa baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana—kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua” (1 Samueli 17:34—35).

Kutoa uhai kwa ajili ya kondoo ni sifa ya “mchungaji mwema.” Pia tunaona Musa alikuwa na sifa hii kwani alikuwa tayari kufa kwa ajili ya wana wa Israeli.

Baada ya wana wa Israeli kutenda dhambi na Mungu akaghadhibika, Musa alienda kuwaombea kwa Bwana na akasema, “Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao—na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika” (Kutoka 32:32).

Musa yuko tayari kupoteza uhai wake kwa kuwaombea Mungu awasamehe wana wa Israeli.

Mchungaji mwema wakati wote yuko tayari hata kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Hii haina maana mchungaji mwema anatakiwa afe, ila kama hayuko tayari kufa kwa ajili ya kulinda kondoo, huyo si mchungaji mwema.

2. Mchungaji wa mshahara: “Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa—mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa—mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake” (Yohana 10:12—13).

Kundi lingine la wachungaji ni wale wa mshahara. Hawa ni wale ambao “uchungaji” ni “taaluma” kama taaluma zingine na siyo “wito.” Wachungaji wa kundi hili hawajali maisha ya kiroho ya kondoo wao.

Hawa ni wachungaji ambao umeokoka au hujaokoka, kwake siyo kitu. Hawezi kuwa anakemea dhambi; hawezi kuwa anafunga na kuomba ili watu waokoke, ila atafunga na kuomba ili mapato ya kanisa yaongezeke.

Kwa sababu hii, “makanisa” yao wamejazwa na watu wasio amini. Badala ya kuwalisha kweli ya Mungu na kukemea dhambi ili watu wamrudie Mungu, watawalea watu kutokana na mapokeo ya dini zao.

Hivyo mtu anakua katika dini yake, na siyo kukua katika kumjua Mungu na Kristo. Wachungaji wa kundi hili wao hunia zaidi ya dunia na pia “mungu wao ni tumbo” (Wafilipi 3:19).

3. Mchungaji aliyevaa mavazi ya kondoo ila ni mbwa—mwitu. Yesu alisema, “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu” (Mathayo 7:15).

Watu ambao wanavaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu siyo manabii tu bali hata watumishi wengine kama waalimu, wachungaji, mitume, na wainjilisti.

Yesu alionya kuwa “Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi” (Mathayo 24:5).

Hawa ni wachungaji ambao ni mbwa—mwitu na kusudi lao ni kuwadanganya wengi. Badala ya mchungaji kuokoa kondoo kutoka kwa mbwa—mwitu, hawa wanachukua kondoo na kuwalisha mbwa—mwitu.

Unapoona mchungaji wa kanisa anakuwa anatembea na mwimbaji wa kwaya, huyu ni mbwa—mwitu aliyevaa mavazi ya kondoo.

Asilimia kubwa ya wachungaji wa leo ni wa “mshahara” au ni “mbwa—mwitu waliovaa mavazi ya kondoo.”

Mchungaji mwema ni yule ambaye anajali sana maisha yako ya kiroho na yuko tayari hata kupoteza uhai wake kwa ajili ya kulinda kondoo.

SWALI: Je mchungaji wako yuko tayari kufa kwa ajili yako au yuko tayari kukuua wewe kwa ajili yake??

WAALIMU/WATUMISHI WA UONGO:

“Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana Yesu aliyewanunua, wakiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao; kwa hao njia ya kweli itatukanwa” (2 Peter 2:1—2).

Waalimu wa uongo ni wale ambao wanatumia Biblia kama njia ya kujipatia faida na siyo kulifundisha neno la Mungu ili watu wakue kiroho na kuutafuta ufalme wa Mungu kwanza.

Neno linasema, “Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa” (2 Peter 2:3). Kuna njia ambazo Biblia imeziweka ili kuwatambua watumishi wa uongo.

1. Watanena ya duniani, na siyo ya ufalme wa Mungu. Neno linasema, “Hao ni wa dunia; kwa maana wanena ya dunia na dunia huwasikia” (1 Yohana 4:5). Watumishi wa uongo wakati wote watakuambia “unayotaka kusikia” badala ya “unayohitaji kusikia.”

