Connect with us

Jinsi ya kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu ya Tano

Mafundisho

Jinsi ya kuwatambua Manabii na Watumishi wa Uongo – Sehemu ya Tano

Bwana Yesu asifiwe,

Leo tutaangalia namna ya kuwatambua watumishi wa uongo kwa kuangalia vipengele vitatu: pesa, kuwekea mikono, na ndoto/maono.

Yesu alisema, “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao” (Mathayo 7:15—16).

Tumeona kuwa watumishi ambao “wamevaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu wakali” si manabii tu bali wachungaji, mitume, walimu, na wainjilisti.

Neno linasema kuna watumishi wanaotoa maono ya mioyo yao (Yeremia 23:16) balada ya uwezo wa Roho Mtakatifu (2 Petro 1:21) na watu wanapenda iwe hivyo (Yeremia 5:31).

Kuwatambua kwa matunda yao ni pamoja na kuangalia “wanavyoliishi neno” na siyo tu “wanavyolihubiri neno.” Kama wanachohubiri hakijawabadilisha wao ili tunda la Roho Mtakatifu (Wagalatia 5:22—23) lionekane katika maisha yao, kwa nini neno lao likubadilishe wewe?

Leo tutaingia ndani zaidi namna ya kuwatambua watumishi wa uongo ili tujitenge nao. Yesu “Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15).

Maagizo ya Yesu ni “kupeleka Injili ulimwenguni” na siyo “kuuleta ulimwengu kwenye Injili.” Katika nyakati hizi, ulimwenguni umeletwa kwenye Injili kwa kiwango kikubwa. Kwa sababu hiyo, badala ya kuwa na “Kanisa” tuna “majengo yaliyojaa wa ulimwengu.”

Badala ya kuwa na “Kanisa lenye kondoo wa Kristo,” sehemu nyingi kuna “majengo yaliyojaa mbuzi.” Neno linasema, Yesu atatenganisha kondoo na mbuzi. Kondoo watapewa ufalme wa Mungu na mbuzi wataenda kwenye adhabu ya milele (Mathayo 25:31—46).

PESA

Kuna njia nyingi ambazo “ulimwengu umeletwa kwenye Injili.” Njia ya kwanza ni pesa. Katika “taasisi za kidini” na kwa “watumishi wa uongo” pesa ni muhimu kuliko Injili. Ndio maana sehemu nyingi watakuhimiza zaidi kutoa sadaka na siyo kumpa Yesu maisha yako.

Ndio maana unaweza kusikia watumishi wakisema “ukiona mtu hakuhimizi kutoa sadaka huyo hakupendi.” Lakini ukweli ni kwamba, “ukiona mtu hakuhimizi kumpa Yesu maisha yako, huyo hakupendi.”

Sadaka ni muhimu baada ya maisha yako kuwa kwa Yesu. Neno linasema, “Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya” (Methali 21:27).

Hivyo kwa Mungu, moyo wako ni muhimu zaidi ya sadaka. Akishapata moyo wako, utamtolea bila kuhimizwa kwani utamjua Mungu unayemtolea.

Hivyo ukiona mtumishi anakuhimiza zaidi kutoa sadaka na siyo wewe kumpa Yesu Maisha, huyo ni “mtumishi wa mshahara.” Yesu alisema, watu wa mshahara kondoo si mali kwao (Yohana 10:12—13). Mtumishi wa Mungu atajali maisha yako ya kiroho kuliko vyote.

Siku hizi watumishi wengi wanaangalia mfuko wako kwanza halafu wanatumia maandiko kupata kilichoko mfukoni mwako. Kutoa sadaka ni muhimu lakini uhusiano wako na Yesu ni muhimu zaidi. Mtoa sadaka mzuri asiye na Yesu ataenda jehanum.

Moja ya swali ambalo nimekuwa najiuliza ndani ya moyo wangu ni hili: “Kama kungekuwa hamna kutoa sadaka, tungekuwa na watumishi wengi kama ilivyo?” Je ni watumishi wangapi bado wana ujasiri wa kuihubiri Injili kama kungekuwa hamna sadaka?

Yesu alisema, hatuwezi kumtumikia Mungu na mali (Luka 16:13). Hivyo ukishaona pesa imepewa kipaumbele kuliko ufalme wa Mungu, hiyo siyo madhabahu ya Mungu au huyo sio mtumishi wa Mungu.

