Mafanikio: Fahamu Jinsi ya Kufanikiwa - Sehemu ya Pili - Gospo Media
Connect with us

Mafanikio: Fahamu Jinsi ya Kufanikiwa – Sehemu ya Pili

Uncategorized

Mafanikio: Fahamu Jinsi ya Kufanikiwa – Sehemu ya Pili

Katika somo hili la leo litatusaidia kutatua kitendawili hiki kikubwa  unapoendelea kufuatilia somo hili  Mungu atakusaidia kujua maana hasa ya mafanikio,

Mafanikio ni jambo la kimkakati, mafanikio ni mchakato, mafanikio si jambo la ghafla, mafanikio hayaji kwa bahati,  mafanikio ni jambo linalohitaji maandalizi  katika nyanja zote. Ubora wa mafanikio hutegemea msingi wa mafanikio hayo  watu wengi hupendelea zaidi matokeo bila ya kuwekeza katika msingi utakaoleta matokeo  mazuri.

MOJA YA NGUZO MUHIMU YA JINSI YA KUFANIKIWA NI  MALENGO+MAONO+NDOTO+MIKAKATI

  • Malengo: ni matarajio fulani ambayo mtu amejiwekea ili kuyafikia ndani ya muda fulani kwa mfano mtu anaweza akajiwekea malengo kuwa kabla ya mwaka huu kuisha awe amefanikisha jambo Fulani, malengo huweza kuwa ni ya muda mfupi na pia huweza kuwa ni ya muda mrefu.
  • Mikakati: ni njia mbali mbali ambazo utazitumia kufanikisha malengo uliojiwekea.
  • Maono: ni picha ya utimilifu wa jambo fulani ambayo huwa ndani ya mtu kwa mfano mtu anaweza akawa ana maono ya kuja kumiliki taasisi kubwa ya elimu, kujenga kiwanda au kufanya biashara fulani hivyo akawa na picha ya namna hiyo mfano kama ni taasisi ya elimu picha hiyo itamwonyesha taasisi itakavyokuwa aidha itaajiri watu wangapi? itakuwa na walimu wangapi? italeta tija gani katika jamii?, kama ni kiwanda akawa na hiyo picha ya kiwanda; bidhaa zitakazokuwa zikitengenezwa ukubwa wa kiwanda kitakuwa na idadi ya wafanya kazi wangapi? mfumo wake wa uongozi utakuwaje? Picha hii huwa ndani ya moyo wa mtu  ikiambatana na shauku kubwa ya kuona utimilifu wa jambo hilo n.k
  • Ndoto: hufanana na maono tofauti yake ndogo ni kwamba ndoto ina muonekano wa jambo lisilokuwepo bado, jambo ambalo halijavumbuliwa bado na hata kama limefanyika halikufanyika kwa mtazamo huo ama halikufanyika katika jamii hiyo mfano ndoto inaweza kuwa kubadilisha mfumo fulani ambao umedumu kwa muda mrefu au kupatia ufumbuzi tatizo fulani ambalo limejikita kwa muda mrefu.
  • Kuna wakati maono, malengo au ndoto ya mtu huweza kutokea kutokana na kipaji cha mtu ,uwezo alionao ujuzi au taaluma aliyoipata kwa mfano mtu anaweza akawa na kipaji cha uimbaji na akayajenga maono yake kutokana na kipaji chake mtu huyu anaweza akawa na maono ya kuanzisha taasisi ya kukuza vipaji vya uimbaji ama mtu mwenye taaluma ya ualimu akawa na maono ya kufungua taasisi ya elimu ama daktari akawa na maono ya kujenga hospitali, Japo pia kuna wakati ndoto ya mtu au maono aliyonayo huwa havishaabiani kabisa na muonekano wake au uwezo alionao kwa hiyo sio lazima ndoto au maono yako vitokane na kipaji chako au muonekano wako ama uwezo ulionao.

NGUVU KUBWA YA NDOTO MALENGO NA MAONO YA MTU HAVIMO KATIKA UWEZO WAKE AMA KIPAJI CHAKE AMA MUONEKANO WAKE BALI KATIKA MSUKUMO WA NDANI.

Ndio maana mtu anaweza akawa ni mlemavu lakini akawa na maono ambayo kwa muonekano wa mtu huyo si rahisi lakini  msukumo anaousikia ndani yake unatosha kumfanya atimilize maono hayo kupitia msukumo wake wa ndani. inawezekana kabisa maono yako hayaendani kabisa na jinsi ya muonekano wako na watu unapowaambia jambo hilo wanakucheka kwa sababu hawaoni mfanano  wa jinsi ulivyo nayale unayoamini jambo la muhimu sana ni kuhakikisha unaamini maono yako pia hakikisha msukumo ndani yako haupotei  maana huo ndio uliobeba muelekeo (dira ) ya kukufanya uyafikie na kuyatimiliza maono yako.

Maono na ndoto  ni mambo ambayo yanahitaji hatua kadhaa, ni mchakato unaohitaji muda huwezi kuyafanya yatimie kwa siku moja na ndio maana ili kuyafikia na kuyatimiliza maono na ndoto tulizonazo  tunahitaji kujiwekea malengo ni lazima tuwe na malengo ya muda mfupi na malengo ya muda mrefu pia, Malengo ndiyo hatua za kukusaidia kufikia maono yako.