Kitu cha msingi kulivyo vyote ni watu kusikia habari za ufalme wa Mungu ili watubu na kuacha dhambi na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Neno linasema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33).

Watumishi wa uongo wakati mwingi watafundisha/kuhubiri mambo ya mwilini kuliko mambo ya rohoni. Yesu alisema, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Mathayo 5:3).

Hivyo angalia mtumishi anaupeleka moyo wako wapi. Kwenye mambo ya dunia au ya mbinguni? Neno linasema, “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, amaketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikiri yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi” (Wakolosai 3:1—2).

Watumishi wa uongo wakati wote watatumia neno la Mungu kujaribu kukufundisha jinsi ya kupata nafasi katika ulimwengu huu wakati Yesu anasema, “Ninyi si wa ulimwengu huu” (Yohana 17:16).

2. Injili/mafundisho ya pesa: Injili na mafundisho yanayolenga utajiri, hayo ni mafundisho ya kipepo.

Biblia inasema, Yesu alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri (2 Wakorintho 8:9). Haya ni maandiko ambao wanaohubiri injili ya utajiri wanapenda sana kuyatumia ila ukitaka kuelewa kitu alichokuwa anaandika Paulo, soma kuanzia mstari wa kwanza.

Mahali pengine neno linasema, “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3 Yohana 3:2). Haya maandiko yanapozungumzia “kufanikiwa” yanazungumzia nini?

Ukitaka kuelewa zaidi soma mistari inayofuata. “Maana nalifurahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli. Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli” (3 Yohana 3:3—4).

Yesu alipokuwa anawaombea wanafunzi wake, alisema, “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yohana 17:17). Kumbuka utajiri unategemea na hazina uliyo nayo na neno liko wazi:

“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi” (Mathayo 6:19—20).

Hivyo hakikisha unapima mafundisho na kuangalia unafundishwa kuweka hazina yako wapi. Kama unafundishwa kuweka hazina duniani, moyo wako utakuwa kwenye mambo ya dunia; “kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mathayo 6:21).

Maandiko haya hayasemi kwamba ni vibaya kuweka akiba ya pesa bank ila kama moyo wako utakuwa hapo na mategemo yako, huwezi kuingia katika ufalme wa Mungu.

Manabii na watumishi ambao msisitizo wao ni kwenye utajiri, hao ni watumishi wa Shetani kwani huwezi kuweka moyo wako kwa Mungu na katika pesa (Mathayo 6:24).

Hujawahi kusikia mafundisho kama haya: “Naona mkono wa Mungu ukiweka pesa nyingi sana kwenye akaunti yako. Kama unaamini sema NAPOKEA KWA JINA LA YESU.” Au “Kama unaamini andika AMEN.” Ila hutasikia wakikuambia kuacha dhambi au kuutafuta ufalme wa Mungu.

Mtu mmoja alituma ujumbe na kusema alikuwa anaenda kwenye kanisa moja ambalo watu wanaambiwa wapeleke pesa zao zote kama “sadaka ya kujimaliza.” Halafu baada ya hapo, watapokea ujumbe na kuwekewa pesa kwenye account zao mara mbili zaidi ya walizoweka.

Mwingine alienda mahali fulani ambako kila ombi moja unalolitaka, unaandika kwenye fomu na unalipia elfu kumi. Kwa hiyo kama una maombi mawili, unatoa elfu ishirini.

Kama huwezi kuona uongo mdogo kama huu, je utaweza kumtambua mpinga Kristo ambaye Biblia imesema wengi watamstaajabia na kumfuata kutokana na ishara kubwa atakazozifanya (Ufunuo 13).

Kama huwezi kutambua uongo mdogo kama huu, je utaweza kutofautisha kati ya miujiza ya mashahidi wawili wa Mungu na ile ya mpinga Kristo katika Ufunuo 11?

KUMBUKA: Kusudi la Yesu kumwaga damu ni ili mimi na wewe tununuliwe na kuoshwa dhambi zetu. Ni kutukomboa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Kristo ili tuwe makuhani na ufalme (Wakolosai 1:13—14; Ufunuo 5:9—10).