Watumishi wengine wanakwambia utoe kwanza sadaka ndio upate huduma ya kiroho kama maombi. Ukishaona hivyo, ujue hawamtumikii Mungu wa kweli. Hao ni wale ambao neno linasema, “mungu wao ni tumbo” (Wafilipi 3:19).

Mungu wetu hana upendeleo (Warumi 2:11) na hawezi kumhudumia mtu kutokana na hali yake ya kiuchumi. Hivyo ukishaona mambo ya ulimwenguni kama hayo yameingia kanisani, ujue kuna shida mahali.

KUMBUKA: Ulimwengu wakati wote utakuwa vizuri kuyafanya ya ulimwengu kuliko kanisa.

Yesu alisema, “wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru” (Luka 16:8b). Neno linasema, Shetani ni mungu wa dunia hii (2 Wakorintho 4:4). Hivyo kuuleta ulimwengu kanisani maana yake kumleta Shetani kanisani.

KUWEKEA MIKONO

Pia kuwa mwangalifu na watumishi ambao “wanawekea mikono kirahisi.” Kuwekea mikono ilifanywa kwa maagizo kutoka kwa Mungu pekee. Moja ya sababu ya kuwekea mikono ilikuwa “kumpaka mtu mafuta” kwa ajili ya kusudi la Mungu.

“BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mikono” (Hesabu 27:18). Hakuna mtumishi aliyewekea mikono pasipo kuongozwa na Mungu.

Pia watu wanawekewa mikono ili wapokee Roho Mtakatifu (Matendo 8:17; 9:17; 19:6). Watumishi wa Mungu huwa wamebeba “nguvu za Mungu mikononi.” Ndio maana wanaweza kuwekea watu mikono wakapokea Roho Mtakatifu.

Pia wanaweza kuwekea mikono watu wakapona (Luka 4:40; 13:13; Mathayo 8:15). Hivyo kitendo cha kuwekea mikono ni cha muhimu sana kwani ni moja ya njia ambayo mtu anaweza kupokea upako.

Ila “kutoa upako” siyo kazi ya mtumishi bali ni ya Mungu. Hivyo unapoona watu wanafunga safari kwenda Afrika Kusini ili “kuwekewa mikono waongeze upako,” unajua hiyo haitoki kwa Mungu.

Eliya alimwambia Elisha aombe lolote naye atamfanyia kabla hajaondoka. Elisha akaomba upako mara mbili zaidi ya Eliya. Lakini Eliya alimwambia ameomba “neno gumu” kwani alitambua siyo kazi yake kumpa (2 Wafalme 2:9—10).

Paulo alimuonya Timotheo na kusema “Usimwekee mtu mikono kwa haraka” (1 Timotheo 5:22a). Hivyo kuwa mwangalifu na watu ambao wanaenda kila mahali kuwekea mikono. Kabla hujaruhusu mtumishi akuwekee mikono, uwe na uhakika na Mungu anayemtumikia.

Kama jinsi mikono ya watumishi imebeba nguvu za Mungu, mikono ya watumishi wa Shetani imebeba “nguvu za Shetani.” Hivyo ukiwekewa mikono na watumishi wa hivyo, kuna roho zitaenda moja kwa moja kuua nguvu zako za kiroho na kupandikiza roho za Shetani.

Kama ni mfatiliaji unaweza kuona kuna watumishi ambao wananyoshea mikono yao kwa watu halafu watu wanaanguka ovyo. Kwenye Biblia, hatuoni mahali watumishi wa Mungu wakienda kurusha watu ovyo kwa nguvu zilizoko mikononi mwao.

Hivyo unapoona watu wanakuwa wanarushwa ovyo kwa namna hii, hiyo inatakiwa ikuambie kitu. Mtu anaweza kuangushwa kwa nguvu za Mungu au nguvu za Shetani.

Wale watu walioenda kumkata Yesu; Yesu aliwauliza wanamtafuta nani wakajibu “Yesu wa Nazareti.” Neno linasema, “Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini” (Yohana 18:6). Huu ni mfano ambao nguvu za Mungu (Yesu) ziliwaangusha watu.

Ukisoma habari za yule mtu mwenye pepo la kifafa, neno linasema, Yesu “Alipokuwa katika kumwenda, pepo akambwaga chini, akamtia kifafa” (Luka 9:42). Huyu mtu aliangushwa chini kwa nguvu za Shetani.

Kuna namna ambavyo watu huwa wanaangushwa chini wakinyooshewa mkono na watumishi. Kuna watumishi wanapenda kufanya hivi ili ionekane “wana upako.” Hii ni moja ya njia Shetani anaitumia “kudanganya wengi.”

