Connect with us

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu Ya Tatu

Mafundisho

Jinsi ya Kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu Ya Tatu

Bwana Yesu asifiwe,

Leo tutaingia ndani kidogo juu namna ya kuwatambua watumishi wa uongo ambao Yesu na mitume walionya. Yesu alisema wazi, “Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watawadanganya wengi” (Mathayo 24:5).

Tafsiri ya Kristo ni “mpakwa mafuta.” Katika maandiko haya, Yesu hasemi kwamba “wengi watakuja kwa jina langu wakisema mimi ni Yesu.” Kitu Yesu anaonya ni kwamba wengi watakuja kwa jina la Yesu wakisema wao ni wapakwa mafuta; nao watawadanganya wengi.

Yesu anazungumzia juu ya watu kuja na upako wa uongo (false anointing) kwa kutumia jina la Yesu. Je utamtambuaje mtumishi anayekuja na maandiko na anatumia jina la Yesu lakini kwa kusudi la “kudanganya wengi?”

Kwanza kabisa kutokana na maneno ya Yesu, watumishi hawa “watadanganya wengi.” Ndio maana Yesu alisema “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia wasiweze” (Luka 13:23).

Leo tutaangalia mambo kadhaa ambayo yatatusaidia kuwatambua watumishi wa uongo:

MIUJIZA YA KUTOKA KWA MUNGU AU KWA SHETANI:

Changamoto kubwa kwa watu wengi ni kujua namna ya kutofautisha miujiza ya kutoka kwa Mungu na miujiza ya kutoka kwa Shetani.

Yesu alisema “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule” (Mathayo 24:24). Mkristo wa uongo tafsiri yake ni “wapakwa mafuta wa uongo.”

Kumbuka kwamba watumishi wa uongo ambao wanafanya ishara na maajabu wanatumia upako wa Shetani. Hivyo kuna mambo ukiyajua ambayo Shetani anayafanya, utajua kuwa miujiza hiyo ni ya Shetani.

Neno linasema, “BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, akaibwaga chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka” (Kutoka 7:8—9).

Kumbuka Farao alikuwa anamwabudu Shetani na hapa tunaona kuwa Farao ndio “atakayetafuta miujiza” kutoka kwa Musa. Kwa hiyo roho inayofanya watu “watafute miujiza” haitokani na Mungu.

“Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona” (Mathayo 12:38—39).

Mahali pengine tunasoma, “Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni” (Mathayo 16:1).

Yesu hakuwapa ishara bali mwisho aliwaambia, “Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya nabii Yona; akawaacha, akaenda zake” (Mathayo 16:4).

Kwa hiyo, ukishaona watu wanatafuta ishara, badala ya kutafuta neno, unajua wazi kuwa hilo halitokani na Mungu, bali Shetani. Kumbuka kwa kila kitu, nyuma yake kuna roho. Roho Mtakatifu wakati wote atakuongoza kwenye kweli ya Mungu (Yohana 16:13).

Roho za Shetani zinaongoza watu wenye uongo na Shetani anatumia zaidi vitu kudanganya watu kwani anajua watu wana mahitaji. Ndio maana ukiwa unapitia changamoto katika maisha, lazima uwe mwangalifu wapi unaenda kupata msaada kwani kuna mahali unaweza kwenda, na Maisha yako ya kiroho yakafa.

Ukiendelea kusoma ile habari ya Musa utaona kuwa fimbo ya Musa iligeuka nyoka na wachawi wakafanya fimbo zao kuwa nyoka. Kuna ishara ambazo Musa alikuwa anafanya na wachawi wanafanya vile vile. Wachawi wa Farao walifanya ishara zingine lakini mwisho walishindwa.

Kibaya ni pale ambapo mtu anatumia uchawi halafu watu wanadhani anatumia nguvu za Mungu.

“Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule mkuu” (Matendo 8:9—10).

Nataka uone watu walidhani Simoni anatumia nguvu za Mungu. Hii inatuambia kuwa Simoni hakuwaambia kuwa anatumia uchawi. Kwa hiyo usitegemee makristo wa uongo kukwambia wanatumia uchawi. Ndio maana “mtawatambua kwa matunda yao” (Mathayo 7:16).

Neno linasema shetani ni “mungu wa dunia hii” (2 Wakorintho 4:4). Hivyo mtu anapokuwa anafanya ishara na kumtaja “Mungu” utajuaje kama anamaanisha “Mungu katika Kristo” au “mungu wa dunia hii?” Angalia matunda yake.

Inawezekana kabisa mtumishi kutumia jina la Yesu lakini asiwe anamzungumzia Yesu mwana wa Mungu. Maandiko yanatuambia juu ya mchawi na nabii wa uongo aliyeitwa Bar-Yesu (Matendo 13:8).

Katika jina la huyu mchawi na nabii wa uongo, unaona imetangulia “Bar” ndipo “Yesu.” Mungu anatufunulia kwamba kinatofautisha ni Yesu yupi, na kile kinachotangulia. Kama ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, lazima kila kitu kifanywe sawasawa na neno lake. Tofauti na hapo, siyo Yesu wa kweli.

