Habari

Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za TAGOANE na vyama vya wasanii – Juliana Shonza

Na Mwandishi wetu, Arusha

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za vyama vya wasanii vinavyojikita katika shughuli mbalimbali zinazoleta maendeleo kwa Taifa.

Shonza amesema hayo baada ya kushuhudia kazi zinazofanywa na Mtandao wa Tasnia ya Wasanii wa Muziki wa Injili Tanzania (TAGOANE) ikiwamo ya kuhamasisha jamii kuchangia damu salama ili kuokoa uhai wa mama na mtoto kupitia tamasha la Mama ni wa Thamani ( TAMANI FESTIVAL).

Akizungumza katika tamasha hilo jijini Arusha, Shonza alisema kazi ya sanaa sio tu kutoa burudani peke yake bali kuisadia jamii kuondokana na changamoto mbali mbali zinazowakabili.

” Tagoane ni kati ya taasisi makini za wasanii iliyoonyesha njia kwamba kumbe inawezekana kutumia burudani kuhamasisha jamii kuondokana na changamoto, ni wakati wa taasisi nyingine kuiga mfano huu,” alisema.

Shonza alisema Serikali ipo tayari kufanya kazi na kuunga mkono vikundi vya wasanii vinavyoweza kutumia sanaa yake kuleta matokeo chanya kwa taifa.

Alisema tamasha la MAMA NIWATHAMANI linamuongezea heshima mwanamke wa kitanzania kwa kuwa ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke anao mchango mkubwa katika jamii yake.

Awali Rais wa Tagoane, Dk Godwin Maimu alisema wasanii wa injili waliamua kuandaa tamasha hilo ili kuenzi mchango wa wanawake wa kitanzania katika kupigania maendeleo ya taifa lao.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akimsikiliza kwa makini mmoja wa mama aliyekuwa anazungumza siku ya tukio hilo.

“Sekta ya afya inatuambia upungufu wa damu ni kati ya sababu kubwa za vifo vya wanawake wakati wa kujifungua, sasa katika kuitambua thamani ya mwanamke tumefungua kampeni ya kuchangia damu salama kuokoa uhai wa mama na mtoto,” alisema.

Alisema kampeni hiyo itafanyika pia katika mikoa ya Manyara, Mbeya, Dar es Salaam na Dodoma na lengo kubwa ni kuihamasisha jamii kuvhangia damu salama.

Mbali na shughuli nyingine, TAGOANE walifanya usafi na kutoa msaada wa mashuka zaidi ya 400 kwa hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha.

Baadhi ya wanamuziki wa muziki huo wa Injili walisema jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanahubiri neno la Mungu kwa njia ya uimbaji pamoja na kufanyia kazi kwa vitendo yale wanayoyaimba.

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Sioni Kama Ni dhambi, Yesu Mwenyewe Aliwachapa Watu Hekaluni - Imma kuleba

Next post

Magreth Sommy Kuweka Wakfu wa Yesu ni Bwana, Oktoba 28