Kibaya ni kwamba watu hawaangushwi tu chini, bali kuna roho ambazo wanazipata zinazokwenda kuua vitu katika maisha yao kwani ndio kazi ya Shetani (Yohana 10:10a).

Hivyo usiwe mwepesi kuwekewa mikono hata kama una matatizo. Hakikisha Mungu amekuongoza kwa mtumishi na amani ya Kristo ndio imeamua ndani ya moyo wako (Wakolosai 3:15a).

Madhara ya kuwekewa mikono na watumishi wa Shetani huwa yanakuwa makubwa kuliko tatizo ulilonalo. Kwa mfano, kwa wanawake wenye mimba, mtumishi wa Shetani akiweka mkono tumboni mwake anaweza kupandikiza kitu cha kipepo kwa mtoto atakayezaliwa pia.

Ukiona unawekewa mikono halafu baada ya hapo, nguvu ya kuomba na kusoma neno hazipo, hiyo inatakiwa ikuambie kitu.

Lakini Mungu bado ana watumishi wake wengi ambao wanawekea watu mikono na wanapokea mambo ya kiroho kutoka kwa Mungu. Shida ni kwamba watumishi wa Shetani ni wengi zaidi, hivyo tunahitaji kuwa na maandiko ili tuweze kutambua kipi kinatokana na Mungu na kipi kinatokana na Shetani.

Katika nyakati hizi za mwisho, lazima uwe mwangalifu kwani neno limeonya kuwa watumishi wa Shetani watadanganya wengi (Mathayo 24:4,5). Shida ni kwamba kuna watu ambao wanawafuata watumishi kwa sababu ya uwezo wao wa kukusanya watu wengi.

Kuna watu wanaangalia ukubwa wa huduma/kanisa kwa kuangalia kiwango cha sadaka zinazokusanywa na idadi ya watu badala ya kuangalia idadi ya watu “wanaofanywa kuwa wanafunzi wa Yesu.”

Mtumishi wa kweli yuko tayari kuihubiri Injili ya kweli kwa watu 10 badala ya injili ya uongo kwa watu 1,000.

Kuna watu wanakimbilia kuwekewa mikono kwa sababu wanaona mtumishi fulani anakusanya watu wengi wakidhani huyo ndio ana upako. Tumia maandiko kuzichunguza njia pana na kama hizo roho zinatokana na Mungu (1 Yohana 4:1)

Yesu alisema, njia pana ndiyo inayoenda upotevuni na watu wengi wataingia katika hiyo (Mathayo 7:13).

NJIA YA NDOTO/MAONO

Njia nyingine ambayo Mungu anaitumia ili kuwajulisha watu waweze kuwatambua watumishi wa Shetani ni njia ya ndoto/maono. Neno linasema, Mungu anatumia ndoto kusema na watu (Ayubu 33:14—15).

Moja ya sababu ya Mungu kutumia ndoto ni ili kuokoa watu wasiangamie kwa upanga (Ayubu 33:18). Neno la Mungu ni “upanga.” Lakini neno la Shetani nalo pia ni “upanga.”

Tofauti ni kwamba “Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili” (Waebrania 4:12a).

Hivyo Mungu anaweza kutumia njia ya ndoto ili kutuambia namna ya kutofautisha kati ya panga hizi zikatazo kuwili. Upanga wa Shetani nao ni mkali, na una nguvu, lakini hauko “hai.” Neno la Kristo ndio hai na lina uzima (Yohana 6:63).

Kuna ndoto nyingi ambazo zinaweza kukupa ujumbe juu ya watumishi wa uongo. Nikupe baadhi ya ndoto:

Kuna mtu mmoja aliota ndoto na kumuona nabii mmoja wa uongo ana mapembe mawili. Mtu mwingine alikuwa katika maombi akaonyeshwa nabii mwingine miguu yake ni mkia wa nyoka. Hawa ni manabii walio wa wafuasi wengi kwa jinsi ya mwili.

Binafsi nimewahi kupata ndoto na maono kadhaa ambayo yalinipa ujumbe juu ya baadhi ya watumishi wa uongo. Kuna mtumishi mkubwa Tanzania ambaye niliwahi kuona nyumbani kwake kuna nyoka mkubwa sana mweusi.

