Habari

Tanzania Mama ni Wathamani(Tamani Festival), Asante Mama 2018 Mungu Ibariki TAGOANE, Ibariki Gospo Media

Na Mwandishi wetu,

Mtandao wa wasanii wa Injili na maadili ya utaifa TAGOANE (Tanzania Gospel Artists Network) chini ya Rais wake Dr. Godwin Maimu imetoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kuhusu kufanyika kwa matukio mawili makubwa ikiwa ni pamoja na “Mama ni wathamani” na Tamasha la ” Tamani Festival”.

Akiongea na gospomedia.com Bw. Godwin Maimu amesema kuwa mwezi Juni, 2018 jijini Arusha Taasisi ya TAGOANE inatarajia kufanya matukio hayo mawili makubwa katika kusaidia jamii na taifa kwa ujumla kutambua umuhimu wa mwanamke katika malezi ya vizazi vyetu na kutangaza utalii wa Taifa.

“Kutokana na umuhimu wa Mwanamke(Mama) katika Taifa letu na duniani pote, jamii, kanisa, na familia, Tanzania Gospel Artists Network(TAGOANE) imehamasika kuwa na wazo la tamasha linalolenga kumtukuza Mungu kwa ajili ya zawadi ya mama(Mwanamke) aliyoizawadia dunia. Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Juni 2018 linalenga kufanya mambo yafuatayo.

  1. Kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa kumuumba Mwanamke na kumfanya kuwa “MAMA WATHAMANI” MAMA WA DUNIA NZIMA, ASANTE MAMA. Swali gumu sana la kujiuliza “Dunia ingekuaje bila mama. Hakika Mama ni shujaa.
  2. Kupima Afya/Magonjwa nyemelezi kama saratani, presha, sukari kwa kina mama na matibabu.
  3. Kuchangia utoaji wa damu safi na salama: Dhamira kuu ikiwa ni kuhamasisha Taifa “Kuchangia Damu Salama kwa ajili kuokoa maisha ya Mama na mtoto.
  4. Onyesho la upendo na Uzalendo kwa mama(Mwanamke) wa thamani “Asante MAMA”
  5. Mafunzo stahiki ya kuwajengea wanawake ujasiri kwa shuhuda na mafunzo mbalimbali kuwa wanaweza ikiwamo kukuza uchumi, jamii na malezi bora kwa watoto kwa mustakabali mzima wa familia,  Jamii, Kanisa na Taifa, dunia kwa ujumla.
  6. Maonyesho ya kazi za wanawake(kinamama) za ubunifu na ujasiriamali zinazolenga kupanua wigo wa fursa angavu katika kumkomboa MAMA na adui umaskini.
  7. Mazoezi kwa Afya; Kuhamasisha vijana na wanawake kufanya mazoezi kwa Afya bora.
  8. Kuwa na muda wa pamoja kwa wanafamilia kuonyesha kwa vitendo upendo na uzalendo kwa mama kwa kusema asante mama kwa malezi, elimu, na kujitoa maisha kwa ajili yetu. Hii itajumuisha zawadi maalumu ya MTOTO kwa MAMA.

Tukio hili linaendeleza utamaduni wa mtanzania na kurudisha utu baina yetu kupitia kumtukuza Mungu kwa yale yote aliyotutendea katika maisha yetu ya kilasiku. Utambuzi wa neno la Mungu na hofu ya Mungu inapotawala uzima wa afya na maendeleo yanakuwepo katika jamii nzima na Taifa. – aliongeza Dr. Godwin

Kuhusu tamasha la Tamani Festival Rais wa Tagoane aliiambia blog ya gospomedia.om kuwa:-

“Tamasha la Tamani Festival ni tamasha lenye malengo makubwa ya hamasishaji wa kuenzi utalii wa ndani na vivutio vyake kuanzia ngazi ya familia, kaya hadi Taifa kwa kuzingatia malezi bora ya Mama kuanzia ngazi ya shule, vyuo, na jamii nyinginezo. Hata hivyo kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika, utalii ni sekta yenye mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi na pato la Taifa kwa kupima mafanikio ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake. Hivyo basi “TAMANI FESTIVAL” inalenga kuchochea kwa nguvu zaidi uzalendo, amani na mshikamano, upendo kwa Watanzania ili kuimarisha uzalendo wenye matunda chanya ya kuhamasisha vichocheo vya utajiri ambao ni zawadi na karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mapenzi yake kuijalia nchi yetu(Mama Tanzania) kuwa na neema ya amani, utulivu, umoja na mshikamano ulimwenguni pote.” – alisema

 

Dr. Godwin amesisitiza umuhimu wa kila mtanzania kutambua nafasi ya mama na wanawake wote katika Taifa la Tanzania na dunia kwa ujumla hivyo TAGOANE ikishirikiana na wadau wengine wanatoa nafasi hii ya pekee kwao ili waweze kudhihirisha upendo na uzalendo wao kwa kujitokeza kwa wingi ili Mungu apate kutukuzwa kwa viwango vya juu kwa kutambua heshima na thamani ya mama katika maisha yetu.

gospomedia.com itaendelea kukuletea taarifa zinazojiri kila wakati kwa kadiri zitakavyokuwa zinatolewa na TAGOANE ili upate kufahamu zaidi juu ya matukio haya makubwa yatakayobadilisha mtazamo wa jamii na taifa kwa ujumla.

Like us on facebook >> Gospo Media Follow us on instagram >> @gospomedia

Advertisements
Previous post

Audio: Zile - Wela

Next post

Aina 15 za wanawake wanaoangamiza ulimwengu wa leo