Nataka uone kabisa kwamba mtu anaweza kutumia jina la Yesu lakini kumbe katika ulimwengu wa roho, anatumia uchawi.

Yule kahaba mkuu na mama wa makahaba (kanisa la uongo lililozaa makanisa mengine ambalo pia ni ule mji mkuu) (Ufunuo 17:5; 18) maandiko yanasema, wanatumia uchawi (Ufunuo 18:23).

Lakini ukienda kwenye hili kanisa, wanataja jina la Yesu. Ndio maana inatakiwa ujue namna ya kutambua makanisa ya uongo na kanisa la Kristo. Mungu akiona uko kwenye kanisa la uongo, Roho Mtakatifu lazima atakuambia “toka huko usipate mapigo yake” (Ufunuo 18:4).

Kumbuka katika nyakati hizi, kila kinachofanywa kinawaandaa watu kumpokea Yesu au mpinga Kristo. Manabii wote wa uongo Shetani anawatumia ili kuandaa watu kumpokea mpinga Kristo aliyetajwa katika Ufunuo 13:1—2.

Shetani anachofanya ni kufanya watu wampokee kwanza ndani ya mioyo yao kwa kuwafanya watafute tofauti na Mungu anachotaka watafute. Ndio maana wakati wote Shetani anatanguliza miujiza mbele ya vyote.

MIKUTANO YA MIUJIZA

Ukisoma Biblia, hamna mahali Yesu alikuwa anakusanya watu kwa ajili ya miujiza. Miujiza ilifuata BAADA ya neno. Yesu alichokuwa anatangaza ni neno, siyo miujiza. Ndio maana Yesu alipoenda kwao nao hawakumwamini, neno linasema, “Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao” (Mathayo 13:58).

Kipaumbele cha Yesu ni sisi tupate neno lake la ufalme kwanza. “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe” (Yohana 7:37).

Huwezi kusikia Yesu anapaza sauti na kutangaza “njoo upokee muujiza wako.” Wakati wote neno linatangulia halafu miujiza na ishara vinafuata kulithibitisha neno. Shetani yeye anatanguliza miujiza kwani anajua kizazi kibaya na cha zinaa kinatafuta miujiza.

Hii ni kwa sababu watu wanapomfuata Yesu kwa sababu tu ya miujiza na siyo neno, hawawezi kudumu. Biblia inasema, “Na mkutano wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara aliwafanyia wagonjwa” (Yohana 6:2).

Ukiendelea kusoma, juu ya hawa waliomfuata kwa sababu ya ishara na baada ya kulishwa mikate kwa muujiza, mwisho hawakufuatana na Yesu na waliacha kuambatana naye kabisa kwani hawakuwa tayari kulipokea neno lake (Yonana 6).

Walikuwa tayari kula mikate yake ya kimwili, lakini hawakuwa tayari kula neno lake lenye uzima. Watu wanaofuata miujiza mara nyingi wako tayari kula muujiza, ila hawako tayari kula neno la Mungu.

Maandiko yanasema, “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya watashika nyoka; hata kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17).

Miujiza ya Yesu wakati wote INAFUATA neno. Yesu alipowatuma mitume maandiko yanatuambia “Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa” (Luka 9:2).

Neno wakati wote linatangulia kabla ya miujiza kwani chanzo cha imani ni kusikia neno la Kristo (Warumi 10:17). Imani chanzo chake siyo miujiza. Miujiza haifanyi watu wawe na imani bali lile neno walilolisikia. Wana wa Israeli waliishi kwa muujiza miaka 40 lakini hawakumwamini Mungu.

Hivyo Yesu wakati wote, atatanguliza neno, na siyo miujiza. Miujiza itafuata ili kulithibitisha neno. “Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo” (Marko 16:20).

Ndio maana Yesu hakuwa na mikutano ya miujiza ila alitenda miujiza katika mikutano yake (kuna tofauti hapa). Sasa unaweza kuelewa kwa nini mara nyingi Yesu alipofanya muujiza, alionya mtu asitangaze alichofanya.

Ndio maana “huduma ya miujiza” kama huduma inayojitegemea, haipo kwenye Biblia. Watumishi ambao wakati wote msisitizo ni miujiza, wanatumia roho ya mpinga Kristo.

MAONYESHO YA MIUJIZA

Pia kuna watumishi ambao wanafanya “maonyesho ya miujiza.” Watatumia hata TV au njia zingine ili kila mtu aone wanavyofanya miujiza. Ukisoma habari za nabii wa uongo (mnyama kutoka katika nchi), neno linasema,

“Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu” (Ufunuo 13:13). Shetani anapofanya ishara, moja ya nia aliyonayo ni “watu waone” ili wafuate miujiza.

Kitakachojenga imani yako kwa Kristo siyo tu miujiza bali kusikia. Ndio maana kama ishara na miujiza havifanywi kutokana na neno la Mungu linavyosema, hata vikitokea, kusudi lake ni kukuondolea imani yako (Kumbukumbu 13:1—5).

Nikutie moyo kuwa Mungu anaweza kabisa kuwa na muujiza wako lakini usiishi kwa kutafuta muujiza kwani hatuishi kwa miujiza, bali tunaishi kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Mungu (Kumbukumbu 8:3).