Lakini pia mara kwa mara nilikuwa namuota akiwa na sura tofauti. Nilingia kwenye maombi na kumuuliza Mungu na akaanza kunionyesha vitu kadhaa.

Pia niliwahi kupata maono juu ya manabii fulani wakubwa Afrika ambao niliota wana jicho kwenye kipaji cha nyuso zao. Mtu mwingine aliwahi kuona mtumishi mkubwa sana Afrika Kusini ana hilo jicho.

Jicho hilo linaitwa “jicho la Lusifa” na limewekwa nyuma ya dola 1 ya Marekani. Jicho hilo ndilo linawasaidia watumishi wa uongo kuwa na “macho ya rohoni.” Mtumishi aliye na “jicho la Lusifa” anaweza kukuangalia na kufahamu kila kitu juu yako.

Lakini ni muhimu kuelewa kuwa pia Mungu ana watumishi wake ambao wana macho ya rohoni na wanaweza kuona vitu katika ulimwengu wa roho. Kitachotofautisha ni “matunda yao.”

Mtumishi wa Mungu aliyepewa macho ya rohoni atatumia hiyo karama kukusogeza kwa Yesu. Mtumishi wa Shetani mwenye jicho la Lusifa atatumia hilo kukuangamiza pasipo wewe kujua.

Mtu mwingine aliwahi kuota mtumishi fulani mkubwa Tanzania ana nywele za ajabu halafu yuko madhabahuni. Mwingine alimuota mtumishi huyu huyu akiwa madhabahuni amekaa kama mamba na yuko anacheza kipepo.

Ndoto hizi na zingine zinakuambia kitu juu ya watumishi hao, hivyo ukiziota, usipuuzie. Unachotakiwa kufanya ni kuingia kwenye maombi na kuomba Mungu aseme nawe na kukuthibitishia unachoonyeshwa.

NDOTO ZA KUZINI

Ndoto ambazo watu wengi wanaziota ni “ndoto za kuzini.” Ndoto hizi zina tafsiri nyingi kibiblia na kwenye kitabu cha ndoto, nimeziandika kwa upana. Ila tafsiri mojawapo ni kwamba unapewa ujumbe juu ya kitu cha miungu mingine kinachoendelea katika maisha yako.

Neno linasema, wana wa Israeli walikuwa wanazini na miungu. “Basi Israeli akaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu” (Hesabu 25:1).

Biblia imetumia “mke” kama kanisa na “kahaba” kama kanisa la uongo (Ufunuo 18:5). Hosea aliambiwa na Mungu aoe kahaba (Hosea 1:2) na Yusufu alichukua mke Misri (Mwanzo 41:45).

Huu ulikuwa unabii wa Mungu juu ya mataifa (Gentiles) kuwa sehemu ya Kanisa la Kristo. Ila sehemu kubwa Biblia inapotumia kahaba inatuambia kitu juu ya kanisa la uongo na zinaa inahusiana na vitu vya miungu.

Yesu alisema kwa kanisa la Thiatira, “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake” (Ufunuo 2:20—21).

Hivyo unapokuwa unaota ndoto za kuzini, Mungu anaweza kuwa anakupa ujumbe kuwa unazini na miungu kwa jinsi ya rohoni. Kuzini na miungu ni pamoja na kujiunganisha na madhabahu ya Shetani (kwa kujua au kutokujua).

Ndoto za kuzini zina tafsiri kadhaa ila hii ni njia ambayo Mungu anaitumia kukukwambia kuwa roho ya Yezebeli inakufatilia au inafanya kazi katika maisha yako au inafanya kazi katika madhabu fulani. Watu wengi wakiota ndoto hizi wanazikemea na kuzikataa halafu wamemaliza.

Kinachotakiwa ni kuomba ili Mungu akufunulie ni ujumbe upi ambao unapewa. Kwa mfano, mwanamume anaweza kuota anazini na mwanamke asiyemfahamu kwa sababu katika ulimwengu wa roho, ameoa pepo.

Mwingine anaota ndoto anazini na mwanamke asiyemfahamu kwa sababu anapewa ujumbe juu ya madhabahu aliyopo. Unaweza kuona ndoto ni za aina moja ila ujumbe tofauti.

Kuna mtu aliota amelala na mwanamke ambaye alikuwa kama mke wake. Halafu akasikia mtu anagonga nje, akaenda kumfungulia. Alichoshangaa, anamkuta ni mke wake akaanza kushangaa kwani alimuacha kitandani. Alipoangalia chumbani, akaona mke wake hayupo.

