Connect with us

Baada ya kuokoka, je ni sahihi kibiblia kushughulika na laana au urithi wa mababu?

Mafundisho

Baada ya kuokoka, je ni sahihi kibiblia kushughulika na laana au urithi wa mababu?

Bwana Yesu asifiwe,

Watu wengi baada ya kuokoka na kumpa Yesu maisha yao, moja ya maombi ambayo wamekuwa wakiyaomba ni maombi ya kujiondoa kutoka kwenye urithi wa mababu au laana zingine za mababu.

Kuna mafundisho mengi na vitabu vingi juu ya jambo hili. Hata mimi binafsi kuna wakati niliamini kuwa mtu ukishaokoka, unatakiwa ushughulike na laana na matatizo mengine ya kurithi ambao waliokutangulia walifanya.

Naamini kuna wengi ambao wamekuwa na imani hii. Tuangalie maandiko yanazungumza nini juu ya hili:

Mungu alisema, “Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu” (Kutoka 20:5b—6). Maandiko haya utaona pia yakijirudia katika Kumbukumbu 5:9—10.

Watu wengi baada ya kuokoka, wamekuwa wakitumia maandiko haya na kuanza kushughulika na mambo ya kurithi au laana za mababu. Ukisoma Biblia, kweli kuna maeneo kadhaa ambapo Mungu aliadhibu mtoto kwa kosa la baba. Tuangalie mfano mmoja katika maandiko haya:

“Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA. BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika uzao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda” (Yeremia 22:29—30).
Huu ni mfano ambao uzao wa mtu (watoto) uliandikiwa kutofanikiwa kwa kosa la baba. Kuna mifano mingine kwenye Biblia.

Ukiendelea kusoma maandiko, neno linasema, “Siku zile, hawatasema tena, Baba wa watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto yametiwa ganzi” (Yeremia 31:29). Hapa tunaona Mungu akisema kuwa siku zinakuja ambapo hataadhibu watoto kwa kosa la mababa/mababu tena.

Wakati wa Yeremia, Mungu alikuwa anaweza kuadhibu mtoto kwa makosa ya wazazi kwani neno linasema, “wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao” (Yeremia 32:18a).

Pia kuna maneno yanayosema, “Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao” (Maombolezo 5:7). Mpaka sasa, Mungu bado alikuwa anaadhibu mtoto kwa makosa ya wazazi.

Lakini wakati wa nabii Ezekieli, Mungu alilitimiza neno alilonena kupitia Yeremia katika Yeremia 31:29.

“Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli” (Ezekieli 18:2—3).

Ukiendelea kusoma Ezekieli 18 utaona Mungu akisema kuwa yule anayetenda kosa ndiye anayeadhibiwa. Mungu alisema haadhibu mtoto kwa kosa la mzazi au mzazi kwa kosa la mtoto. Ndio maana baada ya maandiko haya, hakuna mahali ambapo Mungu ameadhibu mtoto kwa kosa la baba.

Turudi kwenye Kutoka 20:5 katika kipengele kinachosema, “nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.”

Ni muhimu kuelewa kuwa maandiko haya ya kupatiliza uovu hata kizazi cha tatu na cha nne ni kwa wale “wanaomchukia Mungu.” Kwa wanaompenda Mungu, anawaherehemu maelfu elfu.

Kwa hiyo, wewe ambaye umejitoa maisha yako kwa Yesu na kusafishwa kwa damu yake, Mungu hawezi kupatiliza uovu wa mababu au laana zao. Unapookoka na kumpa Yesu maisha yako, Mungu anakusamehe 100%.

Neno linasema, “Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi” (Zaburi 103:12). Kwa hiyo, ukiokoka na kuwa kiumbe kipya sawasawa na 2 Wakorintho 5:17, Mungu anasamehe kabisa.

SWALI: Kwa nini watu waliokoka wanakwamishwa na mambo ya urithi au laana za mababu?

Wengi wanapookoka “hawaamini” kuwa msalaba umewakomboa 100% kutokana na mafundisho wanayopata au wanayoamini na wanadhani kuwa wanahitaji kwenda kushughulika na hizi laana.