Mtu yeyote unayetaka kufanikiwa na kuleta tija kwa jamii yako,  ama unatamani kujikwamua kutoka hali uliyonayo kwenda hali nyingine ni lazima uwe na maono ama ndoto, ni lazima ujue Je unataka kuja  kuwa nani, Unataka kufanikiwa kwa viwango gani,unataka kusababisha matokeo gani katika jamii yako ama unatamani kupatia ufumbuzi tatizo gani linaloikumba  jamii.

Maono na ndoto uliyonayo ndiyo dira itakayokuonyesha  njia ya kwenda na kukupa muongozo wa mambo unayotakiwa  kuyafanya na yale usiyopaswa kuyafanya  ukiyaamini maono yako hautaruhusu jambo lolote kuyaharibu.

Maono yatakutengenezea msimamo utakaoongoza maisha yako.

Maono aliyokuwa nayo Yusufu yalimtengenezea msimamo wa maisha hakuwa tayari kukubaliana na jambo lolote lililokuja kwake kuua maono yake. Sasa basi ili ufanikiwe kuyafikia maono yako na kuyatimiliza ni lazima uwe ni mtu mwenye  malengo na lazima ujiwekee mikakati ya kuhakikisha unatimiliza malengo hayo  pia ni lazima uhakikishe malengo unayojiwekea yanakupa hatua zaidi katika kuyatimiliza maono au ndoto uliyo nayo katika maisha.

Kuna wakati malengo yanaweza yakawa hayafanani sana na maono moja kwa moja kwa sababu kuna wakati itakulazimu ufanye jambo fulani ili likupe hatua ya kufikia maono yako kwa mfano mtu anaweza akawa na maono ya kuwekeza kwenye biashara ya madini lakini ili apate mtaji anaweza akawa kwa wakati huo anafanya vitu vingine tofauti vitakavyo muwezesha kupata mtaji wa kufanya hiyo biashara anaweza akaanza kulima au kufuga si kana kwamba ana maono ya kuwa mfugaji au kuwa mkulima ila kwa sababu ufugaji na ukulima vimewekwa kwenye malengo kama hatua ya kumwezesha kutimiliza maono aliyonayo mtu anaweza akawa ana maono ya kufungua kampuni lakini kwa wakati huu ni mfanyakazi wa kampuni fulani kama hatua ya kumfanikisha yeye kuja kuwa na kampuni yake. Japo pia watu wengi wameishia kufanikisha malengo badala ya maono kwa sababu ya kukata tamaa ama kuridhika, Hivyo ni vema kuwa na malengo lakini  malengo haya yanakuwa na tija pale tu  inapokuwa mwisho wa malengo haya ni kufanikisha maono au ndoto yako.

Jambo lingine la msingi katika malengo ni lazima ujifunze kujifanyia tathmini ya malengo uliyojiwekea  na tathmini hii iwekwe kwa makundi mfano tathmini ya wiki tathmini ya mwezi miezi mitatu, sita, mwaka miaka mitatu mitano n.k. Tathmini hii itakusaidia kujua mahali ulipo itakusaidia kujua mafanikio au kushindwa itakusaidia kujua mahali pa kurekebisha pia itakusaidia kujua kasi ya kwenda nayo kwenye jambo unalolifanya kwa mfano mtu amejiwekea malengo kwenye biashara  kwamba kila mwezi awe na mauzo ya milioni mbili  kulingana na malengo hayo aliyojiwekea ni lazima kila mwisho wa mwezi ajifanyie tathmini ya malengo hayo aliyojiwekea na kama hajayafikia hayo malengo katika mwezi husika ni lazina atafute sababu zilizomfanya asifikie malengo hayo na pia ni lazima atathimimi mikakati aliyonayo na kuweka mbinu mpya zitakazomsaidia kuyafikia malengo hayo.

Jambo lingine la muhimu sana kuhusiana na maono na ndoto pamoja  malengo ni kuandika, Jifunze kuandika malengo uliyonayo maono na ndoto  andika pia mikakati uliyonayo kuandika kutakusaidia kupata muda wa  kujikumbusha maono uliyonayo. Mungu alimwambia habakuki iandike njozi hii ijapokawia isubiri kuna siri kubwa sana iliyojificha katika maandishi kwa sabababu ukijua kuwa maono na ndoto yako ndiyo muongozo wa namna maisha yako yanapaswa kuwa hivyo ni lazima yaandikwe ili yasomwe unaposoma unapata nguvu mpya ya kuendelea mbele pia inakusaidia kuyaombea maono yako na pia unapoendelea kujikumbusha maono uliyonayo inakusaidia kujiwekea malengo ambayo hayatakupeleka nje ya maono yako.

Maono au ndoto uliyonayo kuhusu maisha yako ndiyo vimebeba sababu ya wewe kuwepo duniani aidha ndiyo vimebeba kusudi la Mungu kuhusu maisha yako ya hapa duniani.

Inawezekana haujajua maono yako Muombe Mungu akusaidie kujua na akupe msukumo wa ndani kuhusiana na jambo hilo Maana ni Mungu pekee ndiye anayejua sababu ya kukuumba na kukuweka duniani. Itaendelea….

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Emmanuel Mwakyembe kupitia:
Simu/WhatsApp: +255 716 531 353 au +255 753 361 141
Facebook Profile: Emmanuel Mwakyembe
Istagram: @oficial-mryopace
Email: emamwakyembe@gmail.com

More in Uncategorized

To Top