Ndipo akatambua kuwa yule aliyekuwa amelala naye ni siyo mke wake. Unaweza kuona katika ndoto hii, Mungu alikuwa anampa ujumbe huyu mtu juu ya kanisa. Alidhani amelala na mke wake kumbe siyo mke wake.

Mungu alikuwa anamuonya na kumwambia uhalisia wa kanisa analosali kuwa siyo lake, bali la Shetani. Kwenye kitabu cha ndoto, ndoto ya zinaa nimeiandika kwa upana ila nilitaka uone Mungu anaweza kukupa ujumbe juu ya kanisa kupitia ndoto za namna hii.

Kuzini kuna tafsiri nyingi sana katika ulimwengu wa roho. Watumishi wa Shetani wanaelewa sana hiki kitu. Kuna nabii mmoja mkubwa sana Afrika na kitu ambacho huwa anafanya ni kulala na wanawake kila anapokwenda.

Kuna dada mmoja alijikuta amezini naye pasipo kutegemea na baada ya hapo, roho za ajabu sana zilianza kumfuatilia. Huyu ni nabii ambaye ana wafuasi wengi sana na wanadhani ni mtumishi wa Mungu. Kitendo cha kuzini ni cha kiroho na kuna watumishi wanatumia hii kupata nguvu zaidi za Shetani.

Ila ni muhimu kuelewa siyo kila ndoto ambayo mtu anayoota anazini ina tafsiri hii. Inategema na kile ambacho Mungu anamwambia mtu kama jinsi ilivyo kwenye ndoto zingine. Kwa mfano, ndoto za kuzaa. Ndoto hizi zinaweza kuwa nzuri au mbaya.

Neno linasema, “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa” (Ufunuo 12:1—2).

Huyu mwanamke anayezungumzia ni Israeli. Yusufu pia aliota ndoto kwamba jua, mwezi na nyota 11 zikimuinamia (Mwanzo 37:9). Yusufu aliota nyota 11 kwani yeye ndiye alikuwa wa 12.

Hivyo katika Ufunuo 12, maandiko yanatuambia juu ya Yesu Kristo ambaye alikuwa anaenda kuzaliwa kwani yeye ndiye wa kuyachunga mataifa kwa fimbo ya chuma (Ufunuo 12:5). Yohana alipewa ufunuo juu ya kuzaliwa kwa Yesu.

Hivyo ndoto za kuzaa, zinaweza kuwa zinakuambia juu ya kitu cha kimungu kuzaliwa ndani yako. Lakini pia zinaweza kuwa zinakupa ujumbe tofauti. Kwenye kitabu niliandika ndoto niliyomuota dada mmoja. Niliota ana mimba halafu akazaa katoto kadogo sana.

Huyu ni dada ambaye alikuwa kwenye ndoa zaidi ya mwaka mmoja bila kushika mimba. Niliposhtuka, Roho Mtakatifu akaniambia kuwa yule dada alikuwa akipata mimba zinatoka katika ulimwengu wa roho.

Mungu aliweka msukumo wa kuomba kwa ajili yake na baada ya hapo, akapata mimba. Hii ndoto niliiweka kwenye kitabu na siku chache zimepita tulipata ushuhuda kuna dada ambaye naye alikuwa kwenye ndoa na alikuwa anatafuta mtoto.

Lakini baada ya kuisoma hiyo ndoto kwenye kitabu, akachukua hatua ya kiimani na kuomba Mungu akamfanyie kama yule dada alivyomfanyia. Baada ya hapo, alishika mimba na ataenda kupata mtoto wa kwanza. Kila kitu kinawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23).

TURUDI KWENYE SOMO

Kuna njia nyingi za kuwatambua watumishi wa uongo wanaodanganya watu. Endelea kuomba Mungu akufunulie kwani ukiunganishwa na madhabahu isiyo ya Mungu, madhara yake ni makubwa na itaua kile ambacho Mungu ameweka ndani yako.

Kuna nabii mmoja Tanzania alitokewa na malaika mwenye kwato za mbuzi na baada ya hapo akaanzisha huduma. Alianza kufanya vitu vya ajabu kinyume na maandiko. Unaweza kuona jinsi Shetani anavyoweza kutokea mtu kama malaika wa nuru (2 Wakorintho 11:14).

Mungu akipenda, somo litaendelea…

Mungu akubariki,

Jacob & Devota Makaya
Kingdom of Heaven Ministry

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

More in Mafundisho

To Top