Kwa sababu ya kutokuamini kwao, wanakuwa wamefungua mlango kwa Shetani kuwafunga katika maisha kwani hawaijui kweli ya Mungu ya kwamba “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani msamaha wa dhambi” (Wakolosai 1:13—14).

Lakini unapookoka, ukiamini na kufahamu ndani ya moyo wako kuwa umekombolewa kutoka katika nguvu zote za giza, Shetani anakuwa hana uhalali wa kukufunga kwani neno linasema, “tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32).

Kweli unayoifahamu ndiyo inayokuweka huru. Hivyo ukiamini kwamba msalaba ulimaliza kila kitu na wewe unaishi ndani ya Kristo, hiyo kweli itakuweka huru. Mfano, neno linasema, “tumeketi pamoja na Kristo katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 2:6)

Kama unaamini umeketi pamoja na Kristo na unaamini Kristo ameketi “juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwengu humu tu, bali katika ule ujao pia” (Waefeso 1:21), hii kweli unayoifahamu ndiyo itakuweka huru.

Pia neno linasema, “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutotahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo” (Wakolosai 2:13—15).

Kumbuka Shetani anafanya kazi kwa kutumia sheria ya “dhambi na mauti.” Ndio maana Shetani kazi yake ni “kuua, kuharibu na kuchinja” (Yohana 10:10).

Lakini ili Shetani aweze kuharibu, lazima apate uhalali kisheria. Kwa lugha nyingine, lazima mlango ufunguliwe ili Shetani aweze kuwafunga watu. Moja ya malango ni “ukosefu/udhaifu wa imani” au kuwa na “imani ambayo haitokani na Mungu.”

Kwa mfano, tumeona Mungu akisema kupitia nabii Ezekieli kuwa hatoadhibu mtoto wa kosa la mzazi wala mzazi kwa kosa la mtoto. Ndio maana ukisoma Biblia baada ya neno hilo Mungu alilosema kupitia Ezekieli, huoni mahali popote Mungu akiadhibu mtoto kwa kosa la baba au mababu.

Watu wengi wamekuwa wakisumbuliwa na mambo ya urithi kwa sababu ya kutokuamini kuwa msalaba ulishughulika na kila kitu. Kwa kuwa na imani hii, Shetani anakuwa amepata uhalali wa kupandikiza roho za urithi.

Lakini ukiokoka na ukaamini 100% ndani ya moyo wako kwamba “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli” (Yohana 8:36), maana yake Mungu anakusamehe kila kitu.

Ila kitachofanya wewe uwekwe huru ni hii kweli ya Mungu ambayo unaifahamu. Kweli usiyoifahamu, haiwezi kukuweka huru.

SWALI: Mbona tumekuwa tukifundishwa/kuhubiriwa kuwa baada ya kuokoka tunahitaji kushughulika na laana au matatizo ya mababu?

JIBU: Hata mimi binafsi nilikuwa nimefundishwa hivyo lakini baadae ndipo nikafahamu hayo ni mafundisho ya uongo kwani yanalipinga neno la Mungu alilosema kupitia nabii Ezekieli.

Shetani ndiye amekuwa akipitisha mafundisho yasiyo enda sambamba na neno la Mungu kuwa hata ukiokoka, kuna laana za mababu unahitaji kushughulika nazo. Na unapoamini hivyo, unakuwa umemfungulia mlango.

Mafundisho/mahubiri kama hayo Biblia inayaita “mafundisho ya mashetani.” Neno linasema, “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani” (1 Timotheo 4:1).

Biblia inaposema “mafundisho ya mashetani,” haina maana shetani ndiye atakayekuja kuyafundisha bali mapepo ndiyo yanafunua maandiko halafu mtu anaelewa tofauti na kile neno linasema.

Mafundisho kama haya kwa kiingereza yanaitwa “false doctrine” au “demonic doctrine.” Haya ni mafundisho ambayo Roho Mtakatifu hajayafunua bali akili ya mtu mwenyewe au roho ya mashetani.