Kusudi la damu ya Yesu siyo mimi na wewe tuwe matajiri na kuwa na pesa nyingi. Katika Agano la Kale watu walikuwa matajiri na walikuwa na pesa nyingi na hawakuwa na damu ya Yesu.

Na katika uchumi wa ulimwengu huu, watu ambao wana Kristo na wameoshwa kwa damu ya Yesu uchumi wao ni mbaya zaidi kuliko wale ambao hata hawaombi wala kutumia damu ya Yesu.

Hii haina maana Mkristo hatakiwi kufanikiwa. Hasha! Mategemeo yetu na mafanikio yetu yapo katika Mungu. Ndio maana Yesu alisema, tukiutafuta ufalme wa Mungu, mahitaji yetu yote Mungu atatupatia (Mathayo 6:33).

Shida ni kwamba watu hawajui hata ufalme wa Mungu ni nini. Kwa sababu hiyo, hata jinsi ya “kuutafuta ufalme hawajui.” Hivyo yale ambayo Mungu alisema wataongezewa, hawaongezewi.

Sasa unaweza kuelewa neno linalosema, “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6). Shida ni kwamba watu wa ulimwengu wana maarifa ya ulimwengu kuliko watu wa Kristo walivyo na maarifa ya ufalme wa Mungu.

Yesu alisema, “Wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru” (Luka 16:8b).

Tunachotakiwa ni kuwa na maarifa ya neno la Mungu, kuelewa jinsi ufalme wa Mungu unavyofanya kazi na hapo ndipo Mungu anaweza kutufanikisha sawasawa na mapenzi yake.

Injili ya pesa haikuhubiriwa na Yesu wala mitume. Paulo aliandika, “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyohubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangua kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe” (Wagalatia 1:8—9).

Injili ya pesa ni injili ya Lucifa na chimbuko lake ni kuzimu, siyo mbinguni. Injili ya pesa itapeleka moyo wako kwenye pesa na moja ya kundi la watu walioshindwa kuingia katika ufalme wa Mungu walikwamishwa na pesa.

Tuangalie mifano michache:

1. Tajiri aliyekufa na kwenda kuzimu (Luka 16:19—23).

2. Tajiri aliyekuwa na mali nyingi ambaye Yesu alimwambia auze na kuwagawia maskini. “Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida kwa Tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 19:23).

3. Yuda Iskariote. Kilichomfanya Yuda amsaliti Yesu ni pesa.

4. Anania na Safira walimdanganya Roho Mtakatifu na kufa kwa sababu ya pesa (Matendo 5:1—10).

5. Solomon ambaye alikuwa tajiri mkubwa katika Biblia alimaliza vibaya na kumwacha Mungu.

6. Mafarisayo ambao walikuwa wanazuia watu wasiingie katika ufalme wa Mungu (Mathayo 23:13) walikuwa wapenda pesa (Luka 16:14—15).

7. Tajiri ambaye shamba lake lilizaa sana na akafarijika kwa mali zake nyingi lakini Mungu akamwambia “usiku wa leo wanataka roho yako” (Luka 12:16—21).

Siyo kwamba kuwa na pesa au kuwa tajiri ni vibaya ila kila mtu aliyetegemea pesa kwenye Biblia, alishindwa kuingia katika ufalme wa Mungu.

Hivyo ukiona unafundishwa/kuhubiriwa sana juu ya pesa na siyo kubadilisha maisha yako na kumrudia Mungu, ujue huyo ni Shetani.

Baadae tutaangalia jinsi ya kutofautisha “miujiza ya Mungu” na “miujiza ya Shetani inayofanywa kwa jina la Yesu ili kudanganya watu.” Mungu ana watumishi ambao anawatumia kufanya miujiza mikubwa ili kulithibitisha neno lake.

Lakini utaona kuwa asilimia kubwa ya miujiza, haitokani na Mungu bali ni Shetani anaitumia kudanganya watu. Je unatofautishaje? Tutaangalia kile Biblia inachosema kwani Biblia ndiyo kipimo chetu.

Somo litaendelea… Mungu akubariki,

Jacob & Devota Makaya
Kingdom of Heaven Ministry.

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top