Miujiza ni mizuri inapofanywa kwa nguvu za Mungu ili kulithibitisha neno lake. Lakini msisitizo ukiwa kwenye miujiza, hapo ndipo watumishi wataona wanahitaji kufanya miujiza kila mara ili wapate watu.

Huduma ambayo msingi wake ni miujiza na siyo neno, siyo huduma ya Mungu. Umewahi kujiuliza kwa nini mitume waliona Yesu akifanya miujiza ya kila namna lakini walimuomba awafundishe kuomba (Luka 11:1)?

SHETANI KUTUMIA NENO LA MUNGU KUDANGANYA

Kuna viwango tofauti vya udanganyifu ambavyo Shetani anavitumia. Kiwango cha juu kabisa ni pale anapotumia neno la Mungu tofauti na kile Mungu alichomaanisha. Pia anaweza kuongeza/kupunguza neno kwa kusudi la kudanganya.

Hii ndiyo njia aliyoitumia kumdanganya Eva katika bustani ya Edeni. “Nyoka alimwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwanzo 3:4—5).

Nataka uone baadhi ya vitu ambavyo nyoka alisema vilikuwa vya kweli kwamba wakila watafumbuliwa macho na kujua mema na mabaya. Ila pia tunaona aliingiza uongo kwa kusema “hakika hamtakufa.” Shetani alipokuwa anamjaribu Yesu, pia alikuwa anatumia neno la Mungu. Neno linasema:

“Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Mathayo 4:5—6).

Ni kweli kabisa neno linasema, “Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitakaribia hema zako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Zaburi 91:10—12).

Hapa tunaona Shetani akitumia neno tofauti na lilivyomaanisha. Ile kwamba neno linasema atakuagizia malaika wakuchue haina maana ujitupe chini.

Shetani anapotumia maandiko kudanganya watu ni kitu kinachofanywa sana na watumishi wanaohubiri “injili ya pesa.” Kwa mfano, neno linasema ukitii ndipo utabarikiwa (Kumbuku 28:1—13).

Shetani anachofanya anaondoa kile kipengele cha kutii maagizo ya Mungu halafu anakuhubiria kubarikiwa. Matokeo yake inafanya mtu atafute baraka badala ya kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake ndipo abarikiwe (Mathayo 6:33).

Hivyo ukishaona unahubiriwa tu “kubarikiwa,” haijalishi maisha yako yakoje, hufundishwi jinsi ya kumtii Mungu na neno lake ili uyatende mapenzi yake, unajua kabisa hapo Mungu hayupo. Injili wakati wote inatakiwa ichome mioyo ya watu na kuwafanya watu watubu (Mathayo 4:17; Waebrania 4:12).

Ishara na miujiza vinafuata ili kulithibitisha neno la Mungu kwani ufalme wa Mungu uko katika nguvu za Mungu (1 Wakorintho 4:20).

ROHO YA YUDA ISKARIOTE
Kwenye Biblia, kuna watu wawili ambao maandiko yanatuambia Shetani atawaingia. Shetani alimwingia Yuda Iskariote (Luka 22:3; Yohana 13:27). Na baada ya Shetani kutupwa na mahali pake pasionekane tena, atamwingia mpinga Kristo (Ufunuo 12—13).

Baada ya Mariam kutwaa marhamu na kumpaka Yesu miguu, neno linasema:

“Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marham hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye alisema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfumo, akavichukua vilivyotiwa humo” (Yohana 12:4—6).

Hapa tunaona kuwa Yuda alionekana “kujali maskini” lakini kiukweli anatumia maskini kwa faida yake kwani alikuwa mwivi. Hii ni njia ambayo watumishi wa Shetani wanaitumia.

Kuna watumishi wataonekana wanakujali na wanajali matatizo yako, lakini kiukweli ni akina Yuda Iskariote na wanatumia matatizo yako kwa ajili ya faida yao.

Mtu anayekupenda na kujali maisha yako, kitu cha kwanza na cha muhimu atahakikisha una Yesu ndani ndipo vingine vifuate.

SWALI: Utamtambuaje mtu mwenye roho ya Yuda? Yesu ndiye aliwaambia wanafunzi juu ya Yuda Iskariote. Hivyo Yesu pekee ndiye anayeweza kukufunulia hawa watu kwani huwezi kuwatambua kwa kuangalia mavazi yao ya kondoo waliyoyavaa.

MFANO: Ni muhimu kwa mtu anayeamini kutoa sadaka kwa Mungu kwani ndivyo maandiko yanasema. Je mtumishi anapokuhimiza kutoa sadaka, utajuaje kama anakuhimiza kwa sababu anajua sadaka ni muhimu au anatumia maandiko kukuhimiza ili yeye apate pesa?

Utajuaje “nia” inayofanya akuambie anachokuambia? Hapa lazima Yesu mwenyewe akufunulie kama jinsi Yesu alivyomfunua Yuda kuwa ndiye msaliti.

Somo litaendelea… Mungu akubariki,

Jacob & Devota Makaya
Kingdom of Heaven Ministry.

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top