Ukisoma Mathayo 16 unaona Petro akifunuliwa na Mungu kuwa Yesu ndiye Kristo na Mwana wa Mungu (Mathayo 16:16—17). Ukiendelea kusoma, baada ya Yesu kuwaambia wanafunzi wake kuwa atakwenda kupata mateso, unaona Petro akipewa neno na Shetani na kumwambia “Hasha, Bwana, hayo hayatakupata” (Mathayo 16:22).

Yesu “Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu” (Mathayo 16:23). Huu ni mfano ambao Roho Mtakatifu amefunua kitu kwa mtu na Shetani pia akafunua kitu kingine.

Kwa hiyo, ile kwamba mtu ni mtumishi wa Mungu, haina maana kila anachofundisha/kuhubiri kinatoka kwa Mungu. Shetani naye anaweza kuachilia mafundisho yanayolenga kuwatenga watu na imani ili apate mlango wa kuua mambo yao.

Moja ya malango ambayo Shetani amekuwa akiyatumia ni kuwafanya watu waamini kuwa msalaba haukushughulika na matatizo yao yote hivyo inabidi waende kushughulika na jambo moja moja kama urithi au laana ya babu.

Ndio maana haijalishi mtumishi ana upako wa namna gani, angalia kwenye maandiko kama kile unachofundishwa kinatokana na Mungu. Sisi sote ni wanadamu na inawezekana kabisa mtumishi kusema “Mungu ameniambia hiki na hiki” kumbe aliyesema ni Shetani.

Ndio maana ukifatilia mafundisho/mahubiri pamoja na vitabu ambavyo vinazungumzia mambo ya laana, wakati wote masomo haya yatafundishwa kwa kutumia zaidi maandiko ya Agano la Kale kabla ya kipindi cha Ezekieli.

Lakini pia ni muhimu kuelewa kuwa Mungu aliposema anapatiliza uovu hata kizazi cha tatu na cha nne alikuwa anazungumzia juu ya WANAOMCHUKIA MUNGU. Hivyo wewe uliyeokoka unamchukia Mungu? Jibu ni HAPANA!

Watu wengi wamekuwa wakiota ndoto ambazo zinaonyesha wapo kwenye “agano la urithi” pamoja na kwamba wameokoka. Hii ni kwa sababu ya kutokuamini kazi ya msalaba kwa 100% na kufungua mlango wa Shetani kuwashambulia.

KUMBUKA: Shetani alishindwa kwa damu ya Yesu (Ufunuo 12:11a). Hivyo kazi kubwa ambayo Shetani anayo ni kukushawishi ili uamini kuwa msalaba haukumaliza kila kitu. Ukiamini uongo huu unakuwa umefungua mlango kwa Shetani.

UKWELI: Ndio maana watu wengi ambao wamekuwa wakishughulika na mambo ya urithi na laana za mababu, wataomba sana lakini matatizo yanakuwa pale pale. Likimalizika moja, linakuja lingine.

Ndio maana ni hatari kuchukua mstari mmoja kwenye Biblia na kufundishia au kuhubiria huo bila kuangalia kile neno la Mungu linachosema kwa upana.

Kwa hiyo, pamoja na kumpenda Mungu na kulishika neno lake, ukiamini bado unahitaji kushughulika na laana na urithi wa mababu, unarudi katika nyakati kabla ya nabii Ezekieli.

Maana yake, unakuwa unaendelea kutumia ile methali inayosema “Baba wa watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto yametiwa ganzi” pamoja na kwamba Mungu amesema hutatumia hii methali tena kwani Mungu hatamwadhibu mtoto kwa makosa ya baba.

Tuzidi kusoma neno la Mungu sana ili tuijue kweli ya Mungu. Hivyo, ile kwamba mtumishi amesema kitu, ingia kwenye maandiko uhakikishe kwani inawezekana kabisa mtumishi wa Mungu kukosea na kufundisha false doctrine pasipo kujua.

Mungu akubariki,

Jacob & Devota Makaya
Kingdom of Heaven Ministry

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top